27.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

TANZANIA YA VIWANDA MJADALA MZITO

Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage, akisoma hotuba ya bajeti ya wizara yake bungeni Dodoma jana.

 

 

Na MAREGESI PAUL -DODOMA

KAULI ya Serikali ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda, imeonekana kuwatia hofu baadhi ya wabunge kutokana na jinsi inavyosimamia dhana ya ujenzi wa viwanda hivyo.

Hofu hiyo ilionekana jana wakati wabunge hao walipokuwa wakichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji kwa mwaka wa fedha 2017/18, iliyowasilishwa na Waziri Charles Mwijage.

Miongoni mwa wabunge walioonyesha hofu hiyo ni pamoja na Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye (CCM), ambaye alisema Watanzania wengi hawaelewi maana ya viwanda vinavyojengwa na Serikali.

Kutokana na hali hiyo, Nape alimtaka Waziri Mwijage aeleze ni nini maana ya viwanda ambavyo amekuwa akisema vinajengwa na Serikali kwa kuwa Watanzania wengi hawamwelewi.

“Kuna viwanda vilibinafsishwa, lakini havijafanya vizuri. Kwa hiyo, nakuomba waziri uchukue hatua kwa walioshindwa kuviendeleza kwani licha ya kukopa fedha kwa ajili ya kuviendeleza, fedha hizo walizielekeza kwingine.

“Jambo jingine ninalotaka kuzungumzia ni hili la idadi ya viwanda ambavyo mheshimiwa Mwijage umekuwa ukivisema. Umefika wakati ukitaja idadi ya viwanda, watu wanaangaliana usoni kwani hawakuelewi na inaonekana kuna tofauti ya tafsiri ya viwanda.

“Hebu Mwijage utakapokuja hapa kuhitimisha, utuambie nini maana ya viwanda kwa sababu watu hawaelewi nini maana yake,” alisema Nape.

Pamoja na hayo, mbunge huyo wa Mtama, alizungumzia Kiwanda cha Mbolea Lindi akisema kinaelekea kukwamishwa na mataifa makubwa yanayopingana juu ya ujenzi wake.
“Viwanda ni ukombozi na ukombozi ni vita na vita hii inapiganwa na wale wanaonufaika na kutokuwapo kwa viwanda Lindi na Mtwara.

“Kama Serikali itayumba kwenye hili, watu wa Kusini hawatakubaliana na nyinyi. Tunataka vita ya kiwanda hiki cha mbolea ikapiganwe na wakubwa hao nje ya Lindi na Mtwara,” alisema Nape.

Wakati huo huo, Nape alisema kuna haja Serikali isijiingize katika ujenzi wa viwanda na badala yake iweke mazingira mazuri kwa wawekezaji binafsi ili wafanikiwe katika uwekezaji huo.

SERUKAMBA

Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Peter Serukamba (CCM), alilalamikia utoaji wa vivutio nchini kwa wawekezaji, kwa kile alichosema vinatolewa bila utaratibu.

Alisema utaratibu huo unawakatisha tamaa wawekezaji kwa kuwa hawana uhakika na uwepo au kutokuwapo kwa vivutio hivyo.

“Mfumo wa utozaji kodi nchini si rafiki kwa sababu sisi tunataka kutoza kodi hata kabla uzalishaji haujaanza. Yaani, hata utoaji wa vivutio haueleweki kwani unaweza ukaona mwaka huu vimewekwa na mwaka ujao vinaondolewa.

“Kabla ya mwaka 2009 kulikuwa na vivutio na mwaka 2009 vikaondolewa ambapo uwekezaji ulishuka na mwaka 2010 viliporudishwa, uwekezaji ukapanda.

“Katika suala hili, tatizo lililopo ni Wizara ya Fedha kutokuwa na mtazamo sawa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC). Yaani TIC wakiruhusu vivutio viwepo, Wizara ya Fedha inakataa. Nilitamani Waziri wa Fedha awepo hapa atuambie shule yake ya uchumi ni ipi ambayo sisi hatuijui.

“Hebu twambieni kwa sababu hata Rais aliwahi kusema tusipowekeza viwanda katika Serikali yake, hatutaweza kuwekeza katika awamu yoyote. Sasa nyie hayo maneno mazito mnayachukuliaje?” alihoji Serukamba.

CECIL MWAMBE

Akichangia bajeti hiyo, Mbunge wa Ndanda, Cecil Mwambe (Chadema), alisema kodi kwa wawekezaji ni moja ya mambo yanayokwamisha uwekezaji nchini na kuitaka Serikali ifufue viwanda vya korosho Mtwara ili vichangie kukuza uchumi wa taifa.

DEO NGALAWA

Mbunge wa Ludewa, Deo Ngalawa (CCM), alisema ili Serikali iweze kufanikiwa, ni lazima iangalie kwa umakini miradi ya makaa ya mawe ya Mchuchuma na Liganga.

“Mradi huu unazungumzwa tangu mwaka 1929 mpaka leo, lakini hatuji hatima yake. Kwa hiyo tunaomba Serikali iiangalie miradi hii kwa jicho la tatu,” alisema Ngalawa na kuungwa mkono na Mbunge wa Viti Maalumu, Mary Mwanjelwa (CCM) alipokuwa akichangia bajeti hiyo.

KAMBI YA UPINZANI

Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni katika wizara hiyo, Anthony Komu, alizungumzia kiwanda cha viuadudu kilichoko Kibaha, Mkoa wa Pwani na kusema kinajiendesha kwa hasara kwa kuwa Serikali inaonekana kukisahau.

“Hicho kiwanda kimetajwa na Serikali kama cha kimkakati ambacho kimekabidhiwa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) baada ya ujenzi wake kukamilika kwa mkopo wa Dola za Marekani milioni 22.307 na wenye riba ya asilimia 11 utakaorejeshwa kwa miaka 10.

“Hadi Februari 2017, kiwanda hicho kilikuwa kimezalisha dawa lita 100,000 ambazo ziliuzwa nchini Niger kwa Sh bilioni 1.012.

“Tanzania ambayo inatumia fedha nyingi kupambana na malaria inayoua watu wengi zaidi nchini, haijanunua hata lita moja ya dawa kiwandani hapo.

“Hata Wizara ya Afya ambayo bajeti yake tumeshaipitisha hapa, hakuna fedha zozote zilizotengwa kwa ajili ya dawa kutoka kiwandani hapo, jambo ambalo linakifanya kisiwe endelevu.

“Kiwanda hicho ambacho kina uwezo wa kuzalisha lita milioni sita kwa mwaka, hakizalishi chochote kwa sababu hakina soko la kuuza dawa zake, ingawa kinaendelea kulipa gharama mbalimbali, ikiwamo mishahara na umeme.

“Kwa hiyo, kambi ya upinzani bungeni inataka maelezo juu ya kiwanda hiki,” alisema Komu.

Kuhusu ufufuaji wa kiwanda cha matairi cha General Tyre kilichoko Arusha, Komu alisema hakiwezi kufufuliwa kwa kuwa zinahitajika fedha nyingi.
Kwa mujibu wa Komu, Serikali imetenga katika bajeti ya mwaka wa fedha 2017/18, Sh milioni 70 badala ya Sh bilioni 22.

Pamoja na hayo, Komu alisema kambi yake hairidhiswi na uamuzi wa Serikali wa kuendelea kununua transfoma kutoka nje ya nchi wakati kuna transfoma zinazozalishwa na kiwanda cha Tanalec cha Arusha.

WAZIRI MWIJAGE

Awali akiwasilisha hotuba yake ya bajeti bungeni, Waziri Mwijage, alisema makaa ya mawe nchini yanauzwa kwa bei ndogo na yanatumiwa na zaidi ya viwanda 15 nchini.

“Kutokana na bei ndogo na ubora wa makaa ya mawe yanayozalishwa nchini, zaidi ya viwanda 15 vimeanza kuyatumia makaa hayo kama chanzo cha nishati na kuachana na matumizi ya mafuta mazito pamoja na kuni.

“Matumizi ya makaa ya mawe kwa viwanda hivyo, yanakadiriwa kuwa tani 1,048,056 kwa mwaka, sawa na tani 75,338 kwa mwezi.

“Aidha, makaa hayo yanauzwa nje katika nchi za Kenya, Uganda na Rwanda,” alisema Mwijage.

Kuhusu uanzishwaji wa viwanda, alisema tangu Serikali ya awamu ya tano iingie madarakani, viwanda vikubwa 393 vimeshaanzishwa kufikia Machi mwaka huu.
Kwa mujibu wa Waziri Mwijage, mtaji wa viwanda hivyo ni Dola za Marekani milioni 2,362.59 na kwamba watu 38,862 wanatarajia kuajiriwa.

KAMATI YA VIWANDA

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira, Stanslaus Nyongo, alisema wawekezaji nchini wanalalamikia utaratibu unaotumika kutoa misamaha kwa wawekezaji.

“Wawekezaji wamelalamikia suala la utoaji wa vivutio vya wawekezaji kuwa hauko sawa miongoni mwa wawekezaji.

“Wawekezaji kutoka nje, wamekuwa wakipatiwa vivutio vingi zaidi, hivyo kuwakatisha tamaa wawekezaji wa ndani wanapotaka kuwekeza.

“Mfano ni mwekezaji Dangote ambaye amepewa gesi na makaa ya mawe kwa bei nafuu zaidi wakati wawekezaji wa aina yake hawajapewa.

“Kwa hiyo, kamati inashauri Serikali kuwa motisha ambazo zinaweza kutolewa kwa wawekezaji wote wa ndani na nje, ni vizuri wote wakapatiwa,” alisema Nyongo ambaye pia ni Mbunge wa Maswa Mashariki (CCM).

Kuhusu makaa ya mawe, kamati hiyo iliitaka Serikali iruhusu uagizaji wa makaa ya mawe kutoka nje ya nchi.

“Serikali imezuia kuagiza makaa ya mawe kutoka nje ya nchi wakati yaliyopo hayatoshelezi mahitaji na uamuzi huo umeongeza bei ya makaa hayo yanayozalishwa hapa nchini," alisema.
 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles