24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Viuatilifu feki vyamkera Makamu wa Rais

Derick Milton Na Grace Shitundu -Simiyu

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, ameagiza Wizara ya Kilimo kushughulikia kasoro zilizopo katika upatikanaji wa pembejeo, hasa mbolea, mbegu na viuatilifu ili wakulima waweze kuzalisha kwa tija na kuleta mapinduzi katika sekta ya kilimo.

Alisema kumekuwepo na malalamiko mengi kutoka kwa wakulima juu ya kupelekewa pembejeo ambazo hazina ubora na wakati mwingine kuwafikia zikiwa zimechelewa na kuwafanya wazalishe kidogo.

Samia alisema hayo jana wakati akifungua rasmi maonyesho ya 27 ya Sikukuu ya Wakulima (Nane Nane) kitaifa Viwanja vya Nyakabindi mkoani Simiyu.

Kaulimbiu ya mwaka huu ni ‘Kilimo, Ufugaji, na Uvuvi kwa Ukuaji wa Uchumi wa Nchi’.

Samia ameitaka Wizara ya Kilimo kushirikiana na taasisi zilizoko chini yake zinazohusika na jambo hilo, kuhakikisha wanawasimamia wazabuni wa pembejeo kutokana na kuwa tatizo sugu kwa wakulima nchi nzima.

“Suala la ucheleweshwaji na ubora wa pembejeo, ni suala ambalo limekuwa sugu sana, wizara lazima msimamie wazabuni mnaowapa fedha nyingi kusambaza mbolea, mbegu kwa wakulima, mara nyingi zinachelewa kuwafikia waulima na wakati mwingine zinakuwa chini ya kiwango.

“Malalamiko ya wakulima yamekuwa mengi, hawapati kwa wakati, lakini wakitumia wadudu hawafi, niagize wizara shughulikieni hili tatizo ili wakulima waweze kuzalisha vizuri na kwa tija,” alisema Samia.

Licha ya hali hiyo aliwataka watafiti nchini katika sekta ya kilimo kuhakikisha wanafikisha matokeo ya tafiti zao katika ngazi za chini kwa maofisa ugani na wadau wengine ili wakulima waweze kunufaika.

Alisema watafiti wengi wamekuwa wakifanya kazi nzuri na kupata mbegu bora zinazokinzana na magonjwa pamoja na mbegu zinazohimili mabadiliko ya tabia nchi na alisema tafiti hizo zimekuwa haziwafikii wakulima kama inavyotakiwa ili waweze kubadilika.

“Kumekuwepo na malalamiko juu ya operesheni hii, hasa kwenye ziwa letu hili la Victoria, sheria hazifuatwi, lakini pia hata Serikali inapoteza mapato yake, niagize wizara husika kulifanyia kazi jambo hili ili sheria ziweze kufuatwa kadiri inavyotakiwa,” alisema.

Samia aliwataka wataalamu wa mifugo kutumia maonyesho ya Nanenane mwaka huu kuhakikisha wanatoa elimu kwa wafugaji jinsi ya kufanya ufugaji endelevu wa kuvuna mifugo yao na kujiongezea kipato, ikiwa pamoja na kuondokana na migogoro ya wakulima na wafugaji.

Katika hatua nyingine, Samia amewaagiza wamiliki wa viwanda ambao wameanza kutengeneza mifuko mbadala baada ya kupigwa marufuku mifuko ya plastiki, kurekebisha mara moja kasoro ambazo zimeanza kulalamikiwa na watumiaji.

Kwa upande wake, Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga alisema kuwa sekta ya kilimo imekuwa ikikabiliwa na changamoto nyingi ikiwemo ya upotevu mwingi wa mazao ya wakulima kwa asilimia 25 hadi 40.

Alisema kuwa kutokana na hali hiyo wizara imeandaa mpango wa kudhibiti upotevu wa mazao kuanzia mkulima anapovuna hadi kuhifadhi, ambapo kwa mwaka huu wa bajeti umetengewa Sh bilioni 38.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles