24.4 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Tanzania inahitaji Jeshi la Polisi la kisayansi 

3JESHI la Polisi ndicho chombo pekee kilichopewa mamlaka ya kulinda usalama wa raia pamoja na mali zao. Kukamata wavunja sheria na kupambana na uhalifu ni malengo makuu ya jeshi hili ndani ya nchi.

Pamoja na wananchi kuelewa jukumu mahususi la Polisi kuwa ni kupambana na uhalifu lakini katika hali ya mazoea baadhi yao   wakisikia neno Polisi huhisi ni watu ambao wako kwa ajili ya kukamata watu kwa kutumia nguvu nyingi.

Inawezekana hisia hizi za kuchukulia Jeshi la Polisi kuwa chombo cha mabavu ni la kimfumo unaotokana na historia yake tangu lilipoundwa enzi za ukoloni likiwa na dhima ya kulinda masilahi ya watawala.

Mazoea ya kulinda masilahi ya watawala tangu enzi za ukoloni ndio mara nyingi yamekuwa yakisababisha Jeshi la Polisi kutumia nguvu nyingi hata kwenye maeneo yasiyostahili na hivyo wananchi kulichukulia kama chombo cha ukatili kwa ajili ya kulinda mabwana wakubwa.

Ni ukweli usiopingika kwamba mbali na mtazamo hasi dhidi ya jeshi hili lakini tangu nchi yetu ipate uhuru pamekuwepo na mabadiliko chanya makubwa ambayo yamekuwa yakifanywa na chombo hiki ili kukidhi matarajio ya wananchi na ndiyo maana wananchi siku hizi wanalilia kujengewa vituo vingi vya Polisi ili kukabiliana na uhalifu.

Kutokana na mabadiliko ya kisiasa, kiuchumi, kijamii, kisayansi na kiteknolojia, dunia yetu si salama tena kwani hata uhalifu umekuwa ukikua kulingana na mabadiliko hayo tunayoyashuhudia kwa hivi sasa.

Naamini kabisa kutoka ndani ya nafsi yangu kwamba pamoja na mikakati mizuri inayofanywa na Jeshi la Polisi ili kuwa kimbilio la wananchi bado itakuwa si sahihi kuhisi kuwa msingi mkubwa wa jeshi katika kutatua matatizo ni kutumia nguvu.

Uhalifu unaofanyika duniani kwa hivi sasa unajikita zaidi katika kutumia maarifa na ubunifu wa hali ya juu bila ya nguvu ya misuli.  Ni uhalifu wenye sura ya kujifunza na kuiga kwa kutumia nguvu ya teknolojia inayoifanya dunia kuwa kijiji kama si kitongoji.

Mauaji yaliyokuwa yakifanyika enzi za analojia ni  tofauti na mauaji yanayofanyika enzi za dijitali. Raia wa Tanzania anaweza kumwaga damu ya maelfu ya watu kwa kujifunza  kupitia mitandao baada ya kuona wengine  wanavyojitoa mhanga na kuangamiza watu wasio na hatia katika mataifa mengine.

Mashambulizi ambayo hufanyika katika maeneo mbalimbali kama vile kwenye mahakalu ya ibada na sehemu nyingine zenye mkusanyiko,  washambuliaji huwa hawatumii nguvu nyingi kama Polisi wafanyavyo bali ni maarifa ya hali ya juu yenye kuangalia ni wapi    kuna udhaifu wa ulinzi.

China mbali na kukua kiviwanda pia ni taifa linalochukua nafasi ya tano kidunia kwa  kumiliki Jeshi la Polisi lililo bora na imara. ‘‘The People’s Armed Police Force (PAPF)’’ katika nchi hiyo lina majukumu ya kulinda usalama wa taifa, uthabiti katika jamii na kuhakikisha watu wanaishi na kufanya kazi katika mazingira yenye usalama.

Wajibu mkubwa wa ‘PAPF’ nchini China ni kutunza amani kwa njia yoyote ile na kuondoa uhalifu katika jamii ya kichina ambapo uhalifu mwingi uliozoeleka ni kama vile: utakasaji pesa, madawa ya kulevya, rushwa, biashara ya binadamu, udanganyifu na usambazaji noti feki za fedha.

Inakadiriwa  China kuna watu wapatao bilioni 1.5, hivyo si kazi rahisi kulinda na kusimamia sheria katika nchi yenye watu wengi namna hiyo. Takwimu zinaonyesha China imefanikiwa kutunza na kulinda amani na hivyo uhalifu kupungua kwa kiasi kikubwa  ukilinganisha  na siku za nyuma hii ni kwa mujibu wa ripoti ya kielelezo cha uhalifu ya mwaka 2015 inayoweka viwango kidunia.

Jambo la msingi katika kutunza usalama wa umma nchini humo ni sera ya usimamizi bora ambapo maeneo mengi yamegawanywa katika vipande na kupangiwa askari wa kutosha ili kufanya doria, huku kamera za kurekodi matukio ya uhalifu  pamoja na askari jamii vikiwa vimewekwa maeneo mengi. Ni katika mazingira haya nchi inakuwa kwenye ulinzi wa uhakika masaa 24.

Wahalifu wa ubakaji au unyang’anyi hupewa adhabu kubwa na ikiwezekana adhabu ya kifo. Si hivyo tu hata matendo mengine ya vitisho vinavyoondoa utulivu wa nchi na kuwafanya wananchi waishi kwa hofu huchukuliwa kuwa ni makosa makubwa nchini China.

Majeshi mengine ya Polisi nje ya China ambayo inasemekana ni bora duniani  ni CHP-Calfornia Highway Patrol la Marekani, Royal Canadian Mounted la Kanada, Metropolitan Service la Uingereza, AFP- Australian Federal Police la Australia na Iceland Police la Iceland.

Ukifuatilia kwa karibu majeshi haya katika nchi hizo yamefanikiwa kudhibiti uhalifu si kwa kutumia ramli bali ni vifaa vya kisasa kama vile helikopta za kutosha, magari, kamera na mifumo ya kompyuta.

Ni majeshi ambayo yamesheheni maafisa/askari wachache lakini wenye nidhamu, elimu ya uhakika na ujuzi wa kutosha katika masuala ya uhalifu. Wanao uwezo wa kufanya tafiti mbalimbali na kugundua mbinu na mikakati mipya ya kuvunja mitandao ya uhalifu kabla haijaleta madhara katika jamii.

Pamoja na kuwa Tanzania haina vita ya ndani ya wenyewe kwa wenyewe au kupigana na mataifa jirani, lakini haiko salama vya kutosha kwani vitendo vya kutisha kama mauaji, ubakaji, ulawiti  bila kusahau ujambazi wa kutumia silaha vinazidi kuota mizizi kila kukicha.

Katika muktadha huu wa ukosefu thabiti wa usalama wenye kusindikizwa na harufu ya ugaidi wa kimataifa kuna haja Jeshi la Polisi kujitathimini upya kama limejipanga vizuri katika kumiliki rasilimali watu wenye  nidhamu,  elimu ya uhakika na ujuzi  katika masuala ya uhalifu ambao watakuwa na uwezo wa kufanya upelelezi kisayansi na kuendesha tafiti mbalimbali.

Ulinzi na usalama havina mbadala hivyo kama Jeshi la Polisi lina mapungufu hayo ni wajibu wa serikali kuweka miundombinu imara kwa  kuwapa mafunzo ya uhakika ya ndani na nje ya nchi maafisa/askari wote bila kusahau  kuwekeza zana za kisasa kulingana na teknolojia iliyopo.

Inawezekana ikawa ujinga kama si upumbavu endapo waheshimiwa wabunge na viongozi wa serikali  watakubali kutembelea magari ya kifahari na kulala kwenye majumba  mazuri kana kwamba wako peponi wakati JWTZ, Polisi, Magereza na vyombo vingine vya ulinzi na usalama vikiwa na upungufu wa vitendea kazi ili kukabiliana na uhalifu mamboleo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles