25.7 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

BIDHAA GESI KICHOCHEO SHUGHULI NYINGINE

Mitambo ya kuchakata gesi
Mitambo ya kuchakata gesi

Na LEONARD MANG’OHA,

TANGU kugundulika kwa gesi nchini, Watanzania wengi wamekuwa na matumaini makubwa ya kupata mafanikio ya kiuchumi kutokana na kuuzwa na kutumika kwa gesi katika shughuli mbalimbali za uzalishaji, kwani hutumika kama nishati na mambo mengine lukuki.

Matumaini hayo yanatokana na faida zinazoelezwa kupatikana kutokana na gesi asilia na kiasi ambacho kimegunduliwa huko Mtwara kinachofikia futi za ujazo trilioni 55.8 na kile cha hivi karibuni kilichogunduliwa eneo la Ruvu mkoani Pwani na Kampuni ya Dodsal, inayofikia futi za ujazo trilioni 2.99.

Kwa mujibu wa tafiti mbalimbali, zinaeleza kuwa kwa kiasi cha gesi iliyogunduliwa Mtwara, inaweza kuhudumia nchi ya Uingereza kwa kutoa nishati kwa miaka 30.

Kwa kiwango hicho, ni wazi kuwa tunayo gesi kiasi cha kutosha kwa matumizi ya ndani kwa muda mrefu na kuihakikishia nchi upatikanaji wa nishati ya uhakika pale uzalishaji utakapoanza kufanyika kwa kiwango cha juu, hasa baada ya kuanza kuzalisha umeme katika mradi wa Kinyerezi II.

Kaimu Mkurugenzi Mtendji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Kapuulya Musomba, anasema kwa sasa karibu asilimia 50 ya umeme unaotumika nchini unatokana na gesi asilia inayosafirishwa kutoka Mtwara.

Kutumika kwa gesi kuzalisha umeme kumepunguza kwa kiasi kikubwa uagizaji wa mafuta mazito ya kuendeshea mitambo ya kuzalisha umeme, hivyo kuipunguzia gharama Serikali na kuongeza ufanisi katika upatikanaji wa umeme kutokana na umeme wa gesi kuwa wa uhakika ukilinganisha na umeme kutoka katika maji.

Matumizi ya gesi katika kuendeshea magari pia yatapunguza gharama za mafuta kutokana na matumizi ya gesi kuwa nafuu na bei yake ni rahisi zaidi ya asilimia 45 ikilinganishwa na bei ya mafuta ya petroli.

Kwa mujibu wa TPDC, ulinganifu wa gesi asilia na petroli kinishati ni kuwa kilogramu moja ya gesi asilia iliyoshindiliwa ni sawa na lita 1.54 ya petroli.

“Hivyo basi, ikiwa nishati iliyomo katika lita moja ya petroli inauzwa Sh2,200 za Tanzania, inaweza kuendesha gari kwa kilomita 1, basi utatumia gesi asilia iliyoshindiliwa kiasi cha 0.65 kilo tu kutembea umbali ule ule wa kilomita 12,” ilieleza taarifa hiyo.

Taarifa ya TPDC ilifafanua kuwa kwa bei ya sasa kiasi cha 0.65 ya kilogramu moja ya gesi asilia iliyoshindiliwa kitagharimu fedha za Tanzania Sh 1007.50 tu. Pia gharama za ukarabati wa magari zinapungua endapo utatumia gesi asilia badala ya petroli.

Kuimarika kwa upatikanaji wa umeme kunatakiwa kulenge kupeleka nishati hiyo katika maeneo ambayo shughuli za uzalishaji zinafanyika kwa kiasi kikubwa, ili kuongeza ufanisi na kurahisisha utendaji kazi tofauti na ilivyo sasa.

Licha ya kuwa kiasi cha gesi iliyogunduliwa ni kikubwa, lakini wanachopaswa kuelewa ni kwamba, Tanzania itaendelea kuwapo karne na karne, hivyo ni vema Serikali kutumia uwapo wa gesi kuwezesha sekta nyingine, hasa viwanda na kuleta mapinduzi ya viwanda ambavyo vitawezesha upatikanaji wa ajira kwa vijana wengi wasio na ajira.

Moja ya sekta zinazopaswa kupewa kipaumbele zaidi ni kilimo, kutokana na kuwa ndiyo sekta inayoajiri Watanzania wengi, huku ikitajwa kuwa uti wa mgongo wa uchumi wa Taifa.

Katika sekta hii muhimu Serikali inapaswa kuhakikisha vinapatikana viwanda vidogo vitakavyokuwa vikichakata na kusindika mazao yanayozalishwa.

Liliani Mpinga ni mtaalamu wa kilimo kutoka Wizara ya Kilimo, anasema ni vema ikiwa Serikali itawezesha umeme kufika maeneo ambayo shughuli za kilimo zinafanyika na kuhakikisha upatikanaji wa nishati hiyo kuliko hali ilivyo sasa ambapo  watu wengi wanashindwa kuanzisha viwanda kwa kukosa nishati ya uhakika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles