27.7 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 21, 2024

Contact us: [email protected]

TEMDO yawekeza zaidi ya bilioni tatu kutatua changamoto ya vifaa tiba nchini

Safina Sarwatt, Arusha

Taasisi ya Uhandisi na Usanifu Mitambo ya Temdo Tanzania (TEMDO) imewekeza zaidi ya bilion tatu kutatua tatizo la uhaba wa vifaa tiba nchini.

Akizungumza mwishoni mwa wiki jijini Arusha katika mafunzo kwa Waandishi wa Habari kutoka Kanda ya Kaskazini na kuratibiwa na tume ya taifa ya Sayansi Teknolojia na Ubunifuni (COSTECH), Mkuu wa Kitengo cha mawasiliano na masoko kutoka TEMDO, Dk. Sigisbert Mmasi amesema tayari taasisi hiyo imeweka mikakati mbalimbali kuhakikisha kuwa inazalisha vifaa vya kutosha.

Amesema katika kipindi cha mwaka 2021/2022 taasisi hiyo imewekeza zaidi ya shilingi bilion 3 kwa ajili karakana ya kisasa ya kutengeneza vifaa tiba aina 17 ambapo mpaka sasa vifaa tiba aina saba (7) vimeanza kuzalishwa.

Amesema vifaa hivyo ni pamoja vitanda vya wodi ya wajawazito, stendi za kuwekea drip, vitanda vya wagonjwa kufanyiwa uchunguzi pamoja na vitanda vya wagonjwa wanaolazwa Hospitalini.

Amesema karakana hiyo kwa sasa inauwezo wa kutengeneza vitanda zaidi ya 500 vya wajawazito na vitanda na vya wagonjwa wanaolazwa mahospitalini.

“Taasisi yetu pia tunazalisha majokovu ya kuhifadhia maiti, pia tunategeneza viteketeza taka za mahospitali, hivyo tunakaribisha wadau wa afya na wamiliki wa hospitali binafsi na Serikali kununua vifaa tiba katika taasisi hiyo,” amesema Dk. Mmasi.

Sehemu ya waandishi wa habari

Dk. Mmasi ameishauri serikali kuzielekeza taasisi zake kununua vifaa tiba katika taasisi hiyo kutokana na ubora ili kupunguza gharama kubwa ya kuagiza vifaa hivyo nje ya nchi.

Amesema TEMDO kwa zaidi ya miaka 30 wametengeneza mashine za aina mbalimbali za kilimo, viwandani pamoja na kutoa elimu kwa wahandisi na mafundi uchundo nchini.

Akizungumza upande wa sekta ya kilimo amesema wamezalisha mashine aina mbalimbali za kutengeneza juisi za aina mbalimbali, mashine kutengeneza siagi ya karanga, mashine za kutengeneza unga wa lishe aina zote na mashine za kutengeneze viungo vya vyakula.

Amesema taasisi hiyo pia wanatengeneza mashine za kutengeneza mkaa kwa kutumia mabaki ya mimea, maganda ya karanga na mashudu ya mpunga lengo likiwa ni kukabiliana na changamoto ya uharibifu wa mazingira.

Kwa upande wa sekta ya madini, amesema taasisi imeweza kutengeneza vifaa kwa ajili ya wachimbaji vya kupandishia udongo kutoka migodini kwa ajili ya kuutoa nje ya shimo.

“Taasisi hiyo imegusa sekta zote muhimu hapa nchini, hivyo nitoe rai kwa jamii kutumia tafiti za wataalamu ili kufikia malengo makubwa na kukuza uchumi,” amesema Dk. Mmasi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
583,000SubscribersSubscribe

Latest Articles