Sikonge wapitisha bajeti ya Sh bil 22

0
633

Tiganya Vincent -Tabora

BARAZA la Madiwani la Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge limepitisha mapendekezo ya makisio ya mapato na matumizi ya zaidi Sh bilioni 22 kwa mwaka ujao wa fedha.

Hatua hiyo imefikiwa hivi karibuni wakati wa mkutano wa Baraza la Madiwani kujadili na kupitia mapendekezo ya makisio ya mapato na matumizi ya mwaka 2020/21.

Akiwasilisha mapendekezo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Martha Luleka alisema makusanyo na matumizi ya mwaka ujao wa fedha yatatokana na ruzuku ya Serikali Kuu Sh bilioni 19, mapato ya Halmashauri Sh bilioni 2 na asasi zisizo za kiserikali Sh milioni 542.

Luleka alisema pamoja na makisio ya makusanyo na matumizi katika mwaka ujao wa fedha, halmashauri hiyo imepanga kuhakikisha asilimia 40 ya mapato yake ya ndani yanaelekezwa kwenye miradi ya maendeleo na kuanzisha ukanda wa biashara katika eneo la Tulu (Sikonge Business Park).

Alisema vipaumbele vingine katika bajeti ijayo ni kuimarisha usimamizi wa karibu wa miradi ya maendeleo na kuhakikisha asilimia 10 ya makusanyo ya mapato ya ndani yanaenda kwenye vikundi vya wanawake, vijana na walemavu.

Akizungumza wakati wa mkutano huo, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge, Peter Nzalalila aliwapongeza watendaji kwa maandalizi mazuri ya mapendekezo ya makisio ya mapato na matumizi ya mwaka 2020/21.

Aliomba Serikali kuhakikisha inasaidia fedha kwa miradi ya maendeleo ili waweze kukamilisha iliyobaki ili kuwawekea wananchi mazingira mazuri nao kujiletea maendeleo.

Baraza hilo kwa kauli moja lilipitisha mapendekezo ya makisio ya mapato na matumizi ya mwaka 2020/21. 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here