25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Tasaf yatoa Sh bil 37.9 kunusuru kaya masikini

Nathanniel Limu -Singida

MFUKO wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) Mkoa wa Singida, umetoa zaidi ya Sh bilioni 37.9 kunusuru kaya masikini 38,136 kutoka vijiji 278 kati ya mwaka 2014 hadi Januari mwaka huu.

Hayo yalielezwa jana na mratibu wa Tasaf Mkoa wa Singida, Patrick Kasango wakati akitoa taarifa kwa Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk. Mary Mwanjelwa aliyekuwa kwenye ziara ya kikazi mkoani hapa. 

Kasango alisema uwasilishaji huo wa fedha ni kipengele cha kwanza katika mpango wa kunusuru kaya masikini.

Alisema fedha hizo zimetolewa kwa halmashauri sita kati ya saba Mkoa wa Singida.

Kasango alisema ruzuku hiyo imekuwa msaada mkubwa kwa kaya masikini, hususani katika kununua sare za wanafunzi, madaftari, kulipia gharama za matibabu na kujiunga na Mfuko wa Bima ya Afya ya Jamii (CHF).

Alitaja mafanikio mengine ya mpango huo kuwa ni kaya masikini kupata milo mitatu kwa siku, kuanzisha biashara ndogo ndogo za uwekezaji, kuboresha makazi kwa kujenga nyumba za bati na kuanzisha ufugaji wa mbuzi, nguruwe na kuku. 

“Pia kupitia Tasaf tumejenga zahanati nne ambazo zimesaidia kutoa huduma za afya kwa jamii ya vijiji vinne, vikiwemo Ujaire, Wilaya ya Ikungi na Kidarafa, Wilaya ya Mkalama. Vile vile tumejenga nyumba mbili za kuishi walimu,” alisema Kasango. 

Aidha alisema jumla ya Sh milioni 605.5 zimelipwa kwa wasichana balehe 5,727 wa kaya masikini hadi Desemba mwaka 2018.

“Fedha zingine jumla ya Sh milioni 284.8 tumezitoa ikiwa ni ruzuku maalumu kwa wasichana wa kaya masikini wenye umri wa kati ya miaka 10-24,” alisema Kasango.

Alisema pamoja na mafanikio hayo, bado wananchi wengi ni masikini katika vijiji ambavyo havijafikiwa na mradi. 

Alitaja changamoto nyingine kuwa ni kipindi cha kuandikisha walengwa, baadhi ya viongozi wa vijiji na vitongoji waliingiza watu wasio na sifa. 

“Mkoa ulifanya utafiti wa kina na kuwaondoa walengwa 917. Jumla ya Sh milioni 123.7 tumezirudisha makao makuu ya Tasaf Desemba 2016 kupitia akaunti namba 20110003101 Benki ya NMB,” alisema Kasango. 

Kwa upande wake, Dk. Mwanjelwa alitumia fursa hiyo kuupongeza Mkoa wa Singida kwa kusimamia vema shughuli za Tasaf. 

“Nimeridhishwa na utekelezaji wa Tasaf Mkoa wa Singida, hongereni sana. Uamuzi wenu wa kusaidia mabinti katika kaya masikini kujikomboa kiuchumi ni mzuri na ni sahihi kwa sababu utasaidia mabinti wasipate mimba zisizotarajiwa. Uamuzi huu unapaswa kuigwa na mikoa yote nchini,” alisema Dk. Mwanjelwa. 

Mmoja wa wanufaikaji wa Tasaf Kata ya Mtipa, Manispaa ya Singida, Hawa Hamisi alisema kupitia fedha za Tasaf aliweza kujenga nyumba bora ya bati, amenunua mbuzi wanne, ng’ombe mbili na kuku wa kienyeji kwa ufugaji wa kibiashara. 

“Tasaf imeniwezesha kusomesha watoto wangu bila shida. Natarajia kuanzisha shughuli za ujasiriamali, lengo langu ni kwamba huduma hii ya Tasaf itakapokoma, niwe na uwezo kiuchumi. Mimi na familia yangu na tuwe na uhakika wa kupata milo mitatu kwa siku,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles