26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 22, 2024

Contact us: [email protected]

Kamati SADC kuinua wanasayansi wadogo

Christina Gauluhanga Na Tunu Nassor -Dar es Salaam

SERIKALI imesema itatumia kamati mbalimbali za Umoja wa Maendeleo Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kuwasaidia wabunifu katika sayansi na teknolojia ili wafanye utafiti wenye kutatua changamoto za jamii.

Akizungumza katika maonyesho ya tisa ya Wanasayansi Chipukizi Tanzania (YST), Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, alisema kupitia kamati ya mawaziri wa sayansi, teknolojia na ubunifu, wamejiwekea mipango ya kuendeleza wabunifu.

Alisema suala la kuwatambua na kuwaendeleza wabunifu limepewa kipaumbele.

“Kwa sasa tumeweka mipango na taratibu kuwatambua wanasayansi na wabunifu ambapo jumuia hii inaingia katika mapinduzi ya viwanda, hivyo wabunifu ni watu muhimu,” alisema.

Profesa Ndalichako alisema maonyesho hayo yanaashiria kuwa elimu inayotolewa inakidhi na kuwa na uwezo wa kutatua changamoto za jamii.

Alisema amefurahi kuona miradi iliyoonyeshwa imeongezeka kutoka 81 na kufikia 95 ambayo ni mafanikio kwa sekta hiyo.

“Najivunia kuona kuwa idadi ya wasichana imezidi kuongezeka ambapo kwa mwaka huu wasichana ni 88 sawa na asilimia 46,” alisema Profesa Ndalichako.

Alisema zamani masomo ya sayansi hayakupendwa na wasichana, lakini katika kipindi hiki kumekuwa na mwamko mkubwa kutokana na jitihada za walimu kuhamasisha.

“Hata tafiti zilizofanyika kwa mwaka huu zimekuwa na kiwango bora na zenye kulenga kutatua changamoto zilizopo katika jamii,” alisema Profesa Ndalichako.

Aliwaomba walimu kuwafundisha wanafunzi kufanya utafiti ambao utasaidia ukuaji wa uchumi hasa katika mapinduzi ya viwanda.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Sayansi na Teknolojia (Costech), Dk.  Amos Nundu, alisema kwa muda mfupi vijana kupitia YST wamefanya utafiti unaoonyesha kutatua changamoto za jamii.

“Mfumo huu ni mzuri kwa kuwa umeweza kujenga vijana wadogo wenye uwezo wa kufanya tafiti zenye weledi zinazosaidia kuchangia ukuaji wa taifa,” alisema Dk. Nundu.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya YST, Profesa Yunus Mgaya, aliwapongeza washiriki waliofanya utafiti.

Katika maonesho hayo, washindi walikabidhiwa vikombe na medali. 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles