21.5 C
Dar es Salaam
Saturday, July 27, 2024

Contact us: [email protected]

FURSA ZITUMIKE VIZURI KUFIKIA UCHUMI VIWANDA

Na LEONARD MANG’OHA


meruTANZANIA inakabiliwa na tatizo la ukosefu wa ajira hasa kwa vijana wote wasomi na wasio wasomi, kutokana na Serikali kutokuwa na ajira za kuwatosheleza vijana wote.

Hii ni kutokana na mfumo uliojitokeza siku hizi ulimwenguni kote na tatizo hili limechangiwa zaidi na kutokuwapo kwa viwanda vya kutosha ambavyo vingeweza kupunguza kadhia hii aidha kwa kutoa ajira za moja kwa moja au zisizo za moja kwa moja.

Awali Tanzania iliweza kutoa ajira kwa vijana wengi kupitia viwanda vyake vya nguo vilivyokuwa katika mikoa mbalimbali kama kile cha Urafiki cha Dar es Salaam na vinginevyo ambavyo hata hivyo kwa sasa viko hoi kutokana na kuhujumiwa na watendaji wasio waaminifu.

Viwanda pekee ambavyo vimeendelea kutoa ajira kwa wingi na bila kutetereka ni vile vya Saruji vya mkoani Tanga na maeneo mengine ya nchi ambavyo kwa kiasi fulani vimeendelea kufanya vizuri, huku hivi karibuni vikipata ugeni wa mwekezaji tajiri zaidi Afrika toka Nigeria, Aliko Dangote, ambaye amejenga kiwanda kule Mtwara kinachoitwa Dangote Cement.

Kiwanda hicho kinakadiriwa mwanzoni kutoa kiasi cha ajira 3000, kitaajiri Watanzania 6,000 kitakapokamilisha utendaji kazi. Kwa kutambua mchango wa sekta ya viwanda katika ukuaji wa uchumi na kuongeza ajira kwa wananchi, Chama tawala nchini katika ilani yake ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, kiliamua kuja na sera ya kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi ya viwanda na kumfanya mgombea wake wa Uraisi Dk. John Magufuli kugombea kwa ahadi ya kufanya nchi kuwa ya viwanda.

Baada ya kuingia madarakani, Rais wa Awamu ya Tano, Dk. John Magufuli aliendelea kusisitiza kujengwa kwa viwanda ambapo hadi sasa tumeshuhudia makampuni kadhaa yakijitokeza kuwekeza katika maeneo mbalimbali nchini. Kwa mujibu wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), zaidi ya kampuni 136 zimesajiliwa na kituo hicho kuwekeza katika sekta ya viwanda, huku baadhi zikiwa tayari zimeanza ujenzi na nyingine zikitarajiwa kuanza uzalishaji tangu mwishoni mwa mwaka uliopita.

Miongoni mwa makampuni yaliyojitokeza ni pamoja na Goodwill Ceramic Co Limited inayomilikiwa na mwekezaji raia wa China inayojishughulisha na utengenezaji wa vigae ambayo ilielezwa kuanza uzalishaji hadi kufikia Desemba mwaka jana.

Jitihada ambazo zimekuwa zikichukuliwa kuhakikisha viwanda hivi vinavyojengwa ni pamoja na kuviwezesha kupata nishati itakayowezesha kufanya uzalishaji kwa urahisi. Serikali kupitia kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Prof. Justin Ntalikwa, aliliagiza Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kukiunganisha kiwanda hicho na gesi asilia mara tu baada ya ujenzi kukamilika.

“Kiwanda hiki kinatarajia kuzalisha vigae kwa ajili ya shughuli mbalimbali za ujenzi na katika kuzalisha vigae hivyo, kampuni itahitaji gesi kwa ajili ya kuendesha mitambo na kuzalisha umeme wa megawati nane (8) kuendeshea kiwanda,” alisema Prof. Ntalikwa.

Viko viwanda vingine vingi kama kile cha nondo cha Mohamed Kiluwa Steel Group and Company Ltd cha Mlandizi mkoani Pwani, Kiwanda cha Kusindika Matunda, (Sayona Fruits) kilichopo Chalinze kikielezwa kuwekeza Dola za Marekani milioni 55 kinachotarajiwa kuanza uzalishaji Oktoba mwaka huu.

Viwanda vingine ni pamoja na kile cha Saruji cha Kampuni ya Motisum Group kilichopo Talawanda na Magulumatali- Bagamoyo, cha Nondo cha MMI Intergrated Steel Mill kilichopo Zegereni, Kibaha Pwani na kile cha kuunganisha magari ya zimamoto na Matrekta cha ubia kati ya SUMA JKT na Equator Automech Co. Ltd. Kiwanda hiki kinatarajiwa kuanza uzalishaji Januari hii na kutoa kiasi cha ajira 200.

Huenda ujio wa viwanda hivi ukawa mkombozi kwa wakulima wa matunda kutokana na ujenzi wa Kiwanda cha kukausha matunda cha Elven Agria Company Ltd katika eneo la Mapinga Bagamoyo ambacho pia kinatarajiwa kufunguliwa mwezi huu. Pia Septemba mwaka jana Rais Dk. John Magufuli alizindua kiwanda cha kusindika matunda cha Kampuni ya Bakhresa Food Products Ltd.

Kiasi cha vijana 6,000 wanatarajiwa kupata ajira kutokana na ujuzi wa kiwanda cha kutengeneza vigae na kauri cha kampuni ya Twyford ya China kinachojengwa eneo la Pingo wilayani Chalinze. Kati ya ajira hizo 6,000, ajira 2,000 ni za moja kwa moja na 4,000 si za moja kwa moja na kwa mujibu wa Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Jack Feng, kitaanza uzalishaji rasmi Julai mosi mwaka huu.

Wakati Twyford wakitarajiwa kutoa ajira hizo 6,000, kampuni dada ya Keds Tanzania inayotengeneza sabuni za unga na vipodozi inatarajiwa kuzalisha ajira 2,000 kupitia uwekezaji wake walioufanya katika eneo la Tamco Maili Moja Kibaha mkoani Pwani. Viwanda hivi ni vile vinavyopatikana katika Mkoa wa Pwani pekee ambao unatajwa kuwa kitovu cha viwanda nchini kwa awamu ya tano, ukiwa na viwanda zaidi ya 400 vikijumuisha vikubwa na vidogo ambapo waziri ni mlezi wake.

Hivi karibuni, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Tanzania, Charles Mwijage, akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa kiwanda cha Keds Tanzania, anasema Serikali itahakikisha sekta ya viwanda inachangia walau kwa asilimia 40 ya ajira zote na kuchangia katika ukuaji wa maendeleo nchini. Waziri Mwijage aliitaja hatua ya kuanza kwa ujenzi wa kiwanda hicho kuwa ni sehemu ya utekelezaji wa ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya kuhakikisha Tanzania inafikia malengo ya kuwa nchi ya uchumi wa viwanda.

Kiwanda hicho kinatarajiwa kuzalisha tani elfu 50 huku mauzo ya kampuni yakiwa ni Dola za Marekani milioni 33 kwa mwaka, hii inatoa matumaini kufikia lengo kwa sekta ya viwanda kutoa walau asilimia 40 ya ajira zote. “Kinachonifurahisha na kuona kuwa wataanza uzalishaji mapema ni kuwa shughuli ya kutayarisha eneo la ujenzi wa kiwanda hiki imechukua siku 28 tu na wameniambia kuwa ndani na miezi saba wataanza uzalishaji,” anasema Waziri Mwijage.

Anasema Serikali itahakikisha inaendelea na juhudi zake za kuwavutia wawekezaji kuja kuwekeza nchini ili kuhakikisha fursa zinazopatikana mikoa yote nchini zinatumiwa kikamilifu ili kuchangia katika ukuaji wa uchumi wa nchi na kuboresha kiwango cha maisha ya wananchi. Ikiwa amani iliyopo nchini ikitumika kikamilifu na kuhakikisha mazingira bora na kupatikana sera nzuri za uwekezaji, sekta ya viwanda inaweza kuwa yenye tija na kukata kiu ya muda mrefu ya Watanzania ya kuyatafuta maisha bora ambapo sekta hiyo pia itasaidia kuinua sekta nyingine muhimu.

Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Clifford Tandari, anasema kiwanda hicho cha Keds kinachotarajiwa kuwekeza kiasi cha Dola za Marekani milioni 12 kama mtaji, kitakuwa na faida kubwa kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kuwezesha kupungua kwa bei ya bidhaa hizo ikilinganishwa na hivi sasa ambapo huagizwa kutoka nje ya nchi.

“Pamoja na kuzalisha ajira lakini pia kitasaidia kupunguza matumizi ya fedha zetu za kigeni kuagiza bidhaa hizo nje ya nchi na pengine niwatake kuendelea kuwa mabalozi wazuri na kuendelea kuzitangaza fursa za uwekezaji zilizopo nchini,” alisema Tandari. Mkurugenzi wa Keds Tanzania Limited, Jack Feng, anasema kampuni hiyo itaendelea na shuguli za uwekezaji katika maeneo mengine hasa katika uwekezaji wa viwanda.

‘Tutaendelea pia kuwashawishi wenzetu kuja kuwekeza Tanzania kwa kuzingatia kuwa Tanzania ina amani na kuna miundombinu mizuri ya kutuwezesha kwenda mahali popote, hata ukiangalia hapa tunapojenga kiwanda chetu ni karibu na barabara kuu ya Morogoro,” alisema Feng.

Ni imani yangu kuwa juhudi hizi zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali kupitia Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji sambamba na juhudi za TIC katika kuhakikisha wawekezaji wanaendesha shughuli zao katika hali ya ufanisi, ni wazi kuwa tutafikia ndoto za kuwa na uchumi unaotegemea viwanda. [email protected] 0763207431

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles