23 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

MAGUFULI ATAMBUA UMUHIMU UWEKEZAJI MKUBWA NCHINI

Rais Dk. John magufuli akiwa na na mmiliki wa Kiwanda cha Saruji cha Dangote kilichopo Mtwara Alhaji Aliko Dangote .
Rais Dk. John magufuli akiwa na mmiliki wa Kiwanda cha Saruji cha Dangote kilichopo Mtwara Alhaji Aliko Dangote .

Na LEONARD MANG’OHA,

ZAIDI ya wiki mbili magazeti ya hapa nyumbani yalitawaliwa na vichwa vya habari vinavyohusu sakata la kusitishwa kwa uzalishaji katika kiwanda cha saruji cha bilionea namba moja Afrika Aliko Dangote kilichopo mkoani Mtwara.

Usitishwaji wa uzalishaji unatokana na kile kilichoelezwa ni gharama kubwa za uendeshaji wa kiwanda hicho hali inayosababisha kujiendesha kwa hasara kutokana na kutumia gharama kubwa kupata nishati kuwezesha uzalishaji.

Pia ziko taarifa zinazopingana nazo zinazoeleza kuwa kusitishwa kwa uzalishaji katika kiwanda cha bilionea huyo anayekadiriwa kuwa na ukwasi unaofikia dola za Marekani bilioni 15.4. kuwa ni hitilafu za kiufundi.

Kusitishwa uzalishaji katika kiwanda hicho kuliibua hisia tofauti miongoni mwa Watanzania wengi hali iliyowalazimu Mawaziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji Charles Mwijage pamoja na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kutolea ufafanuzi suala hilo.

Wote kwa nyakati tofauti waliushutumu uongozi wa kiwanda hicho kwa kile walichodai kuwa ni kutaka kununua gesi kwa gharama ndogo sawa na gharama inayotumika kununua gesi ghafi kutoka kisimani jambo wanalosema haliwezekani.

Kadhalika walipinga kitendo cha kiwanda hicho kuagiza makaa ya mawe kutoka nje ya nchi kinyume cha makubaliano ya kutumia makaa ya mawe yanayochimbwa hapa nchini.

Jarida maarufu linalofuatilia nyendo za kibiashara za watu wenye ukwasi mkubwa duniani, akiwamo Dangote, wiki iliyopita liliripoti juu ya tukio hilo, huku likiibua baadhi ya hoja.

Gazeti hili lilinukuu jarida hilo ambalo pia limekuwa likitoa orodha ya matajiri wakubwa duniani lililoeleza kuwa uamuzi wa menejimenti ya Dangote kusitisha uzalishaji, umetokana na kuongezeka kwa gharama kubwa za uendeshaji.

Sababu nyingine iliyotajwa ni ‘kutozingatiwa kwa makubaliano ya mkataba, na Serikali kusitisha uamuzi wa kuiondolea kampuni ya Dangote ushuru wa forodha katika mafuta ya dizeli ambayo imekuwa ikiyaingiza nchini kuendeshea mitambo yake.

Kwa mujibu wa Forbes, kampuni hiyo iliiomba TPDC iweze kuiuzia gesi asilia kwa bei nafuu, lakini maombi hayo yalikataliwa.

TPDC katika taarifa yake iliyotolewa wakati ya msigano huo ukiendelea, inasema kiwanda hicho kilikuwa kikitaka kuuziwa gesi kwa bei ya hasara; inayolipwa kununulia gesi ghafi kutoka kisimani.

Kwa mujibu wa Forbes, moja ya hoja za msingi inayotolewa na TPDC inasema haiwezi kuuza gesi asilia kwa bei ya kisimani, kwa sababu kuna gharama zinazoongezeka katika kuisafisha na kusafirisha.

Taarifa zilizochapishwa na jarida hilo zinaonesha kuwa kiwanda hicho kinatumia kiasi cha dola milioni nne, sawa na Sh bilioni 8.7 kwa mwezi kununua mafuta ya dizeli ili kupata nishati ya umeme wa kuendeshea mitambo ya kuzalishia saruji kiwandani hapo.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kiwanda cha Dangote, Harpeet Duggal, Oktoba mwaka huu akisema; “Kiwanda chetu kinatumia lita milioni sita za dizeli kwa mwezi ili kuwezesha uzalishaji wa umeme kwa jenereta, baada ya ahadi za kupatiwa gesi asilia inayozalishwa karibu na kiwanda chetu kutotekelezwa.”

Jarida la Forbes lilibainisha kuchukuliwa kwa hatua zinazotofautiana juu ya mkataba wa kiwanda cha Dangote na Serikali ya awamu ya nne ya Rais Mstaafu Dk. Jakaya Kikwete na ya tano ya Dk Magufuli

Forbes linaeleza kwamba; “chini ya uongozi wa Kikwete, maofisa wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), walimpatia Dangote ahadi ya nafuu ya kodi na nyingine zisizotajwa.” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Pamoja na kodi pia imekuwa ikielezwa kuwa viko baadhi ya vivutio ambavyo havikubainishwa kuwa aliahidiwa kama mwekezaji mkubwa. Kigezo cha ukubwa ni uwekezaji unaozidi dola za Marekani milioni 50.

Forbes inakandia kuwapo kwa mzozo katika ubora wa makaa ya mawe na gharama za makaa ya mawe kati ya yale yanayozalishwa hapa nchini na yale yanayoagizwa kutoka Afrika Kusini anakonunua Dangote.

Kwa pamoja mambo haya yamekuwa yakitawala mijadala mingi katika mitandao ya kijamii na mijadala hii inatokana na ukweli kwamba kiwanda hicho kinawezesha Watanzania wengi kupata ajira aidha za moja kwa moja au zinazoweza kutokana na fursa zitakazotokana na uwapo wa kiwanda hicho.

Aidha kwa kukubaliana au kutokubaliana kuwa tangu kiwanda hicho kilipoanza uzalishaji kimesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza gharama za ujenzi na bei yake nchi nzima.

Kabla ya kuja kwa kiwanda hicho sokoni bei ya saruji nchini ilikuwa haikamatiki  maeneo mengi ya nchi ikifikia hadi Sh 20,000/= kwa mfuko wa kilogramu 50 kwa mikoa ya kanda ya ziwa na baadhi ikiuzwa kwa Sh 17,000/= hadi 18,000/= kwa uzito kama huo.

Wakati hayo yakiendelea mwishoni mwa wiki iliyopita Rais Dk. Magufuli kwa maombi ya mwenye kiwanda alikutana na mmiliki wa kiwanda hicho, Aliko Dangote, Ikulu Dar es Salaam kutafuta ukweli wa mambo ambalo Rais analitaja kuwa zoezi kuingiliwa na wapiga dili.

Taarifa ya Ikulu iliyotolewa na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu inaeleza kuwa katika mazungumzo baina ya wawili hao, Rais Magufuli anasema hapakuwa na tatizo lolote kuhusu kiwanda hicho isipokuwa mradi huo uliingiliwa na ‘wapiga dili’.

Kwa mujibu wa Rais Magufuli, kulikuwa na watu ambao walitaka kujinufaisha binafsi kupitia mradi huo kwa kufanya biashara za ujanja ujanja kitu ambacho serikali yake hairuhusu.

Dk. Magufuli anasema Dangote ametaka eneo dogo ambalo angelitumia kusafirishia saruji yake  lakini wakajitokeza watu ambao wamenunua eneo hilo na kutaka kumuuzia kwa shilingi bilioni 43 kwa lengo la kujinufaisha kwa kutengeneza faida isiyohalali.

Rais Magufuli ambaye amekuwa akifanya jitihada za kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi ya viwanda alimuhakikishia Dangote kuwa serikali yake itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji wote katika kutimiza azima yake hiyo, na kusisitiza kuwa ujanja waliotaka kufanya watu hao hauwezekani katika serikali yake.

“’Iwapo unataka maelezo yoyote ama lolote linalokukwamisha uwasiliane na viongozi wa serikali badala ya kuwasiliana na watu ambao wako kwa ajili ya kufanya biashara ya ujanja ujanja kwa lengo la kupiga dili, ” Rais Magufuli alimhadharisha Dangote.

Vilevile Rais Magufuli amemtaka Dangote kununua gesi moja kwa moja kutoka TPDC ambacho ni chombo cha serikali badala ya kutumia watu ambao wamekuwa na nia ya kutengeneza faida tu.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo Dangote alidai kushangazwa na taarifa zinazoeleza kuwa amesitisha uzalishaji baada ya kukatazwa kuagiza makaa ya mawe toka nje ya Tanzania kitu ambacho anasema hakiingii akilini kwa sababu makaa ya mawe ya Tanzania ni rahisi na yana ubora kuliko ya kuagiza nje.

Katika kile kinachoonekana na kuishi kwa maneno yake mfanyabiashara huyo ameingiza juzi malori mapya yapatayo 600 kwa ajili ya kusambazia saruji inayozalishwa na maana kuwa uzalishaji nao utaongezeka na kwenda kubebea makaa kwenye mgodi wake wa Ruvuma.

Katika mazungumzo yao Dangote mwenyewe alisema lengo lake la kufanya biashara hapa nchini mbali na kutengeneza faida pia kuisaidia serikali ya Tanzania kutengeneza ajira hivyo hana sababu ya kuagiza malighafi kutoka nje ya nchi ambazo zinapatikana nchini.

Dangote alimuhuhakikishia Rais magufuli kuwa ataendelea kufanya kazi na Serikali ya Tanzania na kamwe hana mipango yoyote ya kufunga kiwanda chake

Dangote awali alikuwa na mipango ya kiwanda cha sukari Mkoa wa Morogoro na Kiwanda cha Saruji mkoa wa Dar es Salaam. Anasema ana mpango wa kuangalia fursa nyingine za uwekezaji nchini kutokana na uwepo wa sera nzuri za uwekezaji chini ya Serikali ya Awamu ya Tano.

Kukutana huko kwa Rais Magufuli na Dangote ni muhimu kufuta taswira potofu kuwa Awamu hii ya serikali sio rafiki kwa wawekezaji. Ni mtihani amabao Rais Magufuli amefanikiwa kupita vizuri na      hivyo kuokoa ajira 10,000.

Vilevile imethibitisha kuwa Rais anatambua umuhimu wa uwekezaji mkubwa unaofanyika nchini na jinsi unavyopunguza tatizo la ukosefu wa ajira na mchango wake chanya katika ukuaji wa uchumi wa Taifa.

Sakata hilo vilevile liliwaumbua watu wa Kenya ambapo vyombo vya habari vya huko vikidai nchi yao iko tayari kununua au kuhamishia mitambo hiyo nchini Kenya.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles