23.9 C
Dar es Salaam
Wednesday, July 24, 2024

Contact us: [email protected]

Natamani kuijua itikadi ya siasa ya Mrema 

MREMAAAUGUSTINE Lyatonga Mrema, kwa maoni yangu ni mtu wa ajabu sana ambaye unaweza kumfanyia utafiti wa kisiasa (case study) na kutoka na kitu kizuri kabisa juu ya tabia za wanasiasa wanaopenda fadhila na kukumbukwa.

Mwaka 1995 ndio mwaka ambao wengi wetu tulianza kumshabikia, hasa pale alipoondolewa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kujiunga na chama pinzani cha NCCR-Mageuzi.

Wengi wa waliomshabikia walitamani Mrema awe ndiye rais wa nchi na kupitia mgongo wake, ndipo watu kama akina James Mbatia wakafanikiwa kuzoa kura nyingi sana za Ubunge mwaka huo.

Pengine umaarufu wa Mrema ulitokana na kazi aliyokuwa akiifanya akiwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.  Hata hivyo Mrema alishindwa kwenye kinyang’anyiro cha Urais, na mshindi wa kiti hicho alikuwa ni Benjamin Mkapa kutoka CCM.

Umaarufu wa Mrema bado haukufifia na muda mchache baada ya aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Temeke, Kihiyo kuvuliwa ushindi wake kutokana na kufoji vyeti vya shule, Mrema aliamua kujitosa kugombea kuwa Mbunge wa Jimbo hilo.  Safari hii alishinda na hata ndani ya Bunge, alikuwa akizungumza kama mpinzani.

Sina hakika sana kama kuporomoka kwa Mrema kulianza baada ya ile migogoro aliyokuwa nayo yeye pamoja na Katibu Mkuu wa chama chake, Mabere Nyaucho Marando.  Ninachokikumbuka ni kwamba baada ya kile kipindi cha kila mmoja kutangaza kumfukuza mwenzake na kisha kuamua kupatana hadharani kisha kugombana tena, Augustine Mrema aliacha kuwa Lyatonga yule tunayemfahamu na badala yake tukaanza kuamini kwamba huenda alitoka kwenye chama tawala kwa kulazimika tu, lakini moyoni bado hajahama.

Ipo mifano kadhaa ya Mrema kuwasifia hadharani wale ambao wapinzani wenzake hawawasifii.  Mwaka 2005 wakati Jakaya Kikwete akigombea urais kwa tiketi ya CCM, Mrema alitangaza kumuunga mkono.  Wala hakujisumbua kujitangaza yeye kuwa mgombea na wala chama chake hakikusimamisha mgombea urais.  Hali iliendelea hivyo kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.

Sina tatizo na Mrema kuamua kutogombea urais kwa vipindi hivyo viwili, wala chama chake kutoamua kusimamisha mgombea.  Tatizo linakuja pale ambapo anatangaza hadharani kumuunga mkono mgombea wa Chama Cha Mapinduzi, huku wakiwepo wagombea wa vyama vingine vya upinzani.  Angewaunga hao mkono, ingekuwa vizuri; angeamua kunyamaza kimya, ingekuwa vema zaidi.

Ajabu ya karne ilitokea katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.  Chama cha Mrema, Tanzania Labour Party (TLP) kilimsimamisha mgombea urais.  Kwa waliokuwa wakifuatilia kampeni za Uchaguzi Mkuu mwaka jana, watakumbuka kuwa mgombea huyo wa kiti cha urais kupitia TLP, Maxmillian Lyimo.  Kilichotushangaza ni kwamba Mwenyekiti wake wa Taifa, hakuwa naye katika kampeni hizo.

Cha kustaajabisha zaidi kilitokea pale mgombea urais kutoka CCM, John Magufuli alipotembelea Vunjo kwenye harakati zake za kampeni, Mrema alitamka kwamba anamkubali Magufuli na anamuunga mkono kwenye kinyang’anyiro hicho cha Urais.  Alishawishika sana kwamba Magufuli ndiye ambaye angeshinda na hivyo akamwomba amkumbuke katika ‘Ufalme’ wake.

Ni tabia za namna hiyo za Mrema ambazo zimekuwa zikisababisha watu wengi wajiulize kama kweli ni mpinzani, ama ni ‘opportunist’ zaidi.  Kwamba akigundua kuwa upande fulani ndio wenye maslahi zaidi basi yeye atakimbilia kuupigia debe upande huo na kuonekana akijisahau kabisa anatakiwa kuwa kambi gani.

Ni kweli kwamba kuwa mpinzani haimaanishi kwamba kila kitu kinachosemwa na Serikali pamoja na chama tawala kinatakiwa kupingwa; lakini inapotokea kwamba Mwenyekiti wa chama anashindwa hata kumuunga mkono mgombea wa kiti cha urais wa chama anachokiongoza, hilo linaibua maswali mengi zaidi.

Bahati nzuri Mrema alishindwa kutetea kiti chake cha ubunge wa Jimbo la Vunjo.  Tangu wakati huo hajasikika, lakini sasa juzi tena ameibuka na kumzungumzia Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), Maalim Seif Shariff Hamad na kudai kwamba analeta uchochezi Zanzibar, kutokana na kushawishi wafuasi wake kuupinga ‘ushindi’ wa Rais Ali Mohamed Shein.

Maalim Seif alinukuliwa akisema kwamba umefika wakati kwa Wazanzibari kutonyamazia suala la urais wa Dk. Shein, kwakuwa alipatikana kwa njia zisizo halali.  Kwamba matokeo ya uchaguzi halali uliofanyika mwaka jana yalifutwa na Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi, Jecha Salum Jecha na kile kilichofanyika mapema mwaka huu kwa kuwa na uchaguzi wa marudio, hakikuwa halali.  CUF walisusia kushiriki uchaguzi huo, licha ya kuwepo kwa wagombea wengine kutoka upinzani, Dk. Shein alipata ushindi wa zaidi ya asilimia 90.

Sasa Maalim Seif hakubaliani na ushindi wa Dk. Shein, na ndio maana akasema kwamba ni vema Wazanzibari wasiokubaliana na hilo kuungana pamoja na kuchukua hatua za kulizungumzia hilo.  Alitolea mfano kwamba mbinu mbalimbali zinatakiwa kutumika kwa ajili ya kufanikisha hilo, kama vile wananchi kukataa kulipa kodi, kuandaa siku ya mgomo, kusimamisha vyombo vyote vya usafiri na hata kupiga honi Zanzibar nzima kuonyesha hawaitaki Serikali ya CCM.

Kutokana na kauli hiyo, Mrema ameibuka na kudai kwamba Maalim Seif ni mchochezi.  Sina hakika hapa kama Mrema amejaribu kuzungumza ili asikike kwamba bado yupo katika siasa, au kama anamaanisha kweli kile anachokisema kwa moyo wa dhati au ndiyo vilevile kwamba bado hajakumbukwa na Magufuli katika ufalme wake na ndio anakumbusha kwamba bado yupo.

Nilishawahi kuandika katika makala zilizopita kwamba zipo nchi ambazo kambi ya upinzani imeshawahi kuchukua hatua kutokana na kutoridhishwa na kufanyika kwa uchaguzi ambao waliususia kwa sababu ambazo zilikuwa zinaeleweka, kama ile ya CUF huko Visiwani.

Nchini Bangladesh mwaka 1996, chama cha upinzani cha Awami League kiliamua kususia uchaguzi wa Bunge na kutaka Waziri Mkuu Khaleda Zia ajiuzulu.  Kususia huko kuliambatana na maandamano na migomo ambayo ilisababisha nchi kushindwa kujiendesha kabisa siku mbili kabla ya uchaguzi.  Kukiwa hakuna upinzani wowote, chama cha BNP kilichokuwa kikiongozwa na Zia kilishinda viti 205 kati ya 207, katika uchaguzi ambao ulikuwa na muitikio mdogo mno.

Hata hivyo, maandamano na migomo iliyoendelea ilimlazimisha Zia akubali kwa shingo upande kuitisha uchaguzi mwingine, na safari hii Awami walishiriki na kuzoa viti 147 kati ya 299, huku chama cha BNP kikipata viti 116.

Sidhani kama huo ni uchochezi.  Na tukichukulia mfano wa CUF, tukumbuke kwamba tofuati na matarajio ya wengi, chama hicho kiliamua kutulia sana kipindi chote hadi kuelekea uchaguzi wa marudi huko Zanzibar, na hakikufanya fujo yoyote hata siku ya kuapishwa kwa Dk. Shein.  Kuzungumzia mbinu mbadala ambazo hazisababisha mauaji yoyote, kunaitwaje uchochezi?

Kwa maoni yangu, Mrema hapa ndiye mchochezi wa kutaka kuamanisha watu kwamba kinachofanywa na wapinzani wa kweli, si haki.  Tulishatambua siku nyingi kwamba yeye si mpinzani wa kweli na mara nyingi matamshi yake yamekuwa ya kujipendekeza na kutafuta kupewa wadhifa.  Amechoka.  Apumzike.  Angalau tutaweza kumkumbuka kwa yale ya zamani aliyoyafanya ambayo yalisababisha awe kipenzi cha wanyonge kwa wakati ule.  Akizidi kuropoka, hata yale mazuri tutayasahau.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles