23.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, April 16, 2024

Contact us: [email protected]

TEVEZ ANASHINDWA KULINDA THAMANI YAKE CHINA

NA BADI MCHOMOLO


DESEMBA 29 mwaka jana, nyota wa soka nchini Argentina, Carlos Tevez, alitikisa dunia baada ya kusajiliwa kwa kiasi kikubwa cha fedha ndani ya klabu ya Shanghai Shenhua ya nchini China akitokea Boca Juniors.

Mchezaji huyo alisaini mkataba wa kuitumikia Shanghai Shenhua kwa miaka miwili na mshahara wake kwa wiki ukitajwa kuwa pauni 615,000, ambazo ni sawa na 1,835,560,000 za kitanzania.

Alisaini mkataba huo akiwa na umri wa miaka 32, wengi walishangaa huku wakiamini kwamba umri huo ni mkubwa sana hivyo hawezi kucheza soka kwa muda mrefu baadae, lakini angekuwa na umri chini ya miaka 25 wasingeshangaa sana.

Klabu ya Shanghai Shenhua iliamua kuingia kwenye biashara hiyo kwa kuonesha jeuri ya fedha, lakini walikosea kwa aina ya mchezaji waliyemchagua. Ni wazi ingekuwa ngumu kwa mchezaji yeyote kukataa kiasi hicho cha fedha, hivyo ni vizuri wangeangalia mchezaji mwenye damu changa.

Tevez hadi sasa ni mchezaji anayeongoza duniani kwa kulipwa fedha nyingi kwa wiki katika klabu, lakini tayari umri wake unaanza kumuumbua na anashindwa kulinda thamani yake ndani ya klabu hiyo pamoja na duniani kwa ujumla.

Wengi macho yalikuwa kwake kuangalia atafanya nini ndani ya kipindi cha miaka miwili alichosaini huku China, lakini hadi sasa mchango wake umekuwa mdogo sana tofauti na thamani yake, tangu ajiunge hadi sasa amefanikiwa kufunga mabao manne kwenye Ligi Kuu, hakiwa kama mshambuliaji ni wazi idadi ndogo ya mabao.

Mbali na kuwa na ukame wa mabao bado wachina hao walionesha nia ya kutaka kumuongezea mkataba mpya na kumfanya achukua pauni 650,000 kwa wiki, lakini bado mchezaji huyo anashindwa kuwashawishi mabosi hao kumpa mkataba mwingine.

Ni wazi umri wake unapunguza thamani yake kwa kuwa mwili unashindwa kufanya vitu ambavyo wachezaji wenye umri mdogo kama vile Neymar, lakini akili inataka, kitu ambacho kinaanza kumshushia thamani yake ni majeruhi.

Mchezaji huyo amekuwa nje ya uwanja tangu mwezi uliopita kutokana na majeruhi, lakini timu yake iliweza kupambana mwezi huo na kufanikiwa kutwaa taji la Kombe la FA. Mchezaji huyo aliamua kuwaaga viongozi wa timu hiyo na kuwaambia kwamba anarudi nchini Argentina kwa ajili ya kujiangalizia majeruhi yake ya mguu.

Mabosi wa Shanghai Shenhua, wameanza kujawa na wasi wasi juu ya mchezaji huyo kuendelea kukaa huko Argentina kwa muda mrefu huku wakiamini kuwa tayari amepona lakini anaamua kuendelea kukaa nchini humo.

Awali walimwambia atumie muda mchache wa kupumzika nchini Argentina na muda unaobaki anatakiwa kuwa nchini China kwa ajili ya kuendelea na matibabu chini ya madaktari wa klabu hiyo, lakini Tevez hadi sasa haoneshi dalili yoyote ya kurudi China.

Kutokana na hali hiyo viongozi wa Shanghai Shenhua wameweka wazi kuwa wameanza kumshangaa mchezaji huyo huku mashabiki wake wakidai thamani ya mchezaji huyo inazidi kushuka kutokana na mchango wake kuwa mdogo.

Hata hivyo viongozi hao wamemtumia ujumbe mchezaji huyo kwamba wanampa wiki tatu za kukaa nchini Argentina, hivyo hadi kufikia Desemba 26 anatakiwa kuripoti kwenye klabu hiyo.

Wamesema endapo hadi kufikia tarehe hiyo atakuwa hajawasili ndani ya klabu hiyo basi atachukuliwa hatua na wanaweza kufikia maamuzi ya kurudishwa kwenye klabu yake ya zamani ya Boca Juniors.

Baadhi ya mashabiki wa klabu ya Shanghai Shenhua, wameamua kumpa jina la utani mchezaji huyo likijulikana kama ‘Very Homesick Boy’ kutokana na tabia yake ya kuugua mara kwa mara na kutengeneza safari za nyumbani kwake Argentina, kitendo hicho kinamfanya mchezaji huyo kushuka thamani na kushindwa kulinda heshima yake.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles