27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

WANAFUNZI TUSIIME WASAIDIA WASIOJIWEZA

Na MWANDISHI WETU – DAR ES SALAAM

WANAFUNZI wa Shule ya Msingi Tusiime ya Tabata, jijini Dar es Salaam wametoa msaada wa vyakula na vitu mbalimbali kwa watu wasiojiweza wanaolelewa katika kituo cha Mama Teresa cha Mburahati, Dar es Salaam.

Msaada huo, uliotokana na michango ya wanafunzi wa shule hiyo, ni pamoja na unga, mchele, mafuta ya kupikia na vinywaji vya aina mbalimbali.

Akizungumza baada ya kukabidhi msaada huo, mmoja wa wanafunzi wa Tusiime, Agnes Heke, alisema walianza kuchangishana wenyewe kwa muda mrefu, lengo likiwa ni kusaidia watu wanaolelewa kwenye kituo hicho.

Alisema dhamira ya kusaidia wenzao wa kituo hicho inatokana na mafundisho ya upendo wanayofundishwa wakiwa shuleni Tusiime.

“Tumekuwa tukifundishwa kuwajali wenye shida na kwa kweli tulianza kuchangishana muda na leo (jana) hii tumeona hiki tulichopata tuwape wenzetu, huu ni mwanzo maana kadri tutakavyokuwa tunapata tutarudi kuwasaidia,” alisema Agnes.

Naye Mkuu wa Taaluma wa Tusiime, Maxon Wilson, alisema msaada uliotolewa na wanafunzi hao ni sehemu tu na wameahidi kuendelea na moyo huo wa upendo kwa wenzao.

Alisema msaada uliotolewa na wanafunzi hao unadhihirisha kuwa, mafunzo ya maadili na kuwapenda wenzao wanayopata shuleni yamewaingia na wanayazingatia kwa dhati.

Mmoja wa wazee wanaolelewa na kituo hicho, Elizabeth Daudi, aliishukuru shule hiyo kwa namna ambavyo imewafundisha wanafunzi wake kuwa na upendo kiasi cha kuamua kuchanga kwa ajili ya wenzao.

“Msaada huu ni ishara kwamba mafunzo ya upendo mnayoyapata shuleni yamefanya kazi, hatukutarajia kupata msaada kama huu, tunawashukuru na Mungu awazidishie,” alisema kwa niaba ya wenzake.

Alisema msaada huo umekuja wakati mwafaka, kwa sababu mara kwa mara huwa wanaishiwa vyakula.

“Hatuna maneno ya kutosha kuelezea furaha yetu, tunaomba watu wengine waige mfano wa Tusiime, waone watu  wanaolelewa hapa ni wa jamii nzima,” alisema.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles