27.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, June 12, 2024

Contact us: [email protected]

TANZANIA INAPOFUNIKA KOMBE KUELEKEA JUMUIYA YA MADOLA

NA WINFRIDA MTOI

MICHEZO ya Jumuiya ya Madola inatarajia kufanyika Gold Coast, nchini  Australia, Aprili mwakani.

Hiyo itakuwa mara ya 21 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1930 ilipofanyika kwa mara ya kwanza nchini Canada.

Tanzania ina historia kubwa katika michezo hiyo na ndiyo mashindano pekee ya kimataifa ambayo imejipatia medali nyingi kuliko mengine.

Tanzania imejikusanyia jumla ya medali 21 katika mashindano ya  Jumuiya ya Madola, sita zikiwa za dhahabu, sita fedha na shaba tisa ambazo zilipatikana kupitia mchezo wa ngumi na riadha.

Miongoni mwa wanamichezo walioiletea heshima Tanzania katika michuano hiyo ni Filbert Bayi, mwanariadha ambaye hadi sasa rekodi yake haijavunjwa tangu alipofanikiwa kunyakua medali ya dhahabu mwaka 1974.

Bayi alivunja rekodi ya dunia ya mbio za mita 1,500 akitumia dakika 3:32.2 na sasa ni miaka 44 imepita lakini hakuna  mwanariadha mwingine aliyeweza kuifikia.

Wanamichezo wengine waliowahi kunyakua medali ni Juma Ikangaa,  Gidamis Shahanga, Zakayo Malekwa, Zakarie Barie, Simon Mrashani, Fabian Joseph, John Yuda, Francis Naali, Samson Ramadhani, Geway Suja na  Willy Isangura.

Bondia pekee wa Tanzania aliyewahi kutwaa medali ya dhahabu katika mashindano ya Madola alikuwa ni Michael Yombayomba, hiyo ilikuwa  mwaka 1998  yalipofanyika Kuala Lumpar, Malaysia.

Hiyo ilikuwa medali ya mwisho kwa Tanzania kuchukua kwenye michuano kama hiyo, hakuna Mtanzania mwingine  aliyefanikiwa kurejea na medali licha ya kuendelea kushiriki michuano hiyo.

Kuelekea mashindano yajayo, hakuna dalili nzuri za Tanzania itarejesha heshima yake kutokana na maandalizi duni ya timu zitakazoshiriki kinyang’anyiro hicho.

Maandalizi yalivyo

Ikiwa imebaki miezi nane kabla ya michuano ya Jumuiya ya Madola haijaanza, maandalizi kwa timu za Tanzania bado yanasuasua baadhi ya michezo ilivyoteuliwa kwenda kuiwakilisha nchi  kushindwa kuonyesha nia ya ushiriki wao.

Vyama vya  michezo vilivyopewa fursa hiyo na Kamati ya Olimpiki Tanzania (TOC) ambao ndio wasimamizi ni mpira wa meza ‘table tennis’, Chama cha Michezo ya Watu Wenye Ulemavu (TPC), Shirikisho la Ngumi za Ridhaa (BFT), Chama cha Kuogeleza Tanzania (TSA) na Shirikisho la Riadha Tanzania (RT).

Vipo vigezo vinavyozingatiwa ili kupata fursa ya kushiriki Michuano ya Jumuiya ya Madola.

Kimojawapo ni ushiriki wa mashindano ya kimataifa, lakini  hadi sasa ni riadha na kuogelea pekee ndio waliofanikiwa kukidhi.

Riadha na kuogelea wamefanikiwa kufikia vigezo hivyo baada ya kuonyesha jitihada katika ushiriki wa mashindano ya kimataifa tangu mwaka jana, wakianzia  kwenye timu ya taifa hadi mchezaji mmoja mmoja.

Ukiachilia mbali michezo hiyo, vyama vya michezo mingine bado vinasuasua hali inayoashiria  huenda mwakani Tanzania  ikawakilishwa na michezo miwili pekee katika michuano ya Jumuiya ya Madola.

Hali hiyo inatokana na ukweli kwamba, hakuna dalili nzuri kwa michezo mingine ukiondoa masumbwi ambayo mabondia wake wameanza kujifua hivi karibuni.

 BFT wafunguka

Katibu Mkuu wa BFT, Makore Mashaga, anakiri kwamba wamekuwa wakishindwa kushiriki michuano ya  kimataifa akisema hali hiyo inasababishwa na ukosefu wa fedha licha ya kwamba wana nia ya kushiriki michezo ya Jumuiya ya Madola.

Anasema katika kuonyesha kwamba wana dhamira hiyo, tayari timu ya taifa ya mchezo huo imeingia kambini na Novemba na Desemba mwaka huu wameandaa mashindano mawili makubwa ambayo wanaamini yatawawezesha kufikia vigezo vitakavyowawezesha ya kushiriki michuano ya Jumuiya ya Madola.

“Tunashindwa kushiriki mashindano ya kimataifa kutokana na ukata na ndiyo sababu hata mwaka huu hatujashiriki mashindano ya dunia.

Lakini nina imani tutakwenda kushiriki michuano ya Jumuiya ya Madola kwa sababu baadhi ya mabondia tayari wana vigezo na mwisho wa mwaka huu, tutaandaa michuano mikubwa miwili yakufuzu,” anasema.

Anataja vigezo muhimu vinavyotakiwa ili bondia aweze kushiriki michuano ya Jumuiya ya Madola ni pamoja na kushiriki michuano ya kimataifa ndani ya miaka mitatu bila kujali matokeo, uthibitisho wa afya yake kuwa timanu katika kipindi cha miezi mitatu kabla ya mashindano na kuwepo kwenye kumbukumbu ‘database’ ya Shirikisho la Masumbwi la Dunia.

Anasema hayo yote yapo ndani ya uwezo wao kwa kuwa wana mabondia walioshiriki mechi ya kimataifa kuanzia mwaka jana.

“Timu nzima inafanya mazoezi kwa sasa na mabondia wote majina yao tumewaingiza kwenye database kwa hiyo sina wasiwasi katika hilo,” anasema.

Kauli ya TOC

Licha ya masumbwi kuanika vigezo vyao kuwawezesha  kushiriki mashindano ya Jumuiya ya Madola, Katibu Mkuu wa TOC, Filbert Bayi, anasisitiza  hadi sasa ni michezo miwili pekee iliyofuzu ambayo ni riadha na kuogelea.

“Wiki iliyopita tulikutana na vyama vya michezo ili kujua mustakabali wao katika michezo hiyo, ambapo tulibaini bado viongozi wake wana jukumu kubwa la kuhakikisha wanashiriki mashindano ya kimataifa tofauti na hapo hawatashiriki Jumuiya ya Madola.

“Vyama ndivyo vyenye jukumu la kuandaa wachezaji, sisi tunasimamia tu lakini hali ilivyo si nzuri kwa sababu wengi bado hawajafuzu kutokana na vyama kushindwa kushiriki michuano vya kimataifa ya kuwafanya wafikie vigezo.

“Kutokana na hali hiyo, tulikutana na vyama vyote hivi karibuni na kujadili suala hilo ambapo tutaangalia hadi kufikia Oktoba mwaka huu mwelekeo utakuwaje katika maandalizi,” anasema Bayi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles