Na Allan Vicent, Urambo
Wananchi wilayani Urambo mkoani Tabora wamepongeza serikali kupitia Mfuko wake wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kwa kufanikisha utekelezaji miradi ya visima virefu vya maji safi na salama katika vijiji vinne kwa gharama ya Sh milioni 256.
Wametoa pongezi hizo jana mbele ya Maofisa wa Mfuko huo kutoka Makao Makuu waliotembelea wilaya hiyo ili kujionea ufanisi wa miradi hiyo ikiwemo kuona miradi iliyoanzishwa na walengwa wa mfuko huo.
Joha Adamu (32) mkazi wa kijiji cha Sipungu kata ya Usisya alisema kuwa maisha ya wakazi zaidi ya 2,000 wa kijiji hicho yalikuwa hatarini kutokana na kunywa maji yasiyo safi na salama, hivyo akaishukuru serikali kwa kuwaletea mradi huo.
Alisema kuwa mradi huo ni mkombozi kwa akinamama na wakazi wote kijiji hapo kwani walikuwa wakiugua mara kwa mara magonjwa ya tumbo, kichocho na kutumia gharama kubwa kunua dawa.
Mjumbe wa serikali ya Kijiji hicho, Idrisa Masudi, alisema kuwa mradi huo uliokamilika Desemba 27, 2019 umekuwa faraja kubwa sana kwao kwani umeweza kutatua kero ya maji iliyokuwa ikiwakabili tangu nchi ipate uhuru.
“Tunaishukuru sana TASAF kwa kutuletea huduma ya maji safi na salama katika vijiji vyetu 4 vya Kalembela, Katunguru, Utenge na Sipungu na hivyo kumaliza tatizo la uhaba wa maji lililokuwepo katika vijiji hivyo,” alisema.Â
Mratibu wa TASAF wilayani humo Danford Yusuph alisema kuwa miradi hiyo iliyofadhiliwa na TASAF imetekelezwa katika vijiji 4 vilivyoko katika kata 3 tofauti ambazo ni Kiloleni (1), Usisya (2) na Nsenda (1).
Alibainisha kuwa visima hivyo vimechimbwa kwa gharama ya Sh milioni 256.2 ikiwemo mchango wa jamii wa Sh milioni 14 na imetekelezwa chini ya usimamizi wa Kamati za Maji kwa kushirikiana na Halmashauri za Vijiji na Ofisi ya Mkurugenzi.
Yusuph alifafanua kuwa miradi hiyo imekamilika kwa asilimia 100 na wakazi zaidi ya 8,900 wa vijiji hivyo 4 wakiwemo wanafunzi wa shule za msingi Kalembele, Katunguru, Sipungu na Mkola wameshaanza kunufaika.
Naye Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Sipungu, Edward Buswelu aliishukuru TASAF kwa kuwaletea huduma hiyo, kwani imeboresha usafi wa wanafunzi na mazingira ya shule na imeongeza mahudhurio na ufaulu wao darasani.