27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

TANZANIA KUTUMIA VIWANDA KILIMO KUFIKIA UCHUMI VIWANDA

Katibu Mtendaji wa Ansaf, Audax Rukonge
Katibu Mtendaji wa Ansaf, Audax Rukonge

Na Joseph Lino,

TANZANIA inapanga kuwa nchi yenye uchumi wa viwanda ifikapo 2025, juhudi za serikali kwa sasa ni  kuhamasisha uanzishaji wa viwanda kuanzia vidogo hadi vikubwa.

Ili kufanikisha mchakato huu, kunahitajika mipango mahususi ya kujenga viwanda vidogo, hasa sekta ya kilimo, ambako malighafi hutokea kwa wingi na rahisi.

Sekta ya kilimo inahitaji maboresho na kuongeza nguvu kwa sababu watu  na wananchi wengi wameajiriwa huko.

Jukwaa Huru la Wadau Kilimo (ANSAF) na wadau wa sekta mbalimbali walijadili namna Tanzania inavyoweza ikafanikiwa katika mageuzi ya kuifanya nchi ya uchumi wa kati unaotokana na viwanda.

Katibu Mtendaji wa Ansaf, Audax Rukonge, anasema kuwa  ili Tanzania iweze kufikia lengo linaloendana na dira ya ifikapo 2025 kuwa nchi inayotegemea uchumi wa viwanda, inabidi sekta ya kilimo iongezewe nguvu kwa kuwajali wakulima ambao ndio wazalishaji wakubwa wa malighafi na hivyo kuinua viwanda.

“Kuna haja kuinua viwanda vya sekta ya kilimo, hasa vidogo na vya kati kwa sababu vina tabia ya kuajiri watu wengi, na kuwa kwa karibu sehemu wanaozalisha pia vinahitaji gharama ya fedha ndogo ya uendeshaji,” anasema Rukonge.

“Serikali  iangalie wafanyabiashara wadogo na wa kati namna wanaweza kujengewa uwezo wa kuwa na viwanda, kuwahamasisha kuwa na viwanda kuliko kuuza mazao nje ya nchi,” anasema.

Rukonge anaelezea kama Ansaf, wanaangalia namna gani baadhi ya sera zinavyohitaji kufanyiwa marekebisho na kuziwekea sheria ili kulinda maslahi ya nchi na kufanikisha masilahi ya wakulima na viwanda.

Kwa maelezo ya Ansaf, tafiti zinaonesha kuwa nchi za jangwa la Sahara, sekta ya kilimo ya inaweza kuondoa umasikini na njaa mara 11 kuliko kitu kingine chochote.

“Ili kufanikisha hili kunahitajika kuwe na mikakati, na lazima ilenge namna inavyoboresha hali ya mzalishaji wa kwanza,”alisema.

Naye Profesa Samuel Wange, Mtafiti wa Uchumi wa kujitegemea anasema kuwa kufuatia dhima ya Serikali kuwa ifikapo 2025 kuwa nchi ya viwanda,  kilimo ni nguzo ya uchumi wa Tanzania katika viwanda.

“Kwa mantiki hii, kusaidia sekta ya kilimo ambapo wakulima wadogo na kilimo biashara kutaweza kuinua sekta ya viwanda,” anasema Profesa Wangwe.

Anaelezea kuwa, shughuli nyingi za uchumi zinatokea kwenye kilimo na sekta isiyo rasmi ambako uzalishaji ni mdogo.

“Malighafi zote zinatokana na kilimo kama chakula, mapato, fedha za kigeni na vitu vingine.”

Anasema utafiti unaonesha kuwa nchi za kusini mwa Afrika chakula kilichotengenezwa viwandani (processed) kinanunuliwa sana.

Wangwe anafafanua kuwa, mapinduzi katika mnyororo wa ugavi wa chakula barani Afrika, unaongozwa na viwanda vidogo na vya kati ambavyo vinafanya kazi katika usindikaji wa chakula, uuzaji jumla na rejareja.

“Uwekezaji wa ndani na nje katika kilimo unaweza kuongeza uzalishaji, ajira na kipato na kutoa fursa kwa ongezeko la ushiriki katika minyororo  ya kimataifa,” anaeleza Wangwe.

Kwa upande wake Ofisa wa Sera na Mipango kutoka Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi , Revelian Ngaiza, anasema sekta ya kilimo itaendelea kubaki kuwa msingi wa uchumi kwa Tanzania.

Ngaiza anasema kuwa mwaka jana sekta ya kilimo ilichangia asilimia 29 katika pato la taifa (GDP), hutoa asilimia 95 ya mahitaji ya chakula na kutengeneza ajira  kwa asilimia 66 ya idadi ya watu na malighafi ya viwanda.

“Kilimo kina uwezo wa kuinua watu wengi na kutoa umaskini na kuchangia kufikia lengo la maendeleo katika kipato cha uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025,” anasema Ngaiza.

Hata hivyo, sekta ya kilimo inaendelea kukumbwa na changamoto mbalimbali, huku takwimu zikionesha kuwa miaka ya karibuni kilimo kinaendelea kushuka.

Ofisa wa Biashara kutoka Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Wilfred  Kahwa,  anasema sekta ya kilimo imekuwa ikishuka tangu mwanzoni mwa miaka ya 2000.

Anasema mwaka wa 2000 kilimo kilichangia ajira kwa asilimia 80, lakini  na mwaka huu kimechangia asilimia 67.

Kahwa anaelezea kuwa katika pato la taifa (GDP) mwaka wa 2000 kilichangia asilimia 30, 2010 asilimia 24, 2015 asilimia 29 na ifikipo 2025 kitachangia asilimia 18 kwa mijibu wa Shirika la Chakula Duniani (FAO).

“Kujenga ukuaji wa uchumi, kilimo cha Tanzania kinahitaji kuboreshwa kutoka mwanzo hadi mwisho, ukijumuisha mnyororo wa thamani na kujenga mahusiano ya masoko,” anasema Kahwa.

Akifafanua zaidi, Profesa wa Chuo cha Sokoine, Ntengua Mdoe, anaelezea kuwa  faida za viwanda vidogo vya kilimo kuwa vina uwezo wa kutengeneza fursa za ajira kwa wingi kwa sababu ni rahisi kusimamiwa na zinahitaji mtaji mdogo wa uendeshaji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles