25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

VIWANDA VYA NYAMA KUJENGWA NCHINI 

Na Mwandishi Wetu


meatKwenye miti hakuna wajenzi, ni msemo uliojengeka na kuota mizizi kwenye jamii zenye kingi lakini hutumia vibaya kile walichonacho au kukosa mbinu ya kutumia utajiri huo.

Suala hilo liko si kwenye mali asili tu hata kwenye fedha na mambo yote yenye thamani, kwani ni aghalabu kukuta vyote pamoja yaani rasilimali na akili pevu.

Mifugo ni sekta muhimu ya kilimo na huunga mkono juhudi za uwekezaji na hivyo kwa maendeleo ya viwanda na inaweza kuwa ni ufumbuzi kuongeza pato la taifa bila kutumia nguvu kubwa.

Tanzania inashika nafasi ya  tatu kwa idadi kubwa ya mifugo  barani Afrika nyuma ya Ethiopia na Sudani ambapo ng’ombe wanafikia milioni 25, mbuzi milioni 16.7, kondoo milioni 8, nguruwe milioni 2.4 na kuku wanafikia milioni 36.

Kwa kifupi, mifugo inalingana na idadi ya watu nchini Tanzania.

Pamoja na kutoa picha inayovutia, sekta hiyo haina mchango wa maana katika uchumi zaidi ya kuleta migogoro na wakulima juu ya malisho na ardhi.

Kuna uhitaji mkubwa wa mazao yanayotokana na mifugo ambao huongezeka kila siku.

Nchini Tanzania, sekta ya mifugo kwa kiasi kikubwa inaendeshwa na wakulima wadogo wadogo na sekta imeajiri mamilioni ya Watanzania.  Shida kubwa katika sekta hii ni uhafidhina wake kwani wengi wa wafugaji hawataki elimu na  maisha yao ni ya kuhamahama wakichunga wanyama wao. Kutokana na kukosa elimu ni wagumu kuelewa mambo na kubadilika na hujikuta mara nyingi wakijificha chini ya kivuli cha mila na utamaduni.

Kimtazamo, wafugaji ni watu masikini lakini kiukweli ni matajiri wasioona mbali na kama wangekubali mabadiliko ya mtazamo na mwenendo wa maisha yao, wangekuwa mbali sana.

Mwakilishi wa Taasisi ya kimataifa inayojihusisha na utafiti wa mifugo ya International Livestock Research Institute (ILRI) Tanzania, Amos Omore, anasema  mifugo ni sekta yenye nguvu  ya kuleta mabadiliko kama tunahitaji wote  kumaliza njaa na kujenga mifumo endelevu ya chakula.

 

Anaelezea kuwa mifugo ni rasilimali isiyoisha kwani ni jadidi na dunia nzima, watu bilioni moja huishi kwa kutegemea mifugo hasa wanawake na ajira kwa vijana. Asilimia15 ya kalori na asilimia 25 ya protini inatokana na wanyama  ambao ni muhimu katika mlo kamili na kuongeza uwezo kipato kwa idadi kubwa ya watu masikini.

Kwa mujibu wa Omore, ongezeko la thamani ya bidhaa za mifugo ni nzuri hasa kwa kilimo biashara kutokana na kwamba  bidhaa sita za kimataifa zinatokana na  kilimo ambacho chanzo chake ni wanyama ikiwemo (maziwa, nyama ya nguruwe, nyama ng’ombe, kuku na samaki) ambayo thamani yake inafikia Dola za Marekani bilioni 715. Hilo si pato haba ukizingatia kuwa teknolojia inayotumika ni duni na haina ubunifu wa kina.

Hata hivyo, ingawa mifugo inachangia asilimia 40 ya Pato la Taifa  katika nchi nyingi ambazo ni masikini zaidi duniani, lakini zinapata asilimia 4 tu ya misaada ya maendeleo  ya kilimo.

Kutokana na maelezo ya mwakilishi huyo, sekta ya mifugo Tanzania  huchangia wastani wa asilimia 13 ya Pato la Taifa ambacho ni kiwango cha chini ikilinganishwa na nchi zenye mifugo wachache kama Botswana ambayo inaongoza mauzo nje kutoka Afrika. Hivyo basi, tija ni ndogo Tanzania kwenye sekta ya mifugo.

“Lakini, hii inaweza ikabadilika kutokana na uwekezaji zaidi na kutumia fursa zinazojitokeza,” anasema.

Anasema kuwa kufika mwaka 2050, uhitaji wa nyama na maziwa katika soko la dunia unatarajia kuongezeka asilimia 145 na 155 katika kipindi hicho, uzalishaji wa nyama Afrika utaongezeka vile vile.

Soko la maziwa litakuwa kubwa katika Afrika hasa Afrika Mashariki, kuliko katika kanda nyingine yoyote isipokuwa Asia ya Kusini.

Ongezeko la uzalishaji wa mifugo haitarajiwi kuendana na ongezeko la matumizi ya nyama, maziwa na mayai katika bara la Afrika.

 

“Afrika itakuwa mwagizaji wa bidhaa za vyakula zinazotokana na wanyama kama uwekezaji hatutafanya; uwekezaji unahitajika ili kuendana na faida zinazotokana na mifugo kwa jamii na ukuaji endelevu wa sekta ya mifugo ambayo inaweza kuzalisha,” anaelezea Omore.

Ongezeko la mahitaji ya bidhaa za mifugo nchini Tanzania na Afrika itafanikiwa kwa kujibu maswali haya matatu kwa mitazamo tofauti:

“Tanzania ipo katika nafasi nzuri ya kuendana kupanda kwa soko la bidhaa za wanyama kutoka Afrika na inakadiriwa kuwa ifikapo mwaka 2050, thamani yake itakuwa Dola za Marekani  bilioni 151.

“Hii inatoa fursa kwa  uwekezaji kutoka sekta binafsi katika  kuwekeza kwenye uzalishaji, au katika utoaji wa huduma zinazoweza kusaidia wafugaji  wadogo kufikia shughuli za ufugaji wa kati,”.

Anafafanua kuwa sekta ya umma na binafsi inatakiwa kuingiliana katika minyororo ya kuongeza thamani katika mifugo.

“Ni lazima kuchukua hatua ya kuongeza nguvu katika maendeleo ya sekta ya mifugo barani Afrika ili kuhakikisha kuwa mchango wa sekta hii si kunufaika kwa chakula tu na lishe, lakini pia maendeleo ya kiuchumi kwa jamii ikiwemo, afya na mazingira ya binadamu,”.

Viwanda vya nyama  

Inasikitisha kuona kuwa pamoja   na kuwa na mifugo mingi, Tanzania haifaidiki vilivyo na rasilimali hiyo kwa mauzo ya kibiashara  na kwa matumizi kama chakula.

Wataalamu wanasema kuwa pamoja na changamoto za mifugo, mahitaji ya nyama nchini na duniani kwa  ujumla yanaonesha kukua na hivyo yanahamasisha ujenzi wa machinjio ya kisasa na viwanda vya kusindika kitoweo hiki kinachopendwa na wengi.

Serikali ya Tanzania imebuni  miradi mbalimbali  ikiwa ni ile miradi  ya kiubia, binafsi na ipo mbioni na halmashauri zinakopa Benki ya Dunia kuweka vitega uchumi.

Ongezeko la uzalishaji wa nyama nchini kwa miaka ya hivi karibuni limefungua fursa mpya za uwekezaji kwenye machinjio ya kisasa na viwanda vya usindikaji ili kulisha soko la ndani na nje. Mpaka sasa hakuna mafanikio makubwa yaliyopatikana, ila kutokana na kushamiri changamoto katika sekta kila hatua inayopigwa. Kifupi miundombinu yake ni ya kizamani, imechakaa na haiaminiki kimuundo na kibiashara.

Takwimu za Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, zinaonesha kwamba kwa miaka sita mfululizo (2006/07-2011/12), kumekuwa na ongezeko kubwa la uzalishaji wa zao la nyama kutoka tani 181,000 hadi karibu tani 300,000.

Kadhalika, uzalishaji kwa mwaka 2013/14 uliongezeka kwa asilimia 6.2 kutoka tani 563,086 hadi kufikia tani 597,757 mwaka 2014/2015, kwa mujibu wa wizara hiyo.

Mahitaji ya nyama nchini ni zaidi ya tani 450,000 kwa mwaka kama ilivyobainishwa na ripoti ya Serikali ya fursa za uwekezaji kwenye viwanda vya nyama ya 2011 (Investment Opportunities in Livestock Industries December 2011). Pamoja na soko la ndani, pia nyama huuzwa Iraq, Vietnam, Hong Kong, Oman na Falme za Kiarabu (UAE). Watu wachache wanajua hilo.

Kituo cha Taifa cha Uwekezaji (TIC), kinakadiria kuwa mwaka 2030, mahitaji ya nyama nchini yataongezeka kwa asilimia 200, sababu mojawapo kubwa  ni ongezeko la watu, si Tanzania pekee bali duniani kote.

World Watch inasema ifikapo mwaka 2050, tani milioni 645 za nyama zitahitajika duniani na kwamba zitazalishwa kutoka nchi zinazoendelea.

Aidha, nyama, maziwa na ngozi zinazalishwa zaidi na nchi zinazoendelea kuliko mataifa yaliyoendelea. Nyama inahitajika zaidi India na China kwenye watu wengi zaidi duniani.

Ongezeko la mahitaji linaonekana nchini kwani wastani wa ulaji nyama ni kilo 15 kwa mwaka kwa mtu, kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS).

Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO) linaloshauri kula angalau kilo 50 za nyama kwa mwaka kwa mtu, awali TIC ilisema Watanzania hula kilo 12 kwa mtu kwa mwaka. Takwimu hizo hazioneshi  mema kwa ugavi na kwenye mahitaji ya nyama kama nchi.

Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William Ole- Nasha, anasema ili kupata tija, Watanzania wanalazimika kubadili ulaji wa nyama, kwani wengi wanafurahia kula kitoweo ‘chenye damu’ kinachotoka machinjioni na kuuzwa buchani, badala ya ile iliyosindikwa.

Hii ni kutokana na mazoea na ukubwa wa bei ya nyama sokoni, kwa kawaida nyama ya ng’ombe huliwa zaidi ikifuatiwa na samaki na kuku. Kuku  na haswa wa kienyeji  ni ghali kuliko  mboga nyingine yoyote.

“Hawajazoea kula nyama ya kusaga, soseji, vipande (fine cuts) steki ya ‘t-bone’ nyama laini ya ‘fillet’.

Endapo wataelimishwa kula nyama hizo, wazalishaji wataongeza thamani ya zao hili ambalo licha ya kuliwa kwa wingi bado halijasindikwa.

“Kinachoudhi wengi ni udhalili wa machinjio yetu,” anasema John Massawe na kuongeza  kuwa mazingira ya machinjio mengi nchini  ni mabaya na  inahitaji uwekezaji mkubwa wa rasilimali, elimu ya usafi  na teknolojia  ya maandalizi na ile ya uhifadhi ili kulinda afya ya walaji.

Tukiweza hayo, ndio tufikirie masuala ya viwanda vya nyama nchini ili kuongeza thamani na kupata faida nyingi (profit maximization) katika  biashara.

Nasha anasema ili kuwe na mafanikio katika viwanda vya nyama, kazi ya kwanza ni kuhamasisha walaji watoke kwenye mazoea ya nyama za buchani na kula zilizoongezewa thamani ili kupata aina nyingi za ulaji badala ya kuzoea mchanganyiko.

Anataja maduka makubwa yenye nyama zilizosindikwa kama soseji, minofu, mbavu, khima, mkia na vipande vilivyokatwakatwa ambayo inauzwa bei kubwa baada ya kuongezewa thamani. Nayo supu, mshikaki na mapande nayo huuzwa ghali wakati ongezeko lake ni kukatwa na kuchoma tu.

Msajili wa Bodi ya Nyama, Susan Kiango, anaeleza kuwa uwekezaji upo kwenye mashirika ya umma, halmashauri za miji na sekta binafsi ambazo zimeanzisha machinjio ya kisasa na viwanda vya kusindika nyama.

“Mwaka 2008 kulikuwa na viwanda vitatu vya kuchinja na kusindika nyama, lakini sasa viko zaidi ya 20,” anasema.

Akitaja Kampuni ya Al-Kaffir ya Oman, iliyowekeza mkoani Dodoma ikishirikiana na Tanzania Meat Company (TMC) kuwa zina vibali vya kuuza nyama nje.

Anasema ujio wa kampuni hiyo umeongeza uwezo wa kuchinja na kusindika nyama na kwamba sasa inachinja ng’ombe 400, mbuzi na kondoo 6,000 kwa siku. Al-Kaffir inakusudia kuuza nyama zaidi kwenye masoko ya nchi za Kiarabu. Huko Arabuni kikwazo ni kufikia nyama iwe ‘halal’ kwa dini ya Kiislamu kwa kufuata misingi ya dini katika uchinjaji  na kushughulikia nyama hiyo  ili iwe na chapa ya ‘halal’  mpaka inapomfikia mteja. Malaysia  uuzaji wake wa nyama umeshamiri baada ya kuweka chapa ya ‘halal’ na kuteka soko la Mashariki ya Kati.

Kiango anaendelea kusema kuwa mwaka 2008, Tanzania ilikuwa na machinjio ya kisasa matatu tu, nayo ni Saafi yaliyoko Sumbawanga, TMC Dodoma na Arusha Meat inayoendeshwa na Halmashauri ya Jiji la Arusha.

“Ushindani umeanza kushamiri na ninaona kuna mwitikio kutoka katika soko, kwani wageni wengi wanakuja kuulizia upatikanaji wa nyama, “anakamilisha Kiango.

Aina ya uwekezaji
Bodi ya Nyama imethibitisha kwamba uwekezaji katika sekta hii haujafikia kiwango cha usindikaji ambao ungeongeza thamani, ajira na mapato zaidi kwa Serikali. Kiwango kikubwa cha nyama inayouzwa nje ya nchi haijasindikwa na pia wanyama hai wakiwamo mbuzi na ng’ombe huuzwa nje.

Ili kudhibiti ubora, bodi inaagiza machinjio ya kisasa kutumia bunduki ya kupiga wanyama ili wapoteze fahamu, kabla ya kuchinjwa au kutumia ‘shoti ya umeme’ kuwaduwaza kama wanavyofanya Zimbabwe.

Uwekezaji lazima uwepo kwa  kuishtua mifugo kabla ya kuichinja kunahusu wanyama wote.Kigezo kingine ni kuwa na vyumba vya ubaridi vya kuhifadhi nyama, yazingatie usafi wa hali ya juu na kufuata taratibu zote za uchinjaji za kimataifa ambazo zimeainishwa kwa mahitaji mbalimbali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles