24.2 C
Dar es Salaam
Monday, September 23, 2024

Contact us: [email protected]

Tanzania yaanza vyema michuano ya kufuzu Kombe la Dunia la ICC T20

Na Mwandishi Wetu

Timu ya Taifa ya kriketi ya wanaume ya Tanzania imeitandika timu ya Mali kwa wiketi 10 katika siku ya ufunguzi wa mashindano ya kundi A ya Afrika kuwania kufuzu Kombe la Dunia la T20 jijini Dar es Salaam uliochezwa Jumamosi, Septemba 21, 2024.

Timu za Cameroon, Ghana, Lesotho, Malawi, Mali, na Tanzania zinachuana katika mashindano yanayoendeshwa na Baraza la Kimataifa la Mchezo huo (ICC).

Mechi hiyo iliyochezwa katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ilishuhudia Mali ikianza kupiga mpira na kumaliza ikiwa na mikimbio 18 na wapigaji wake wote kutolewa katika ova 12.5.

Wapiga mpira wa timu ya Mali hawakuweza kufua dafu mbele ya warusha mpira wa Tanzania na hivyo hawakufanikiwa kupata mikimbio mingi.

Kikosi hicho kilishindwa kupata mbinu ya kumiliki mchezo wakati wapigaji walioanzishwa, Theodore Macalou- aliyepata mikimbio miwili na mwenzake Mohamed Coulibaly, aliyetolewa bila kupata mikimbio, walipotolewa.

Kikosi hicho kiliendelea kuwa na wakati mgumu baadae kufuatia kutolewa kwa wachezaji wake wengine ndani ya muda mfupi wakati wa zamu ya kupiga mpira.

Nahodha wa timu, Yacouba Konate, na Sanze Kamate  waliopata mikimbio mitatu kila mmoja ndio waliokuwa na mikimbio mingi katika kikosi hicho.

Mrusha mpira wa Tanzania Sanjay Bom alikuwa na wakati mzuri ambapo alipata wiketi nne katika ova tatu na kukiongoza kikosi hicho kuinyima Mali fursa ya kupata mikimbio mingi.

Mchezaji huyo hatimaye alichaguliwa kuwa mchezaji bora na kupewa zawadi baada ya mechi hiyo.

Warusha mpira wengine- Harsheed Chohan na chipukizi Laksh Snehal- pia walionyesha umahiri wakati wa kurusha mpira, wakipata wiketi mbili kila mmoja.

Ally Mpeka na Halidi Amiri waliongeza machungu kwa Mali kwani warushaji hao walipata wiketi moja kila mmoja.

Tanzania haikupata changamoto kubwa wakati wa zamu yake kupiga mpira, ikipata mikimbio19 bila kupoteza wiketi katika mpira mitano na kuondoka na ushindi mkubwa.

Wapiga mpira wa timu hiyo walioanzishwa wakati wa zamu ya kupiga mpira- Zafar Khan na nahodha Abhik Patwa- walionyesha uzoefu wao uliofanikisha kupatikana kwa ushindi katika muda mfupi.

Khan alipata mikimbio 12 na Patwa alipata mikimbio miwili huku wote wakiwa hawajatolewa.

Timu ya Cameroon ilikwaana na Ghana huku Malawi ikicheza na Lesotho katika mechi nyingine za siku hiyo ya ufunguzi.

Mrusha mpira Richmond Baaleri alionyesha umahiri wake, akiiongoza Ghana kuishinda Cameroon kwa wiketi nane katika uwanja wa Klabu ya Gymkhana.

Cameroon ilipata fursa ya kuanza kupiga mpira na kumaliza ikiwa na mikimbio 40 katika ova 14.2.

Nahodha Obed Harvey aliiongoza Ghana kupata ushindi katika mechi hiyo, ambapo kikosi hicho kilifanikiwa kuvuka idadi ya mikimbio ambayo Cameroon ilipata.

Ghana ilipata idadi hiyo ya mikimbio huku ikipoteza wiketi mbili katika ova 8.1.

Mpiga mpira Sami Sohail alikuwa na mchezo mzuri wakati Malawi ikiishinda Lesotho kwa mikimbio 93 katika mechi nyingine iliyochezwa katika uwanja huo huo.

Malawi ilianza kupiga mpira na kumaliza ikiwa na mikimbio 144 huku ikipoteza wiketi nne katika ova 20.

Wapigaji mpira watano wa mwanzo walicheza vizuri na kuisaidia timu hiyo kupata mikimbio mingi.

Sohail, aliyepata mikimbio 61, alikuwa mpiga mpira aliyepata mikimbio mingi zaidi katika kikosi cha Malawi.

Mpiga mpira mwingine Donnex Kasonkho pia alicheza vizuri na kupata mikimbio 30.

Lesotho, iliyokuwa ikitakiwa kufikisha mikimbio 145 ili kuibuka na ushindi, haikufanikiwa kupata idadi hiyo kwani iliishia kupata mikimbio 52 huku wapigaji mpira wote wa timu hiyo wakitolewa.

Warusha mpira Suhail Vayani na Daniel Jakiel waliihakikishia Malawi ushindi walipoonyesha mchezo mzuri wakati wa zamu ya kikosi hicho kurusha mpira.

Wachezaji hao walipata wiketi nne kila mmoja.

Cameroon ilitarajiwa kuchuana na Mali katika moja ya mechi zilizopangwa kufanyika jana.

Ghana ilipangwa kuonyeshana umwamba na Malawi katika mechi nyingine ya siku hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles