NA GEORGE MSHANA
Mfuko wa jamii unaotoa ruzuku kwa kaya masikini nchini (Tasaf), umekuwa unatoa ruzuku kwa kaya masikini ili waweze kumudu mahitaji yao muhimu ya kila siku kama vile chakula, mavazi, elimu, afya, barabara na maji safi na salama.
Hayo yamesemwa na Ofisa Habari wa Tasaf, Estom Sanga, katika mahojiano maalumu jijini Dar es Salaam wiki hii.
“Ripoti tunazopata kutoka sehemu mbalimbali zinaonyesha kuwa mpango huu umekuwa na mafanikio. Mwaka 2013 tumeanza kwenda nchi nzima kutafuta walengwa ili kuwapa ruzuku ambayo itawasaidia kumudu mahitaji yao ya msingi kama vile chakula, elimu, afya, barabara na maji. Mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya elimu ni kwamba, watoto kutoka kaya masikini mahudhurio yao yameongezeka.
Sharti la kwanza la Tasaf katika kutoa ruzuku ni kwamba mtoto lazima aende shule. Kabla ya kupata ruzuku, watoto walikuwa wanashindwa kwenda shule kwa sababu ya ukosefu wa sare za shule, daftari, viatu, kalamu, lakini baada ya kupata ruzuku ya Tasaf, wanaweza kwenda shule na kupata mahitaji yao muhimu. Mtoto asipohudhuria shule ruzuku inakatwa,” alisema Sanga.
“Ruzuku hii ipo kwenye afya na imewahamasisha watu wengi kupata huduma za afya. Mama mwenye mtoto mdogo amehamasika kwenda kliniki mara kwa mara ili kuangalia afya ya mtoto wake na pia afya yao kama wazazi.
“Hizi ni kaya masikini ambazo zilikuwa haziwezi kupata lishe, walikuwa wanakula mlo mmoja. Idadi kubwa ya walengwa wameweza kuanzisha miradi midogo midogo ya kiuchumi kama vile kufuga kuku wa kienyeji, nguruwe, kupika maandazi, kulima bustani na kujenga nyumba ndogo ndogo za bati,” anaongeza.
Miradi hii ya kiuchumi imeleta mabadiliko kwenye familia zinazopata ruzuku hii. Vilevile, utengenezaji wa miundombinu kama barabara kwenye maeneo yanayofikiwa na mpango huu umesaidia kurahisisha wananchi kufikia masoko, hospitali na vituo vya afya kwa urahisi.
Mpango huu pia umewezesha hawa walengwa kupata pesa na hivyo kujiamini na kutoka kwenda kwenye mikutano, kwa sababu wameweza kuvaa nguo nzuri na kanga nzuri na kupendeza. Wameunda vikundi vya kuweka na kukopa na hivyo kuweza kupata mtaji wa kuanzisha mradi ambao utawasaidia kujipatia kipato na kuondokana na umasikini. Pia wameweza kuibua miradi mingine ya kimaendeleo kama vile upandaji wa miti, vilevile wamejenga matuta kuzuia maji yasiingie kwenye mashamba yao wakati wa mvua.
Tasaf wanahakiki kila wakati kuhakikisha kuwa wale wanaopata ruzuku ya mradi kweli ni walengwa wao. “Uhakiki wa walengwa wetu ni endelevu. Zoezi hili linafanyika wakati wa kutoa pesa na kila mlengwa anatakiwa awe na kitambulisho ambacho tunakitoa sisi (Tasaf). Kama mlengwa amefariki au hajulikani alipo na haendi kuchukua fedha Tasaf, wanamuondoa kwenye mpango. Uhakiki hufanyika nyumba kwa nyumba,” anasema.
Awamu ya kwanza na ya pili, Tasaf ilikuwa inajikita sana kwenye sekta ya elimu, maji, afya, barabara, kilimo, mifugo na shughuli za kiuchumi kama vile kuweka akiba kwa njia ya vikundi na hivyo kuweza kukopa na kuanzisha au kuendeleza miradi ya maendeleo ambayo itawaingizia kipato na kuwafanya waondokane na umasikini.
Tasaf ilianza mwaka 2000. Masharti kwa watu wanaoishi mjini na watu wanaoishi vijijini ni yale yale. Lengo la Tasaf ni kuwapa ruzuku ili kuwajengea uwezo ili nao waweze kushiriki kwenye miradi ya maendeleo na kulipa kodi na hivyo kuchangia pato la taifa. Ni sharti mojawapo kuhakikisha kuwa mtoto anahudhuria shule kwa asilimia 80 na kuhudhuria kliniki kwa ajili ya matibabu.
Kaya ambazo zipo kwenye mpango ni kaya takribani milioni moja na laki moja na watu waliopo kwenye mpango ni milioni sita, hao ndio walengwa wetu. Kaya hizi ni zile ambazo zinapika pamoja na kutunza watoto pamoja.
Tathmini inaonyesha kwamba, kuna mabadiliko makubwa kwenye hizi kaya. Walengwa wanapokua na kufikia hatua ya kuweza kujimudu, hao wanaondolewa kwenye mpango na wengine wanaingizwa kwenye mpango. Hawa ni wale ambao wana miradi ya kuwaingizia kipato. Asilimia 29 ya Watanzania ni masikini na wangepaswa kuingia kwenye mpango. Uwezo wa kifedha wa Serikali kuhudumia/kutoa ruzuku kwa watu wengi zaidi bado ni mdogo.
Changamoto ni kwamba mahitaji ya watu na idadi ya kaya ambazo ni masikini ni kubwa na uwezo wa Serikali wa kuwapa ruzuku ni mdogo.
“Tumefikia vijiji kwa asilimia 70 na asilimia 30 wangepaswa kuingia kwenye mpango. Pia baadhi ya watendaji katika ngazi ya maeneo ya utekelezaji wa mpango huu wamekuwa si waaminifu na hii imeathiri utekelezaji wa mpango na wamekuwa wakichukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria za nchi,” alisema Sanga.