32.1 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Tanzania inawajali wawekezaji

Elizabeth Hombo -Dar es salaam

RAIS Dk. John Magufuli amemtaka mfanyabiashara maarufu nchini, Mohamed Dewji ‘Mo’, kuendelea kufanya uwekezaji na kuitangaza Tanzania namna ambavyo inawajali na kuwathamini wawekezaji. 

Vilevile amemtaka bilionea huyo namba moja Afrika, kujali masilahi ya wafanyakazi kama ambavyo anafanya katika klabu ya Simba.

Aliyasema hayo jana wakati wa hafla ya uzinduzi wa kiwanda cha kusaga nafaka kilicho chini ya Kampuni ya Mohammed Enterprises Tanzania Limited (MeTL) inayomilikiwa na mfanyabiashara huyo.

“Mohammed Dewji chapa kazi nenda mbele, wala usiwe mnyonge, Tanzania ipo pamoja na wawekezaji. Kazi unayoifanya ni nzuri, uwekezaji uliofanya ni mkubwa, endelea Serikali iko pamoja na wewe.

“Pia ninakupongeza sana katika hili na ninakuomba uwajali wananchi wanaofanya kazi hapa, hasa masilahi yao, kwa hiyo unapokuwa unaangalia masilahi ya Simba uangalie pia masilahi ya wafanyakazi wa 21st Century Food and Packaging,” alisema Rais Magufuli.

Aliitaka Kampuni ya MeTL Group kuacha utaratibu wa kuagiza ngano kutoka nje ya nchi na badala yake waanze kulima nchini kwani kwa kufanya hivyo itasaidia Watanzania wanaohitaji ajira.

“Ninatoa wito kwa MeTL Group chini ya Mohamed Dewji, nilipokuwa ninapewa maelekezo nimeambiwa mahindi yanatoka Tanzania ambayo yanatengenezwa tani 300 kwa siku, lakini ngano inayotengeneza tani 1,400 kwa siku inaagizwa kutoka nje, hii tuibadilishe.

“Katika maisha yangu nilikuwa nafahamu kulikuwa na mashamba makubwa sana ya ngano kule Basutu, Manyara, lakini sasa hivi hayatumiki na kuna wakati wawekezaji wakijaribu wanachomewa moto, sasa nitoe wito hata kwa kampuni yako muanze kulima ngano, kwani mtakuwa mmewasaidia Watanzania wengi,” alisema Rais Magufuli.

Alitoa wito kuwa zitumike teknolojia za kawaida za uzalishaji wa bidhaa katika uwekezaji wa viwanda, ambazo ni rahisi kwa watu kujifunza hasa katika kipindi cha mwanzo.

Katika hilo, alisema ni vizuri Mamlaka ya Vyuo vya Ufundi Stadi (Veta) kuwa na ushirikiano wa karibu na Shirika la Kuendeleza Viwanda Vidogo (Sido), ili uzalishaji wa vifaa vinavyotumia teknolojia kwa viwanda vidogo vya kilimo vihusishwe.

Aidha, alimwagiza Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa kuwachukulia hatua watendaji wa wizara yake wanaoweka vikwazo kwa wawekezaji.

“Nimepata taarifa kuna baadhi ya wawekezaji wanaotaka kuja kuwekeza nchini wanawekewa vikwazo, wanazungushwa na wengine wanaombwa rushwa… unamzungusha mwekezaji wa nini wakati hela ni ya kwake.

“Waziri wa Biashara (Bashungwa) kalishughulikie hili, kama kuna watendaji wako ndani ya wizara bado hawajaelewa mtazamo wa Serikali, wakae pembeni sisi tuendelee.

“Tunataka wawekezaji waje, ana hela yake mwoneshe mahali ardhi ipo. ‘Mindset’ zetu zibadilike kwa sababu inafika mtu anapotaka kuwekeza atazungushwa weee mara kibali cha NEMC (Baraza la Uhifadhi wa Mazingira) mara OSHA (Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi) mara nini.

“SI uende wewe basi ukaoge mwenyewe kama unataka kunaniii, waziri wewe ni kijana, nenda kafanye kazi kwa manufaa ya nchi hii,” alisema Rais Magufuli.

Kwa upande wake, Mohamed Dewji, alimpongeza Rais Magufuli kwa jitihada anazozifanya katika uongozi wake, huku akisema mageuzi makubwa yaliyofanywa katika kipindi cha awamu ya tano ndiyo yaliyosababisha kuendelea kuwekeza nchini.

 “Mheshimiwa Rais, tunaamini kwamba wale wasiokuelewa leo watakuelewa baadaye na wasioelewa lengo wataeleweshwa na matokeo ambayo tunaamini hayako mbali sana, kwani mageuzi makubwa chini ya uongozi wako ndiyo yaliyotushawishi kuendelea kuwekeza nchini kama unavyoshuhudia leo hii.

“Binafsi ninashuhudia kuimarika nidhamu kwa watumishi wa umma, mkazo mkubwa serikalini, kutekelezwa kwa miradi mbalimbali ya maendeleo, kupungua kwa rushwa na kushughulikiwa kwa migogoro ya ardhi nchini, pia tumeguswa na namna ulivyoshughulikia matatizo ya wafanyabishara,” alisema.

Mo akizungumzia kiwanda hicho, alisema ni miongoni mwa viwanda vikubwa na vya kisasa kinachojishughulisha na uzalishaji wa unga wa ngano na mahindi.

 “Hivi sasa kiwanda kimeboreshwa kwa kuwekeza kwenye mitambo mikubwa iliyogharimu jumla ya Sh bilioni 105 na inatumia teknolojia ya kisasa zaidi, uwekezaji huu umefanyika chini ya awamu ya tano.

“Leo tunashuhudia kiwanda cha mahindi chenye uwezo wa kusaga tani 300 kwa siku, kiwanda cha ngano chenye uwezo wa kusaga tani 1,240 kwa siku, mitambo yenye uwezo wa kupokea tani 600 kwa saa za nafaka na uwezo wa kuhifadhi nafaka hadi tani elfu 50,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles