24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

TFF INAPOJIVUA GAMBA UDANGANYIFU UMRI WA WACHEZAJI

jamal-malinzi-640x425

Na ADAM MKWEPU-DAR ES SALAAM

ULIMWENGU wa soka umeshuhudia mengi ya kusikitisha na mengine ya kuburudisha, hasa baada ya dakika 90 za uwanjani.

Kuna wakati mwingine mchezo wa soka huitwa wa maajabu kutokana na kile kinachotokea ndani ya uwanja.

Kwani ndio mwanzo wa kuibuka kwa mambo mbalimbali yanayohusu soka yakiwamo upangaji matokeo, kubebwa na waamuzi, umri mkubwa na kushuka kiwango.

Jambo kubwa linalopigiwa kelele kwa sasa ni umri mkubwa kwa wachezaji, hasa wanaotoka barani Afrika.

Wachezaji wa soka kutoka Afrika, wamekuwa na sifa ya udanganyifu wa umri ili kupata nafasi ya kucheza soka barani Ulaya.

Mbali ya kucheza Ulaya, tabia hiyo imekuwa ikifanyika hata katika michuano ya ndani inayoendelea Afrika.

Ukweli wa jambo hilo umejitokeza kwenye ligi ya vijana  wenye umri chini ya miaka 20, iliyomalizika hivi karibuni kwa timu ya vijana ya Simba kuibuka mabingwa.

Ligi hiyo ambayo ilichezwa kwa takribani wiki tatu, ilighubikwa na malalamiko ya udanganyifu wa umri wa wachezaji kila kona.

Kutokana na malalamiko hayo wengine waliondoa maana ya uwepo wake kwani waliona ni jambo la ajabu  kuwapo kwa vitendo hivyo.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limekuwa likikemea tabia za viongozi wa klabu za soka nchini, kudanganya umri  wa wachezaji, badala ya  kuwa na maono ya mbali ya kuhakikisha wanakuza vipaji vya wachezaji chipukizi katika klabu zao.

Katibu Mkuu wa TFF, Celestine Mwesigwa, anasema kuwa klabu zinatakiwa kutekeleza ipasavyo jukumu la kupima umri wa wachezaji kabla ya kuwasajili wachezaji wao ili kuepusha udanganyifu wa umri katika michuano mbalimbali nchini.

“Udhibiti wa umri upo katika ngazi tofauti kwa kuwa klabu ndio yenye jukumu kubwa la kuhakikisha wachezaji wao kabla ya kushiriki ligi au mashindano yoyote nchini wanahakikiwa umri.

“Hata hivyo, katika kutekeleza jukumu hilo, klabu hutofautiana katika kutekeleza utaratibu huo kutokana na gharama za upimaji wa kila mchezaji kuwa kubwa,” anasema Mwesigwa.

Mwesigwa anasema kuwa licha ya jitihada za udhibiti kufanyika kwa kiasi kikubwa, klabu zinatakiwa kutekeleza jukumu hilo ili kuepusha migogoro ya udanganyifu wa umri dhidi ya klabu nyingine.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi  wa Mashindano TFF, Jemedar Saidi, anaeleza kuwa TFF haina jukumu la kuhakiki umri wa wachezaji.

“Mbali na siasa za soka zinazoendelea, lakini TFF si jukumu lake kuhakiki umri wa wachezaji na kuwa na vituo vya kukuzia vijana kwani kazi hiyo hufanywa na klabu.

“Klabu nyingi zinakimbia majukumu ya kupima wachezaji wao na kuitupia lawama TFF ambao hawana mchezaji,” anasema Said.

Said anaeleza kuwa klabu nyingi hudanganya umri kwa kuwa hazina mpango wa kukuza maendeleo ya soka, bali kupata ushindi wa muda mfupi na baadaye hupotea katika medani ya soka nchini.

“Klabu ndio wanatakiwa kupokea  vielelezo vyote vya mchezaji kabla ya kumsajili, hivyo wanatakiwa kujiridhisha kwanza kutokana na vigezo vinavyotakiwa kabla ya kuanza kuilamu TFF.

“Viongozi wa klabu hujidanganya wenyewe bila kujitambua, kwani hujiingiza katika hatari ya kufutiwa matokeo hata kushushwa daraja kutokana na vitendo hivyo wakati wanapogundulika wamefanya udanganyifu,” anasema Said.

Said anasema tabia hiyo ndio sababu ya  timu za Tanzania kushindwa kufanya vizuri Ulaya hasa kwenye michuano ya wakubwa.

“Afrika katika timu za vijana tunafanya vizuri kutokana na kutodanganya umri, lakini katika timu za wakubwa tunaambulia ziro,” anasema Saidi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles