31.2 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Tanzania, Finland kuimarisha uhusiano

Sauli_NiinistöNa Mwandishi Maalumu, Finland
UHUSIANO baina ya Tanzania na Finland utaendelea kuimarishwa zaidi kuliko ilivyo sasa, imeelezwa.

Kauli hiyo imetolewa jana mjini Helsinki na Rais Sauli Niinisto wa Finland, katika mazungumzo yake na Rais Jakaya Kikwete yaliyofanyika Ikulu nchini hapa.
“Uhusiano wetu ni wa muda mrefu, ni uhusiano ambao umedumu kwa miaka 50, tumekuwa na uhusiano ambao umeleta maendeleo ya kiuchumi kwa Tanzania.” Rais Niinisto alisema na kuongeza: “Hii inatupa nafasi ya kutafuta mbinu mpya za kuleta maendeleo na kukuza ushirikiano huu zaidi.”
Rais Kikwete aliwasili Helsinki Juni mosi mwaka huu kwa ziara ya kikazi ya siku tatu ambapo pamoja na mambo mengine ametumia nafasi hiyo kumshukuru Rais Niinisto kwa mwaliko wake ambapo amemwelezea hali ya kisiasa, kiuchumi na kijamii nchini Tanzania.
Alimweleza mwenyeji wake kuhusu Uchaguzi Mkuu ujao nchini Tanzania na kuweka bayana kuwa, “Nimekuja kukushukuru pamoja na wananchi wa Finland kwa ujumla kwa mchango na misaada yenu ya maendeleo kwa Tanzania tangu nchi yetu ipate uhuru hadi leo na bado uhusiano wetu upo imara,” alisema Rais Kikwete.

Aliiomba Finland iendelee kuisaidia Tanzania katika jitihada zake za kukuza uchumi na kuletea watu wake maendeleo.
Rais Kikwete pia alitumia ziara hiyo kuwaaga na kuwashukuru viongozi na washirika wa Tanzania katika maendeleo, ambao wametoa mchango mkubwa na msaada kwa Serikali na wananchi wa Tanzania katika kipindi chake cha uongozi.
Katika ziara yake nchini humo, Rais Kikwete alifanya mazungumzo na wabunge wa Finland ambao ni viongozi wa vyama vya siasa nchini humo, wakiongozwa na Spika wao Maria Lohela.
Spika Lohela, alisema ndiye kiongozi mkubwa wa nje kutembelea na kufanya mazungumzo na wabunge hao ambao wameshika nyadhifa zao mpya kuanzia Aprili mwaka huu.
Rais Kikwete amemueleza Spika Lohela kuhusu kuisha kwa muhula wa Bunge la sasa nchini Tanzania ambapo Spika Lohela alisema Bunge la Finland, linapenda kuendeleza ushirikiano na Bunge la Tanzania na hivyo kutoa mwaliko kwa wabunge wapya watakaochaguliwa katika uchaguzi wa Oktoba, mwaka huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles