30 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 26, 2023

Contact us: [email protected]

SIMBA HIYOO KILELENI

simba-640x388-gud

NA WAANDISHI WETU

TIMU ya soka ya Simba imeendeleza ubabe katika michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara, baada ya jana kuchomoza na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Ndanda FC na kurejea kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo kwa kishindo.

Mchezo wa jana ambao ulikuwa wa kwanza kwa Simba katika mzunguko wa pili wa ligi, ulichezwa katika Uwanja wa Nangwanda Sijaona, Mtwara, ambapo matokeo hayo yaliwawezesha kufikisha pointi 38.

Katika mchezo huo, Simba iliwatumia nyota wapya waliosajiliwa katika dirisha dogo, kipa Daniel Agyei na kiungo James Kotei, wote kutoka Ghana na kufanikiwa kuwashusha kileleni mahasimu wao Yanga waliojikusanyia pointi 36.

Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu, Yanga, walifanikiwa kushika usukani kwa muda baada ya juzi kuwachapa maafande wa JKT Ruvu mabao 3-0 katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.

Simba walianza mchezo kwa kasi ambapo dakika ya tisa mshambuliaji, Javier Bukungu, alikosa bao la wazi baada ya kushindwa kuunganisha vyema pasi ya Ibrahim Ajib akiwa nje kidogo ya eneo la hatari.

Hata hivyo, kutokana na kasi kubwa ya mchezo kocha wa Simba, Joseph Omog, alilazimika kufanya mabadiliko ya kumtoa Kotei dakika ya 19 kipindi cha kwanza na nafasi yake kuchukuliwa na Mzamiru Yassin.

Dakika ya 21, Ndanda walicharuka na kufanya shambulizi kali kupitia kwa Salum Mineli ambaye aliunganisha krosi iliyopigwa na Paul Ngalema akiwa ndani ya eneo la 18, lakini shuti lake lilitoka nje ya lango.

Simba ilipata bao la kuongoza dakika ya 63 kipindi cha pili kupitia kwa Yassin ambaye alipokea pasi safi iliyopigwa na Shiza Kichuya aliyekuwa umbali wa mita chache kutoka katika lango la Ndanda.

Wakati Ndanda wakitafuta mbinu za kusawazisha bao hilo, walijikuta wakifungwa bao la pili dakika ya 81 na Mohamed Ibrahim ambaye aliwanyanyua mashabiki wa Simba waliojitokeza kushuhudia mchezo huo.

Kwa upande wao Azam FC walianza duru ya pili ya ligi kwa kusuasua baada ya kulazimishwa sare ya bila kufungana na African Lyon katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Azam Complex uliopo Chamanzi, Dar es Salaam.

Matokeo hayo yameiwezesha Azam kufikisha pointi 26 huku ikiendelea kushika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi.

Mchezo mwingine wa ligi hiyo ulichezwa katika Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, ambapo wenyeji Mbao FC waliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Stand United ya Shinyanga.

Maafande wa Tanzania Prisons walifanikiwa kufikisha pointi 22 baada ya kuichapa Majimaji FC bao 1-0 katika Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,726FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles