NA ZAINAB IDDY
HIVI karibuni Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lilimemwondoa mwamuzi, Hussein Athuman, kwenye orodha ya waamuzi wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL), baada ya kupata alama za chini ambazo hazimwezeshi kuendelea tena kuchezesha ligi hiyo.
Mwamuzi huyo amekutwa na rungu hilo mara baada ya kuchezesha mchezo namba 150, uliozikutanisha timu za Yanga na Majimaji katika dimba la Majimaji mkoani Ruvuma, Januari 17 mwaka huu huku Wanajangwani wakitoka kifua mbele kwa ushindi wa bao 1-0 lililofungwa na Deus Kaseke.
Ni jambo zuri lililofanywa na TFF kupitia kamati yake ya waamuzi iliyopo chini ya mwenyekiti wake, Salum Chama, kwani ni wazi msimu huu shirikisho hilo limepanga kuhakikisha ligi inachezeshwa na waamuzi bora.
Lakini kutimuliwa kwa mwamuzi huyo, kumezua swali iwapo kama tatizo lipo kwa waamuzi wa ligi au klabu ya Yanga.
Swali hilo linakuja kutokana na hivi karibuni waamuzi wengi wanaokutwa na rungu hilo, lazima wanakuwa wamechezesha mechi inayowahusu mabingwa hao watetezi, Yanga.
Inakumbukwa Aprili 29, mwaka jana katika mchezo wa FA wa kombe linaloandaliwa na TFF, mwamuzi Abdallah Kambuzi, alifungiwa mwaka mmoja wakati msaidizi namba mbili, Charles Simon, akiondolewa kwenye orodha ya waamuzi, huku Yanga wakitinga hatua ya fainali.
Ukimtoa mwamuzi huyo yupo pia aliyechezesha mechi namba 49 kati ya Yanga na Simba, Martin Saanya na msaidizi wake, Samweli Mpenzu, walioondolewa kwenye orodha ya waamuzi wa Ligi Kuu.
Maamuzi hayo yamefanywa na Kamati ya Usimamizi na Uendeshaji ya Bodi ya ligi, iliyobaini mapungufu mengi ya kiutendaji yaliyofanywa, ikiwemo kutoa kadi nyekundu kwa nahodha wa Simba na kukifanya kikosi cha Wanamsimbazi kucheza pungufu mechi iliyomalizika kwa sare ya bao 1-1 ya Oktoba mosi mwaka jana.