PATRICIA KIMELEMETA, Dar es Salaam
SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco) leo linatarajia kuweka hadharani deni la Sh bilioni 121 inazowadaiwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).
Kauli hiyo imetolewa siku chache baada ya Rais John Magufuli kuliagiza shirika hilo kuikatia umeme SMZ baada ya kushindwa kulipa deni hilo kwa ajili ya kusambaza umeme visiwani humo.
Rais Magufuli alitoa kauli hiyo wakati wa kuweka jiwe la msingi katika kituo cha kupooza umeme wa kilovoti 132 kilichopo Mtwara.
Alikuwa kwenye ziara ya siku nne ya mikoa ya Pwani, Lindi na Mtwara, wiki iliyopita.
Ofisa Habari na Uhusiano wa Tanesco, Leyla Muhaji amesema shirika haliwezi kuficha suala hilo kwa sababu tayari Rais Magufuli amelizungumzia.
Alisema uongozi wa shirika hilo umepanga kutoa mchanganuo wa deni hilo tangu lilipoanza hadi lilipofikia wananchi waweze kulielewa.
“Hatuwezi kuficha deni la Zanzibar kwa sababu tayari Rais Magufuli ameliweka wazi.
“Mimi na viongozi wangu tutajipanga tuweze kutoa mchanganuo wa deni lenyewe tangu lilipoanza hadi lilipofikia, kwa sasa tupo safarini lakini kesho(leo), tutakuwa ofisini,”alisema Muhaji.
Alisema wataandaa taarifa hiyo ambayo itatolewa kwa waandishi wa habari waweze kuwahabarisha wananchi.
Rais Magufuli alisema suala la umeme lisigeuzwe kuwa la siasa.
Alisema wadaiwa sugu wa umeme wakatiwe umeme kwa vile shirika hilo halipo kisiasa bali kwa utendaji, hivyo wadaiwa sugu wote wanapaswa kulipa madeni hayo na watakaoshindwa wakatiwe umeme hata kama ni Ikulu.
Alisema Tanesco inapaswa kufuatilia madeni yake popote kwa sababu wakati mwingine fedha zinakuwa zinatolewa wizarani lakini wanaona umeme siyo muhimu.