Na Clara Matimo, Mwanza
Katika kuhakikisha wanawake nchini wanashiriki kujenga na kuinua uchumi wao na taifa, Benki ya Biashara Tanzania (TCB) imewakutanisha wanawake zaidi ya 300 Mkoani Mwanza na kuwapa elimu ya biashara itakayowasaidia kuzitambua fursa za kibenki kwa ajili ya maendeleo.
TCB imelikutanisha kundi hilo ikiwa ni mwendelezo wa kongamano la wanawake na biashara ambalo ililizundua mwanzoni mwa mwezi huu jijini Dodoma mada yake kuu ikiwa ni ‘Nafasi ya Mwanamke katika kukuza Uchumi wa Taifa’ lililolenga kubainisha mahitaji maalumu ya kifedha ya wanawake na kuwapa fursa kujifunza mambo mbalimbali pia kuijua benki hiyo na huduma zake.
Akizungumza jijini Mwanza leo katika kongamano hilo, Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa TCB, Moses Mnyatta, amesema pamoja na changamoto nyingi za kifedha walizonazo wanawake watahakikisha ajenda ya kuwawezesha kiuchumi inafikia malengo yaliyokusudiwa kwa kuwaonyesha fursa walizonazo na kuwaelimisha jinsi ya kufanya biashara zenye tija.
Mnyatta amesema TCB imejiandaa vizuri kwa hilo kwani ina fursa lukuki za kibiashara na uwezeshaji kupitia huduma maalumu kama akaunti ya Tabasamu na na suluhishi mbalimbali kama bima ya nishike mkono na kinamama sera pia iko imara kifedha , hodari wa kidijitali, bingwa wa ubunifu, wigo mpana wa huduma na mtandao mkubwa wa kuzifikisha popote kwa wakati.
“Tuna mtandao wa matawi makubwa 46, madogo 36, ofisi za wakala za shirika la posta Tanzania 120, ATM 84 ambazo zimeunganishwa na ATM 350 za mtandao wa Umoja Switch hivyo itakuwa rahisi kuwafikia wanawake wengi na kusaidia kuwawezesha kupitia matawi na vituo vyetu vya huduma vilivyosambaa Tanzania bara na visiwani.
Mafanikio ya jitihada hizi yatatokana na mpango mkakati tulionao TCB wa kufanya mapinduzi makubwa ya kuwahudumia wanawake, tutatekeleza jukumu hili adhimu kwa kuwa kinara wa huduma jumuishi za kifedha za akina mama na kiongozi mbunifu wa huduma hizo sokoni hili linawezekana kwani mwaka 2007 hadi 2020 mikopo imeongezeka kwa zaidi ya Sh bilioni 580 hadi sasa wanawake ambao ni nusu ya wateja wetu milioni moja tumeishawakopesha zaidi ya Sh bilioni 120 ,”amebainisha Mnyatta.
Mgeni rasmi katika kongamano hilo, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Angeline Mabula, amesema serikali itaendelea kusimamia, kupitia na kutekeleza sheria mbalimbali ambazo zinalenga kumuinua mwanamke kiuchumi.
Amewata TCB kuangalia namna ya kuwafikia wanawake wanaoishi kijijini kwa kupeleka makongamano kama hayo kwenye maeneo ya pembezoni ili nao wanufaike na fursa wanazozitoa kwa kufanya hivyo hakuna mwanamke atakayebaki nyuma katika kujiinua kiuchumi yeye na taifa kwa ujumla.
“TCB mmesema kongamano kama hili litaendelea mikoa ya Tanga, Arusha, Dar es Salaam na kule Zanzibar, kama jukwaa la kuwakutanisha wanawake kujifunza mambo mbalimbali na kuijua zaidi benki yenu na huduma mnazozitoa hakika yamekuja muda muafaka yatasaidia serikali kuhakikisha hakuna mwanamke anayeachwa nyuma kiuchumi na kimaendeleo maana yatabadilisha hadhi ya wanawake nchini kifedha na kiuchumi nawapongeza sana,”amesema.
Nao baadhi ya wanufaika wa mikopo kutoka TCB wameiomba taasisi hiyo ya fedha kuangalia namna ya kupunguza riba pamoja na kuwafikia wanawake wenzao wanaoishi vijijini ili lengo walilolikusudia la kumuinua mwanamke lifanikiwe kwa asilimi kubwa maana wengi wako maeneo hayo.
Mkurugenzi wa Shirika lisilo la Serikali linalojishughulisha kuwawezesha wanawake na wasichana kumiliki rasilimali zalishi ili waweze kujikwamua kiuchumi la Mikono Yetu, Maimuna Kanyamala, ameiomba benki hiyo kuwafikia wanawake wa kijijini ambao wanajishughulisha na kilimo ili nao waweze kunufaika na mikopo wanayoitoa kwani yeye ingawa anaishi mjini lakini mkopo aliopata ameutumia katika kilimo na anaendelea kunufaika.
“Wito wangu kwa TCB ambao wana nia ya kuwasaidia wanawake wawafikie wenzetu wanaoishi kijijini maana wakienda kukopa wanakutana na changamoto nyingi kutoka taasisi za fedha lakini nao wana ndoto wana nia pia wana morali ya kujikwamua kiuchumi wakiwezeshwa mitaji wanaweza kuleta mabadiliko chanya katika taifa na familia zao,“amesema Kanyamala.
Khadija Liganga ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Dida Vitenge wear amesema” Ukiangalia riba ambayo anaitoa mwanamke mjasiliamali ni sawa na kwamba anachuma kwa ajili ya taasisi za fedha, tunataka taasisi hizi ziwe msaada na sio zenyewe zisaidiwe na wajasiliamali.
“Vilevile tukisema tunaenda na mama 2020 basi tuanze na wanawake wa chini ambao pia wanachangia pato la taifa hili ambao wengi wao wanaishi vijijini,’alibainisha Liganga.
Naye Diwani Viti Maalumu (CCM) kutoka Wilaya ya Ilemela, Winifrida Gyunda, amesema “Changamoto kubwa inayotukabili wanawake ni kuhusu suala zima la kupata mikopo , taasisi nyingi za fedha zimekuwa zikijinasibu kwamba zinatoa mikopo mizuri na kwa haraka lakini tukienda kwenye utekelezaji hii sio halisi.