24.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, May 22, 2024

Contact us: [email protected]

SHABIBY AKERWA MGOGORO WA DC, DED, WATUMISHI

Na Ramadhan Libenanga, Gairo

MBUNGE wa Gairo (CCM), Ahmed Shabiby, ameelezea kukerwa na mgogoro uliopo kati ya wakuu wa idara wa halmashauri, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Gairo (DED), Agnes Mkandya na Mkuu wa Wilaya ya Gairo, Siriel Mchemba.

Akizungumza mjini hapa jana, Shabiby, alisema mgogoro huo umekuwa kikwazo kikubwa cha maendeleo katika wilaya hiyo kutokana na uhusiano mbaya kati ya Mchemba, watumishi wa halmashauri hiyo na Mkandya.

Shabiby alisema kutofanya kazi kwa pamoja kwa makundi hayo mawili yenye dhamana moja ya kutumikia wananchi, kunasababisha shughuli nyingi za maendeleo kukwama.

“Kwa sasa natafuta nafasi ya kumwona Rais Magufuli ili anisaidie kumaliza mgogoro huo kwani maendeleo yanakwama,” alisema.

Hivi karibuni wakuu wa idara katika halmashauri hiyo walimwandikia barua Mkandya kutishia kutofanya kazi pamoja na Mchemba kwa madai ya kuwatolea lugha za kuwadhalilisha na kashfa kwenye vikao na mikutano ya nje mbele ya wananchi.

Gazeti hili lilizungumza na watumishi, wakuu wa idara katika halmashauri hiyo na madiwani walisema mkuu huyo wa wilaya amekuwa akitumia vibaya kifungu cha sheria namba 83 kinachompa nafasi Mchemba kumweka mahabusu mtu kwa saa zisizozidi 48.

Akizungumzia hali ya kutokuwepo na uhusiano mzuri kikazi kati ya watumishi hao, Shabiby, alisema ni mfumo wa ubabe kwa Mchemba dhidi  ya watumishi hao na lugha zisizofaa kutolewa kwenye vikao.

“Hata hivyo, nashangaa kuona kamati hizo zinazokuja kuhoji zinahoji watumishi na wananchi na kuondoka mbona mimi mbunge sihojiwi lolote kwa kuwa mimi ndiko jimboni kwangu,” alisema.

Shabiby alisema pamoja na kamati mbalimbali kuwaita na kuwataka kumaliza tofauti zao na kufanya kazi walizotumwa,  lakini bado hali imekuwa tata kwa Mchemba.

Pia alisema hali hiyo inajulikana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, Naibu Waziri wa Tamisemi, Suleiman Jaffo na Kamati ya Siasa ya CCM ya Mkoa wa Morogoro na Wilaya ya Geita wameshatoa onyo la kuwataka kumaliza mgogoro wao lakini hali bado mbaya.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Gairo, Rachel Nyangasa, alisema kumekuwa na malalamiko mengi ya madiwani wake na watumishi wa halmashauri dhidi  ya matukio ya ubabe dhidi ya Mchemba.

Alisema amekuwa akitishia kuweka ndani watumishi na wengine wakiwekwa ndani pasipo kesi za msingi ambazo zingemalizika katika vikao vya pamoja  kwa busara.

“Vitisho vya kuwekwa ndani kwa wakuu wa idara na watumishi ndani ya halmashauri kunaondoa hamasa ya kufanya kazi, kama hivi karibuni mkuu wa idara ambaye ni mhandisi wa maji, Herman Mundo, alikamatwa na polisi na kuswekwa rumande kwa amri ya mkuu wa wilaya wakati akishauri utaratibu mzuri wa ugawaji maji,” alisema.

Alisema Mundo aligomea agizo la Mchemba kutaka maji yatoke kwa saa sita katika mgawo wa sehemu moja wakati utaratibu ni saa tatu ili kuweza kupeleka maji katika maeneo mengi ya wilaya kutokana na maji kupungua katika vyanzo vya maji.

“Lakini ushauri huo wa kitaalamu ulisababisha mhandisi huyo kufunguliwa kesi na kuagiza Jeshi la Polisi kumweka ndani kwa saa tatu,” alisema.

Naye Mkandya alipoulizwa kuhusiana na suala hilo alikiri kuwa wakuu wa idara wamemwandikia barua ya kutishia kugoma kuambatana naye katika ziara zake kutokana na kuwa na lugha kali zenye kuwakwaza watendaji na kuwafanya kukosa hari  ya kufanya kazi.

Pia alisema lakini tayari ameshazungumza na wakuu hao wa idara na kuwataka kusitisha mgomo huo na kuwataka kuendelea kutoa ushirikiano kwa Mchemba.

“Mimi kama mkurugenzi siko  tayari kuona shughuli za maendeleo zinakwama katika wilaya yangu, nitaweka tofauti zetu pembeni ili kuhakikisha tunafanya kazi tuliyotumwa na Rais Dk. John Magufuli,” alisema.

Kwa upande wake, Mchemba, alipopigiwa simu kuhusu malalamiko hayo ya watendaji katika halmashauri alikana na kudai kuwa yupo vizuri na wakuu wa idara na watumishi wa halmashauri hiyo.

“Mimi sina tatizo na wakuu wa idara wala watumishi wa halmashauri, wewe kama umesikia hayo mpigie mkurugenzi wa halmashauri ndio msemaji wa halmashauri,” alisema.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
587,000SubscribersSubscribe

Latest Articles