26.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, May 21, 2024

Contact us: [email protected]

TFDA NA TBS WAKATAA KUWEPO MGOGORO

tbs

NA GORDON KALULUNGA,

TAASISI za Serikali ambazo ni Mamlaka ya Dawa na Chakula (TFDA) na Shirika la Viwango Tanzania (TBS), zimejikuta katika mwingiliano wa kimajukumu kiutendaji.

Kwa mujibu wa Sheria ya  Chakula, Dawa na Vipodozi ya mwaka 2003, TFDA imepewa majukumu ya Kufanya uchunguzi wa kimaabara ili kuhakikisha kuwa bidhaa husika zinafikia viwango vya ubora na usalama.

Kutoa leseni na vibali mbalimbali vya kuendeshea biashara ya vyakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba. Kuelimisha jamii kuhusu ubora, usalama na matumizi sahihi ya vyakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba.

Kifungu cha sheria ya Viwango Na. 2 ya mwaka 2009, TBS inafanya majukumu ambayo ni pamoja na kupima na kuhakiki katika maabara bidhaa zinazozalishwa viwandani. Kutoa leseni za matumizi ya alama ya ubora kwa bidhaa za ndani na nje zilizokidhi viwango.

Kwa mujibu wa wajasiriamali wa viwanda, wamezitaka taasisi hizi kutafuta muda mwafaka wa kukutana na kuzungumza jinsi ya kuondoa tatizo la mwingiliano wa majukumu ya taasisi hizo. Lakini TFDA inakataa kuweko hali hiyo.

Mjasiriamali na mbunifu wa kusindika vinywaji aina ya mvinyo na vyakula katika Wilaya ya Mbeya, Sarah Kalinga, mwenye kampuni iitwayo Mama Neema Food Product, yenye namba ya usajili BRELA 193265, anasema kufikia maendeleo ya viwanda kama ilivyo ndoto ya Rais John Magufuli ni kazi.

Mjasiramali huyo ambaye pia ni Katibu Mkuu wa wasindikaji bidhaa katika Halmashauri hiyo, anabainisha kuweko changamoto mbili kwa wawekezaji wadogo ambazo ni  kukosekana  soko la uhakika na upimaji wa bidhaa moja na kuilipia katika mamlaka mbili za serikali ambazo ni TFDA na TBS.

Alisema jambo la kushangaza ni kuweko kwa bidhaa ambazo hazifai katika soko zinazotengenezwa na baadhi ya wawekezaji wakubwa, zikiwemo nazi za maji na soda zinazowekwa fleva  ya machungwa wakati sio halisi, lakini watendaji wa mamlaka hizo
hawazigusi. Vilevile analalamikia uwepo utitiri wa kodi.

“Tuna mzigo wa kodi na kutakiwa kulipia leseni Halmashauri, Wizara ya Afya, Osha, Brela, TRA, Umeme, Maji, TBS na TFDA” alisema Sarah.

Wasindikaji na wakufunzi wa masuala ya usindikaji kupitia SIDO Mbeya, Rehema Msina na Anitha Mwasajone, wanasema changamoto ni nyingi, ikiwamo kulipia upimwaji wa bidhaa zao kwa dola za Kimarekani ambazo hufikia kiasi cha Sh 600,000.

“Nafuu TBS wanapima bidhaa zetu kwa Tsh 50,000, tofauti na hawa TFDA ambao sisi tayari tumepata vibali vyao, lakini baada ya kupitia changamoto mbalimbali ikiwamo ucheleweshaji wa upimwaji bidhaa,” walisema wajasiriamali hao kutoka eneo la Nane Nane Uyole, huku wakidai mitaji kuwa kikwazo kikubwa kwa wajasiriamali.

Mwekezaji  Ivan Kibona, ambaye ni Mkurugenzi wa  Ivan Products inayozalisha bidhaa za viwandani, zikiwamo sabuni na mafuta ya kupakaa mwilini naye anasema mwingiliano wa majukumu ya taasisi hizo ni moja ya kikwazo.

Mkurugenzi huyo alionesha barua ambayo inamkataza kuuza bidhaa zake, licha ya kuthibitishwa ubora na TBS.

Barua ya Machi, 29 mwaka huu kutoka TFDA iliyosainiwa na Meneja wa Mamlaka hiyo kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Rodney Alananga, inasema kuwa pamoja na kutambua kuwa bidhaa za kiwanda hicho zimethibitishwa na TBS, bado wao hawatampatia kibali cha kuendelea na uzalishaji na usambazaji.

“Bidhaa zako zimethibitishwa ubora na TBS na kuwa zina ubora wa juu na pia unaomba Mamlaka itambue uwepo wa TBS katika bidhaa zako. Kumbuka kuwa kwa mujibu wa mwongozo wa usajili wa bidhaa za vipodozi wa mwaka 2015, kifungu namba 2.2, mchakato wa usajili hufanywa ndani ya siku 90, ikiwamo kujibu hoja zitakazotolewa, kama maombi hayajakidhi matakwa ya Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi mwombaji anatakiwa kuomba upya na maombi yaambatane na malipo mapya pamoja na fomu husika,” imeeleza barua hiyo yenye kumbukumbu namba EC.67/82/364/01/08.

Mwandishi alifanya mahojiano na mamlaka hizo mbili na yalienda kama ifuatavyo;

Meneja wa Shirika la viwango Tanzania (TBS) kanda ya Nyanda za juu Kusini, Abel Mwakasonda, anasema hakuna mwingiliano wa majukumu kati yao na TFDA maana kila mamlaka inatekeleza majukumu yake.

“Sioni kama kuna mwingiliano wa majukumu kwa sababu kila taasisi inatekeleza majukumu yake na hatuna ugomvi,” anasema Mwakasonda.

Naye Meneja wa TFDA kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Rodney Alananga, alipoulizwa alisema kuwa kuna maswali kwa ngazi yake hapaswi kuyajibia mpaka makao makuu jijini Dar es Salaam.

“…kuna utaratibu wa kujibu maswali yanayogusa sheria na nchi nzima, kwa utawala wa Kanda yangu si busara kujibu maswali kama hayo
yanayoweza kuathiri utendaji wa sheria nyingine, na kushauri uwasiliane na Mkurugenzi wa Usalama na Chakula,” alisema Alananga.

Mwandishi alifanya mawasiliano ya barua pepe na Mkurugenzi huyo, Raymond Wigenge, ambaye alijibu maswali ya mwandishi baada ya mwezi mmoja na yafuatayo ni maswali ya mwandishi wa makala haya na majibu ya Mkurugenzi huyo kutoka TFDA.

SWALI:

Katika utekelezaji wenu wa majukumu kuna sheria au majukumu yanayoonekana kugongana, hasa suala la upimaji wa bidhaa za wajasiriamali wenye viwanda vidogo nadhani na vikubwa ambapo watu hao wanapaswa kulipia gharama za upimaji TFDA na TBS pia.

JIBU:

TFDA na TBS ni taasisi za Serikali zilizoanzishwa kwa mujibu wa sheria. TFDA ipo chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Ilianzishwa chini ya Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi, Sura 219.

Lengo la kuanzishwa Sheria hii na Taasisi hii ni kulinda afya ya jamii dhidi ya madhara yanayotokana na matumizi ya chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba na ndiyo maana ipo chini ya Wizara yenye dhamana ya Afya.

Watumiaji wa vyakula wanapaswa kulindwa bila kujali vyakula husika vinazalishwa na viwanda vikubwa au vidogo. Ikiwa kunatokea magonjwa
yanayotokana na vyakula, Wizara yenye dhamana ya afya kupitia TFDA inawajibika na wala si taasisi nyingine yoyote.

Kabla ya bidhaa inayodhibitiwa na TFDA haijaruhusiwa kuingia katika soko, moja ya hatua inayochukuliwa ni kupima katika maabara ili kupima usalama wake. Kwa hiyo TFDA inatekeleza majukumu yote yanayolenga kulinda afya ya mlaji dhidi ya madhara yanayotokana na chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba.

TBS vivyo hivyo imeanzishwa chini ya Sheria ya Viwango na inatekeleza majukumu ili kufikia malengo yaliyokusudiwa na kuchangia katika malengo ya Wizara  ya Uendelezaji Viwanda, Biashara na Uwekezaji.

Upimaji wa bidhaa unafanywa pia ili kujiridhisha juu ya ubora wake, ikiwa ni sharti mojawapo kabla ya kuruhusiwa kutumia alama ya ubora inayotolewa na TBS.

Kutokana na maelezo hayo, kuna wakati taasisi hizi zinaweza kufanya majukumu yanayofanana lakini kwa malengo tofauti.

SWALI:

Sheria zinazogonganisha majukumu kati ya TFDA na TBS, je, kuna haja ya kupatanishwa? Katika nchi nyingine kuna mgongano wa namna hiyo? Na kama upo au ukitokea nini kinafanyika? Ni nchi gani kama zipo?. Na je, ninyi kama TFDA kuna hatua au maoni yoyote mmeyapendekeza ngazi za juu zaidi?

JIBU:

Katika utekelezaji wa majukumu ya taasisi hizi mbili kumekuwapo malalamiko miongoni mwa wadau kuwa kuna mwingiliano kiutendaji. Katika nchi nyingi zilizoendelea shughuli za taasisi za viwango zimetenganishwa na shughuli za udhibiti wa usalama wa vyakula kama ilivyo kwa Tanzania.

Nchi nyingine katika Afrika zenye mfumo kama wa Tanzania ni pamoja na Ghana na Nigeria. Ingawa ni vigumu kutenganisha majukumu ya taasisi hizi mbili kiurahisi, jambo ambalo linaweza kukuonesha ikiwa shughuli inayofanyika ina lenga kulinda afya ya walaji hilo litakuwa jukumu la TFDA.

Ikiwa linalenga kuendeleza viwanda, biashara na masoko, hilo ni jukumu la TBS. Kuna baadhi ya majukumu yanaweza kufanywa na taasisi zote kwa malengo tofauti. Mfano ukaguzi wa kiwanda unaweza kufanywa na taasisi hizi mbili kwa lengo na kusajili na kutoa kibali cha usindikaji (TFDA) na kutoa alama ya ubora (TBS) kama nilivyoeleza hapo juu.

Changamoto ya mwingiliano kiutendaji kati ya taasisi za Viwango na zile za Udhibiti zinajionesha zaidi miongoni mwa nchi zinazoendelea kuliko katika nchi zilizoendelea.

Kutokana na malalamiko ya wadau, taasisi hizi mbili zipo katika mazungumzo ya kuchukua hatua zenye lengo la kuondoa mwingiliano uliopo.

SWALI:

Kuna madhara yoyote yanayotokana na mwingiliano wa majukumu hayo?

JIBU:
Hakuna madhara yoyote yanayotokana na mwingiliano huo kwa upande wa taasisi hizi mbili, isipokuwa mzigo kwa wadau wanaohitaji huduma kutoka pande hizi mbili.

SWALI:
Ni vikwazo gani vinawakabili wabunifu kupata vibali vya biashara kutoka TFDA? Je, kikwazo ni utengenezaji hafifu wa bidhaa kutokana na teknolojia isiyo ya kisasa?

JIBU:

TFDA inatekeleza majukumu yake kwa kuzingatia Sheria, Kanuni na miongozo mbalimbali ili kuhakikisha kuwa chakula ni salama.
Wajasiriamali wanapata changamoto katika kukidhi matakwa ya kisheria kuhusu majengo, usafi, kuzingatia misingi bora ya uzalishaji, usalama wa bidhaa na kushindwa kugharamia uchunguzi wa maabara wa sampuli za vyakula husika ikiwa ni miongoni mwa sharti kabla ya kusajiliwa na kuruhusiwa sokoni.

Kwa mujibu wa Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji nchini 2016/2017, Waziri wa Wizara hiyo, Charles Mwijage, ametaja kuwa hapa nchini kuna viwanda vidogo 6,907.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles