Theresia Gasper -Dar es salaam
KOCHA Mkuu wa Simba, Sven VandenBroeck, amesema mabadiliko ya mfumo wa uchezaji wa kikosi chake ndio siri ya ushindi wao dhidi ya Mtibwa Sugar.
Simba juzi iliibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Mtibwa Suhar, katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, uliochezwa Uwanja wa Jamhuri Morogoro.
Kabla ya kukutana na Mtibwa, Simba iliumana na JKT Tanzania na kulala bao 1-0, mchezo wa ligi hiyo uliochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Akizungumza baada ya pambano lake na Mtibwa Sugar, Sven alisema mfumo wa 4-1-3-2 alioutumia kwenye mchezo dhidi ya Mtibwa uliweza kuwabeba na kufanikiwa kupata ushindi huo mkubwa.
“Huko nyuma nilikuwa natumia mfumo wa 4-2-3-1, lakini kwenye mchezo na Mtibwa nilitumia 4-1-3-2 ambao ulitupa ushindi mnono,”alisema Sven na kuongeza.
“Baada ya kupoteza mchezo dhidi ya JKT Tanzania tulijipanga upya na kuingia uwanjani kivingine kabisa.
“Hatukutaka kupoteza mchezo kwa mara nyingine ndio maana tulikuja tukiwa na ari mpya, kuanzia benchi la ufundi hadi wachezaji, pia nilibadilisha mfumo ambao uliwashinda wapinzani na kupata pointi tatu muhimu,” alisema.
Alisema anafurahi kuona wachezaji wake wakiendelea kupambana bila kuchoka na kuonyesha uwezo mzuri.
VandenBroeck alisema ataendelea kuangalia mfumo bora zaidi utakaowawezesha kufanya vizuri zaidi katika michezo yao ya Ligi Kuu Tanzania Bara.
Simba inakamata usukani wa Ligi Kuu Tanzania Bara, ikiwa na pointi 53, baada ya kushuka dimbani mara 21, ikishinda michezo 17, sare mbili na kuchapwa mara mbili.