28.2 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Tambwe aweka rekodi Afrika

Amissi TambweBADI MCHOMOLO, DAR ES SALAAM

MSHAMBULIAJI wa mabingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, Amissi Tambwe, ameweka rekodi mpya ya kuwa mfungaji bora kwa ligi za Afrika ambazo zimemalizika hivi karibuni.

Mchezaji huyo raia wa Burundi, amekuwa mchezaji namba moja kwa kupachika mabao mengi msimu huu wa Ligi Kuu akiwa na jumla ya mabao 21 na kuongoza katika orodha ya wafungaji wa klabu mbalimbali Afrika.

Nchini Namibia, mshambuliaji wa klabu ya Orlando Pirates, Terdius Uiseb, amekuwa kinara wa ligi hiyo kwa kufunga mabao 20, wakati timu yake ikishika nafasi ya nane kwenye msimamo wa ligi.

Ligi Kuu nchini Botswana, mshambuliaji wa klabu ya Gilport Lions, Matthews Nyamadzawo, amemaliza ligi huku akifunga mabao 19, wakati huo timu yake ikishika nafasi ya 10 kwenye msimamo wa ligi.

Mshambuliaji wa klabu ya URA ambayo inashiriki Ligi Kuu nchini Uganda, Robert Ssetongo, amekuwa nyota wa ligi hiyo kwa kufunga mabao 18 wakati huo klabu yake ikimaliza ligi katika nafasi ya nne.

Nchini Afrika Kusini msimu ulimalizika huku mshambuliaji wa klabu ya Mpumalanga Black Aces, Collins Mbesuma, akicheka na nyavu mara 14, wakati timu yake ikishika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi.

Wakati huo ligi ya nchini Malawi imemalizika kwa nyota wa klabu mbili kugongana kwa mabao, mshambuliaji wa klabu ya Nyansa Big Bullets, Chiukepo Msowoya na Innocent Bokosi wa Red Lions, wote wakiwa na mabao 14.

Kwa upande wa Ligi Kuu nchini Morocco, nyota wa klabu ya Far Rabat, Mahdi Naghmi, alifunga mabao 13, huku timu hiyo ikishika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi.

Ligi ya nchini Algeria, mshambuliaji wa klabu ya MC Oran, Mohammed Zubya aliibuka kidedea kwa ufungaji bora akiwa na mabao 13, huku timu yake ikishika nafasi ya 10 katika msimamo wa ligi.

Rekodi hiyo ya Tambwe inaweza kumwezesha kuendelea kukaa katika ufungaji bora ligi za Afrika kama hakutatokea mchezaji wa kupita idadi ya mabao 21 aliyonayo kwenye ligi ambazo hazijamalizika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles