Na Ramadhan Hassan, Dodoma
TANZANIA imepiga hatua kubwa katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa ukoma ambapo takwimu zinaonyesha idadi ya wagonjwa imeshuka kutoka zaidi 40,000 hadi hufikia 1,200 kwa mwaka 2021, huku Serikali ikiweka mikakati ya kuhakikisha inatokomeza kabisa ugonjwa huo ifikapo mwaka 2030.
Hayo yameelezwa jana Jijini hapa na Mratibu wa Taifa wa Mpango wa Kutokomeza Ukoma nchini,Dk.Deus Kamara wakati akifungua mkutano wa wadau wa mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Amesema wakati nchi ikipata Uhuru ugonjwa wa ukoma ulikuwa ni moja kati ya magonjwa matano yaliyokuwa yakiongoza ambapo sasa hivi ni miongoni mwa magonjwa ambayo hayana tena umuhimu kwa sababu juhudi kubwa zimefanyika
“Miaka ya nyuma visa vya ukoma vilikuwa zaidi ya 40,000 sasa hivi ni 1,200, hali ya ukoma imepungua sana hizi juhudi zote tunazotekeleza kwa sasa tunaita wadau kufanya tathmini ya kina ili kuleta tija baada ya karibu miaka 60 sasa tunakutana tena na wadau,”amesema.
Amesema Serikali imedhibiti kwa kiwango kikubwa ugonjwa huo na hadi sasa ni wilaya 13 tu ndio zinaripoti wagonjwa.
Kwa upande wake Mwakilishi wa Shirika la Afya duniani (WHO) Dk. Alphonciana Nanai, amesema hadi sasa wagonjwa walioripotiwa ulimwenguni ni zaidi ya 16,000 huku Bara la Asia likiongoza kwa kuwa na wagonjwa wengi.
Akimwakilisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya,Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto Prof. Abel Makubi katika mkutano huo Dk. Khalid Massa kutoka Idara ya Kinga katika wizara hiyo amesema mikakati imefanyika kuhakikisha ugonjwa huo unapotea nchini.