Na DERICK MILTON-BARIADI
NAIBU wa Waziri wa Kilimo na Ushirika, Innocent Bashungwa, ametoa muda wa siku tatu kuanzia Novemba 6, mwaka huu kwa Bodi ya Pamba Tanzania (TCB), kuhakikisha kila mkulima wa zao hilo mkoani Simiyu anapata mbegu za kutosha.
Pia alimtaka Meneja wa TCB Kanda ya Ziwa, Jones Bwahama, kubaki mkoani Simiyu baada ya ziara yake ya siku mbili mkoani humo kuhakikisha kila mkulima anapata mbegu za pamba kwa ajili ya msimu mpya wa kilimo.
Agizo hilo alilitoa Jumatano wiki hii katika Kijiji cha Kilalo wilayani Bariadi baada ya kukutana na malalamiko ya wakulima wa pamba kutopatiwa mbegu za kutosha kutoka bodi ya zao hilo wakati tayari msimu wa kilimo umeanza.
Mwakilishi wa wakulima hao, John Athuman, alimweleza Bashungwa kuwa wakulima wanapatiwa mbegu chache kulingana na mahitaji yao halisi na wengine kukosa kabisa.
Wakulima hao walisema wanapatiwa kilo 20 za mbegu zinazotosha katika shamba lenye hekari mbili, huku baadhi yao mahitaji yakiwa kilo 50 kutokana na kuwa na eneo kubwa la kulima zao hilo.
“Tatizo letu kwa sasa ni mbegu, hazipatikani kwa wakati, tunapewa chache, mimi nimepata kilo 15 lakini mahitaji ni 50, mwaka huu tumeangaika, tunaomba mbegu,” alisema mmoja wa wakulima hao, Masunga Jacob.