28.7 C
Dar es Salaam
Friday, May 24, 2024

Contact us: [email protected]

BAVICHA WAJIANDAA KUFANYA MAANDAMANO

Na PATRICIA KIMELEMETA

BARAZA la Vijana la Chadema (Bavicha) limesema linaendelea kuratibu kimya kimya maandamano yanayotarajiwa kufanyika hivi karibuni, baada ya vikao vyao vinavyoendelea kumalizika.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Bavicha Taifa, Patrobas Katambi, alisema uamuzi huo umefikiwa baada ya Jeshi la Polisi kushindwa kujibu barua yao ya Agosti 24, mwaka huu, ambayo pamoja na mambo mengine, ililitaka Jeshi hilo kusikiliza malalamiko ya wananchi kuhusu kukamatwa kwa baadhi ya wabunge wa upinzani.

Alisema katika barua hiyo pia walilitaka Jeshi hilo kutoa maelezo ya sababu zinazochangia kukibeba Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuwaruhusu kuendelea kufanya mikutano ya kisiasa, huku vyama vya upinzani vikipigwa marufuku.

Alisema kutokana na hali hiyo, baraza hilo liliwasilisha barua hiyo kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro na Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI) ili kujua hatima ya barua yao, lakini hadi sasa hakuna majibu yoyote yaliyotolewa na viongozi hao, badala yake wamewatuma askari kuzungumza katika ofisi za chama hicho huku wakiwa na magari yenye bendera nyekundu.

Kutokana na hali hiyo, alisema ukimya wa kutojibiwa barua hiyo unaonyesha wazi kuwa, wamekubaliana na uamuzi wao wa kuandamana, jambo linalowafanya waendelee kuratibu maandamano hayo kupitia baraza lao.

“Tunaendelea kuratibu maandamano katika kipindi hiki cha mpito, ambacho Baraza la Vijana linakutana kichinichini kwa ajili ya kujadili suala hili, kwa sababu kila tunavyolalamika hatusikilizwi, jambo ambalo limetufanya tufikie uamuzi huu, kilichobaki ni kupambana na hali zetu,” alisema Katambi.

Pia alisema maazimio mengine yanayotarajiwa kutolewa na baraza hilo ni pamoja na kuwataka wananchi kutumia mitandao ya kijamii kwa ajili ya kukosoa kazi za Jeshi hilo na Serikali pamoja na kutoa matamko ya kulaani vitendo vya viongozi wa upinzani kukamatwa.

Alisema hadi sasa mambo hayaendi sawa, jambo linalowafanya wapambane na hali hiyo ili kuhakikisha haki inatendeka na Jeshi hilo linaacha kuibeba CCM, badala yake litimize majukumu yake kwa mujibu wa sheria.

Katambi alisema hawana dhamira ya  kuona amani ya nchi inavurugika, ila wanachokitaka wao ni kuhakikisha haki inatendeka kwa vyama vyote na si chama kimoja, jambo linalowafanya waone kama wanakandamizwa.

“Chuki ikizidi, wananchi wanaweza kufanya uamuzi mgumu ambao ni pamoja na kuchukua sheria mkononi ili kutafuta haki, jambo ambalo limetufanya tuandike barua kwa viongozi hao ili kuwazuia wananchi wasifike uko,” alisema.

Pia alisema wanachokitaka wao ni kuhakikisha kuwa jeshi hilo linafanya kazi kwa weledi bila ya kuegemea upande wowote wa chama kama ilivyo sasa na kama wataona linakwenda kinyume watalazimika kumwandikia barua Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba, ili kumweleza malalamiko yao pamoja na kwenda mahakamani wanapoamini wanaweza kupata haki zao.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles