29.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

Tecno yaunga mkono mashindano ya Umisseta, Umitashumta Mwanza

Na Mwandishi Wetu, Mwanza

HALMASHAURI ya Jiji la Mwanza imefungua rasmi msimu wa mashindano ya michezo kwa shule za Sekondari (Umisseta) na Msingi (Umitashumta) mwaka 2024, huku kampuni ya simu ya Tecno ikiunga mkono kwa kusaidia vifaa vya michezo kwa wanafunzi.

Wanafunzi wa shule za sekondari Alliance (jezi ya bluu) na Pamba (jezi ya kijani) wakipokea vifaa vya michezo leo katika hafla ya uzinduzi wa msimu wa mashindano ya Umitashumta na Umisseta mwaka 2024 kwenye Uwanja wa Mirongo jijini Mwanza.

Mashindano hayo yamefunguliwa leo Jumanne Machi 12, 2024 katika viwanja vya Mirongo jijini Mwanza na Kaimu Afisa Elimu Sekondari halmashauri ya jiji hilo, Bertha Donald ambaye ametoa wito kwa walimu kuzingatia ratiba iliyowekwa ya mashindano hayo ili iende sambamba na ile ya kitaifa na kuhitimisha katika muda uliopangwa.

Jumla ya shule 156 za msingi na 65 za Sekondari wilaya ya Nyamagana zitashiriki katika michezo mbalimbali ikiwemo soka, netiboli, kikapu, wavu, mikono, riadha na mingine kuanzia ngazi ya shule, kata na wilaya kupata timu ya halmashauri hiyo itakayoshindana ngazi ya mkoa.

“Tuwasaidie wanafunzi wetu kwa kuibua vipaji vyao na wale walio na vipaji tayari tuwaendeleze, kuwafundisha na kuwasaidia watimize ndoto zao, niwaombe walimu wa michezo tukitoka hapa tusibweteke tuanze michezo hii ngazi za shule na tutengeneze ratiba tutakayoifuata,” amesema Bertha.

Meneja wa kampuni ya Tecno Kanda ya Ziwa ambayo imetoa jozi zaidi ya 100 za viatu, Edward Mathias, amesema wameamua kuunga mkono michezo ngazi ya chini kwa kusaidia viatu vya kuchezea soka kwa wanafunzi ili watimize ndoto zao huku akiongeza kwamba hatua hiyo itakuwa ni mwendelezo ambapo wataifikia mikoa yote ya Kanda ya Ziwa na Kigoma.

“Kupitia program yetu ya ‘boost kipaji’ ambayo tuliianza wakati wa mashindano ya Afcon tumeamua kuweka nguvu tumeangalia vipaji ngazi ya chini shuleni ambako watoto hawana uwezo wa kupata vifaa vya michezo. Tunatoa ombi kwa walimu na wazazi kununua bidhaa zetu kuisaidia watoto wetu na wanafunzi kupata maendeleo kwenye vifaa vya michezo.

“Watoto wengi wanapenda michezo lakini hawana uwezo wa kununua vifaa vya michezo tumeanza na eneo la viatu kuwawezesha wanafunzi wetu wacheze mpira wakiwa wamevaa viatu lakini vijana wetu wengi hawana soksi hawana jezi, tumeanza na vifaa lakini tutaenda mbali kwa kuweka nguvu katika kuboresha miundombinu ya kuchezea,” amesema Mathias

Akizungumzia mashindano hayo kwa niaba ya Mkurugenzi wa halmashauri ya jiji la Mwanza, Kaimu Afisa Michezo na Utamaduni wa halmashauri hiyo, Agnes Majinge, amewapongeza Tecno ambao wametoa pea zaidi ya 100 za viatu vya kuchezea mpira wa miguu na taasisi ya Sport Charity ambayo imetoa mipira zaidi ya 200 kwa shule zote za jiji hilo.

“Lengo kubwa ni kutoa hamasa kwa walimu wa michezo shuleni kuibua michezo kwa ngazi ya darasa mpaka mkoa, tunashukuru tumepata wadau mbalimbali ambao wametuunga mkono viatu pea zaidi ya 100 na mipira zaidi ya 200 na tunatoa wito kwa watoto, wazazi na walimu wahakikishe watoto wote wanashiriki michezo hii,” amesema Majinge na kuongeza kuwa:

“Tunatarajia baada ya uzinduzi huu tutaona michezo ikiendelea kwa ngazi ya madarasa, shule, kata na baadaye ngazi ya wilaya ili kupata timu za wilaya zitakazotuwakilisha mkoani na hatimaye kwenye ngazi ya taifa mkoani Tabora,” amesema afisa huyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles