ELIYA MBONEA-ARUSHA
Sekta ya Wanyamapori inatarajiwa kuimarika zaidi baada ya kuanza kazi kwa mfumo mpya wa Jeshi usu linalosimamia Uhifadhi na Misitu nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Kamishna Mhifadhi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA), Dk James Wakibara leo Jumanne Julai 16, alipopokelewa kwa gwaride rasmi ofisini kwake.
Akizungumza na wafanyakazi Dk. Wakibara amesema TAWA imefungua ukurasa mpya wa kufanya kazi, hivyo amewataka kuhafanya kazi kwa bidii ili kukabiliana na changamoto za uhifadhi.
Aidha, amemshukuru Rais John Magufuli, Uongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii kwa hatua muhimu iliyofikiwa kwani itasaidia kukuza sekta ya wanyamapori nchini.
Dk.Wakibara alivishwa cheo cha Kamishna Mhifadhi wa TAWA na Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamis Kigwangalla kisha kula kiapo cha utii na uadilifu mbele ya Rais Dk. Magufuli Julai 9, mwaka huu katika Hifadhi ya Burigi-Chato mkoani Geita.