22.9 C
Dar es Salaam
Sunday, June 23, 2024

Contact us: [email protected]

PATACHIMBIKA LEO KATI YA MSONDO NGOMA, MASTAA WA DANSI

 

NA VALERY KIYUNGU

LEO ndio leo! Ndivyo unavyoweza kusema kufuatia tamasha la muziki wa dansi, Dimba Music Concert litakalofanyika leo katika Ukumbi wa Travertine Magomeni jijini Dar es Salaam na kuwakutanisha mastaa wao pamoja na wakali wa muziki huo.

Tamasha hilo lililokuwa likisubiriwa kwa hamu kubwa na mashabiki wa muziki huo, litahusisha burudani kutoka kwa wanamuziki kutoka bendi kongwe ya Msondo Ngoma dhidi ya timu ya Taifa ya muziki wa dansi.

Maandalizi ya onyesho hilo yamekamilika na hivi sasa unasubiriwa wewe msomaji ambaye upo Dar es Salaam na maeneo ya jirani kusogea ukumbuni kupata burudani kwani waandaaji wa onyesho hilo wameweka utaratibu mzuri utakaokidhi kiu yako ya muziki mzuri.

Ni burudani ambayo imekuwa kama mpambano baina ya hizo pande mbili yaani Msongo Ngoma na timu ya Taifa ya muziki wa dansi kufuatia majigambo ya wanamuziki hao yaliyodumu takribani mwezi mmoja sasa.

Akizungumza na Old Skul hivi karibuni jijini Dar es Salaam, Kikumbi Mwanza, Mpango King Kiki, alisema leo katika Ukumbi wa Traverntine patachimbika kutokana na yeye pamoja na wanamuziki wenzake kujinoa vyema.

King Kikii ambaye ni miongoni mwa wanamuziki wanaounda kikosi cha timu ya Taifa ya Dansi, alisema onesho hilo ni la aina yake pia litaweka historia, tofauti na mengine ambayo yaliwahi kufanyika hapa nchini.

“Onesho hili ni kabambe tena litakuwa la kihistoria kwani halijawahi kutokea, mimi na kundi langu tumepanga kuwapa burudani safi mashabiki,” anasema mwanamuziki huyo ambaye pia ni kiongozi wa bendi yake ya La Capital maarufu kama Wazee Sugu anayetamba na wimbo wake unaoitwa Kitambaa Cheupe.

Baadhi ya wanamuziki wengine wanaounda kikosi cha timu ya Taifa ya Dansi ni pamoja na Ali Choki ‘Mzee wa Farasi’, Juma Kakere, Mwinjuma Muumin maarufu ‘Kocha wa Dunia, Hassan Rehan Bitchuka,  Hussein Jumbe ‘Mzee wa Kuchechemea’,  Nyoshi El Saadat na Adolf Mbinga.

Kwa upande wa bendi ya Msondo Ngoma baadhi ya wanaotarajia kutoa burudani ni pamoja na Said Mabela, Zahoro Bangwe maarufu kama ‘Kidevu Cheupe’, Othman Kambi, Hassani Moshi ‘TX Junior’ Roman Mng’ande, Hamisi Mnyupe na Juma Katundu, ambaye atawakumbusha mashabiki sauti za marehemu Suleman Mbwembwe na Maalim Gurumo.

Akizungumza na mwandishi wa makala haya hivi karibuni, Katundu alisema bendi yake imejipanga vema, katika kuwaburudisha mashabiki ambao watafika kwenye Ukumbi wa Traventaine uliopo Magomeni jijini Dar es Salaam.

Katundu ambaye pia kiongozi wa jukwaa bendi ya Msondo Ngoma, anasema katika kuhahakikisha bendi yake inakonga nyoyo za mashabiki wa muziki wa dansi, yeye na wanamuziki wenzake walilazimika kuweka kambi maalumu.

“Leo pale Travertine hakutakuwa na mchezo kwani patachimbika, hakutakuwa na kingine cha zaidi bali ni kazi tu,” alisema mwanamuziki huyo ambaye ni kiraka hapo Msondo Ngoma.

Onesho hilo na mengine ya bendi zaidi ya moja huwa hayana majaji bali mshindi huamuliwa na mashabiki ambao leo watahudhuria kwenye ukumbi huo, hivyo jitokeze leo uwe jaji wa mpambano huu wa Msondo Ngoma na timu ya Taifa ya Dansi.

Maoni yalete hapa 0714288656

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles