24.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

Takukuru yawashikilia Wanafunzi 59 kwa udanganyifu wa mitihani

Na Nyemo Malecela, Kagera

Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Kagera inawashikilia watu 67 wakiwemo wanafunzi 59, wakufunzi wanne, wakuu wa vyuo vya Ufundi VETA Kagera na Tuinuane VTC na wasimamizi wa mitihani wawili kwa tuhuma za udanganyifu katika mtihani wa Taifa wa Elimu ya Ufundi.

Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Kagera, John Joseph amesema leo Desemba 15, kuwa katika Chuo cha Ufundi cha VETA kilichopo Manispaa ya Bukoba inawashikilia wanafunzi 38, wakufunzi wawili ambao walikuwa wasimamizi wa mitihani, Francis Mwangosi na Ssenabuly Daud pamoja na Mkuu wa Chuo hicho, Baluhi Mayala.

“Kwa upande wa Chuo Tuinuane VTC kilichopo katika Kijiji cha Kabale Kata ya Karabagaine Halmashauri ya Bukoba tunawashikilia wanafunzi 21, wakufunzi wawili ambao ni Charles Byabachwezi na Verdiana Myaka, Mkuu wa Chuo, Emmanuel Jonas pamoja na wasimamizi wawili wa mitihani ambao ni waajiriwa wa Chuo cha Ufundi Veta Kagera ambao ni Evodius Kaiza na Aderick Anastaz,” amesema.

Pamoja na kukamatwa kwa watuhumiwa hao katika Chuo cha VETA Kagera pia Takukuru imekamata simu 41 ambapo simu 38 ni za wanafunzi na tatu za wakufunzi ambazo waliingia nazo kwenye katika chumba cha mtihani wa Taifa wa elimu ya ufundi.

“Simu hizo zilikuwa zinatumiwa na wanafunzi waliyokuwa katika chumba cha mtihani kwa kurusha maswali kwenye kundi la WhatsApp lililopewa jina la Secret Magic na wakufunzi walikuwa ofisini walijibu maswali hayo na kisha kuwatumia wanafunzi majibu husika kwenye kundi hilo wakiwa katika chumba cha mtihani.

“Na katika Chuo cha Tuinuane VTC ambacho pia kimesajiliwa na Veta pia tumekamata simu 21 za wanafunzi, simu nne za wakufunzi pamoja na fedha taslimu shilingi 151,000 ambazo zilichangwa na wanafunzi kwa ajili ya kuwapatia wasimamizi wa mitihani hiyo,” amesema Joseph.

Joseph alisema na kwa upande Chuo cha Tuinuane VTC waliunda kundi lililopewa jina la Kabale VTC ambalo pia wanafunzi walilitumia kuweka maswali magumu kwenye mtihani huo kwa kuyapiga picha na wakufunzi kuyajibu na kuwarudishia majibu hayo kwenye kundi hilo na wanafunzi ambao hawakuwa na simu zisizokuwa za kupangusa ‘smartphone’ walitumiwa majibu hayo kwa njia ya ujumbe wa kawaida kwenye simu zao.

“Tumewashikilia watuhumiwa hao kufuatia taarifa za kiintelijensia kuwa kumekuwepo na udanganyifu katika mitihani hiyo kwa wakufunzi kuwapatia majibu ya mitihani wanafunzi pamoja na wanafunzi kuingia na simu za mikononi katika vyumba vya mitihani, makosa ambayo ni kinyume cha sheria.

Uchunguzi unaendelea ukikamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani,” amesema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles