SAMATTA WAPE ‘KIZIZI’ CHA MAENDELEO NGASSA, LUIZIO

0
1529

samatta-mbwana-640x640

Na ZAINAB IDDY

WAKATI Watanzani hususani wadau wa soka wakipiga kelele kutaka soka la Tanzania likue angalau tuweze kupata kikosi bora cha kwanza cha wanandinga wanaocheza soka la kulipwa, hali inaonekana kwenda kinyume baada ya baadhi ya wachezaji kurejea nyumbani kusakata kabumbu.

Hadi sasa Mtanzania anayepeperusha bendera kimataifa na kutufanya tutembee kifua mbele ni straika anayekipiga katika klabu ya Genk ya Ubelgiji, Mbwana Samatta pekee, shukrani kwake.

Tunajua zipo changamoto nyingi amepitia hadi kufika pale alipo sasa, lakini yapo maswali mengi yanayozunguka katika vichwa vya wadau wengi nchini.

Kwanini Samatta peke yake, je, miguu yake kuna kitu amefunga kinachomtofautisha na wanandinga wengine wazawa au kuna kamzizi alichopewa na babu ambacho ameshindwa kuwagawia na wenzake angalau Watanzania wakajisifia kwa kuhesabu orodha ndefu ya wachezaji wanaoitangaza nchi kwenye soka la kulipwa.

Tunajua wapo Watanzania wengi wanaocheza soka nje, lakini shida ni hawana wanachofanya kiasi cha kuushawishi umma utambue au Watanzania wenyewe kutembea wakiimba majina yao kama ilivyokuwa kwa Samatta mtoto wa Mbagala.

Wakati tukihangaika na kina Simon Msuva, Farid Mussa na John Bocco, wanaoishia kufanya majaribio tu, mara Mrisho Ngassa na Juma Luizio wamerejea kuongeza idadi ya vipofu nchini.

Luizio aliondoka Tanzania miaka miwili iliyopita, baada ya kusajiliwa na Zesco United ya Zambia akitokea Mtibwa Sugar, lakini hivi sasa yupo nchini akiwa na kikosi cha Simba, tena ikielezwa amejiunga kwa mkopo huku Ngassa naye akirejea kujiunga na Mbeya City, japo haijafahamika amekuja katika mazingira yapi, je, kwa mkopo kama Luizio au amevunja mkataba na Fanja FC ya Oman kama alivyofanya awali kwa Free State ya Afrika Kusini?

Hapo ndipo panapochanganya na kufanya watu kumgeukia Samattta, kisha kujikuta wakijihoji wenyewe pasipo majibu.

Je, Samatta anakipi miguuni mwake tofauti na wengine? Ni juhudi, heshima kuwa na malengo ya mbele au kuna kimzizi kinachomsaidia kufika anapotaka? Au tuseme wachezaji wetu hawana mawazo endelevu.

Kipi tatizo, kwani haiwezekani kuona familia moja inajenga nyuma, lakini ghafla miongoni mwao wajenzi waamue kuibomoa, au kile kitu kinachoitwa ‘ndumba’ kinachotumika sana na wachezaji kinawamaliza hata wale wanaocheza soka la kulipwa.

Je, mahali alipokuwa Ngassa Afrika Kusini na kule Zambia kwa Luizio nako kuna mafundi wa kupigana ‘misumari’ iliyosababisha washindwe kusonga mbele na badala yake waamue kurudi nyuma.

Chonde Samatta, wape basi Ngassa na Luizio hicho ‘kimzizi’ chako waweze kupigana kwenda mbele na si kurudi walipotoka.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here