Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
SERIKALI inatarajiwa kujenga maabara ya kisasa ya matumizi ya teknolojia ya vinasaba ya kuboresha mbegu za mimba za ng’ombe (embryo transfer).
Taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu ilisema jana kuwa maabara hiyo ya kisasa itajengwa katika Ranchi ya Mzeli mkoani Tanga na kampuni ya Overland Livestock Multiplication Unit and Embryo Transfer kwa kutumia teknolojia kutoka New Zealand na kwa kushirikiana na Kampuni ya Taifa ya Ranchi (NARCO).
Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Feisal Edha akifuatana Waziri wa Mifungo na Uvuvi, Dk. Titus Kamani, mtaalam kutoka New Zealand na baadhi ya wajumbe wa Bodi ya NARCO alimwambia Rais Kikwete mjini Dodoma kuwa maandalizi yote yamekamilika kwa ajili ya ujenzi wa maabara hiyo.
Alisema maabara hiyo itakuwa ya pili ya aina yake Afrika Mashariki.
Maabara hiyo inawezesha ng’ombe bora mama bandia (surrogate mother) kupokea mbegu bora kutoka kwa ng’ombe bora mfadhili (donor) na kumlea hadi kutoa ndama wa kisasa ambao wanazaliwa kwa wingi kulingana na idadi ya ng’ombe mama bandia ambao wanaweza kuuzwa kwa wananchi.
Feisal alimwambia Rais Kikwete kuwa kwa kawaida ng’ombe huzaa ndama 13 katika maisha yake ya wastani wa miaka 13 hadi 16 lakini kwa kutumia teknolojia hiyo, ng’ombe anaweza kutoa mayai 126 kwa mwaka ambayo yanaweza kupandikizwa ng’ombe mama bandia kwa wakati mmoja baada ya ng’ombe hao kuingizwa katika joto.
Alisema teknolojia hiyo inamwezesha mfugaji kuchagua kwa uhakika zaidi anataka kuzalisha ng’ombe wa namna gani – wa maziwa, wa nyama, dume au jike na kwamba teknolojia hiyo pia ni bora zaidi kuliko ile ya uhamilishaji ambayo ndiyo imeanza kutumika nchini kwa sasa.
Mkurugenzi huo alisema kwa mujibu wa makubaliano na wabia wake wa New Zealand, watanzania watapelekwa kusomea teknolojia hiyo nchini humo na nchi hiyo imekubali kuipa Tanzania teknolojia hiyo moja kwa moja.
Feisal alisema asilimia ya maboresho yote ya ng’ombe na sekta hiyo duniani inatumia teknolojia hiyo kwa sasa.
Rais Kikwete alionyeshwa kufurahishwa kwake na hatua hiyo akisisitiza kuwa amekuwa akielekeza kuhusu umuhimu wa kuleta mageuzi katika ng’ombe na mifugo ya Tanzania kwa miaka yote ya uongozi wake.
“Nimewapenda na kuwaamini watu wetu wa mifugo lakini hakuna jambo la maana wamefanya katika muda wote. Nakushukuru Feisal kwa uamuzi wako huu na nataka kukuhakikishia kuwa kama watu wetu wanakuzungusha, wewe endelea tu na mimi niko yatari kukusaidia,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:
“Nimefurahi kusikia habari hii sasa nyie endeleeni na mipango yetu ya ujenzi wa maabara, msiingie kwenye urasimu wa hawa watu wetu. Msikubali wawababaishe kwa sababu kama hawa watu wa wizara ama NARCO hawako tayari kusonga mbele nyie endeleeni tu, wacha wao waendelee to run around in circles.”