Na SHEILA KATIKULA- MWANZA
TAASISI ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (Takukuru) mkoani Mwanza imewataka wagombea wote wa nafasi za kisiasa kuacha kujihusisha na vitendo vya rushwa katika kipindi cha kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajia kufanyia Oktoba mwaka huu, huku ikionya wale wanaotoa taarifa za uongo kwa leo la kuchafuana.
Akizungumza jijini Mwanza juzi na wagombea 105 wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Nyamagana, Mkuu wa Dawati la Upelelezi wa Takukuru mkoani hapa, Innocent Shetui, alisema wagombea wanapaswa kujiepusha na vitendo vya rushwa.
Alisema ni vema kila mgombea kuwa na sifa kwani wanaotoa rushwa ili majina yao yapitishwe wanaminya haki ya wananchi kuchagua kiongozi wanayemtaka .
“Wapo baadhi yenu wameanza kutoa taarifa za uongo kwenye vyombo vya ulinzi na usalama ili kuchafuana, sisi tunachunguza taarifa zote mnazotuleta na tutakapo baini wewe ni muongo tutawaambia viongozi wenu wa chama kuwa hauna sifa, zipo mbinu nyingi mlizonazo za kukaa vikao usiku, tunazijua acheni kufanya hivyo tukiwabaini tutawachukulia hatua kali za sheria.
“Nimekuja kuwakumbusha kusoma kanuni zenu ili mzijue, sisi hatutamuonea mtu yoyote kwasababu Takukuru ni ya Watanzania wote, kila mmoja anahaki ya kuleta taarifa za ukweli na tutazishughulikia bila kumuonea mtu,” alisema Shetui.
Kwa upande wake Katibu wa CCM, Gedfrey Kavenga alisema kipindi hiki wagombea wamejitokeza kwa wingi kwa sababu ya utendaji mzuri wa Rais John Magufuli.
Aliwataka wapambe wa wagombea kuacha kuwachafua wagombea wengine na kuona wake ni bora kuliko wa mwenzie.
Aidha Katibu wa Mwenezi wa Wilaya ya Nyamagana, Mustapha Baningwa, alisema mwaka huu watu waliojitokeza kutia nia kwenye majimbo yaliyo kwenye wilaya hiyo ni 117, waliochukua fomu 108 na waliorudisha 105.
Baadhi ya wagombea hao wakizungumza kwa nyakati tofauti, walisema utendaji mzuri wa Rais Magufuli wa kuleta maendeleo kila sehemu, umewafanya wajitokeze kwa wingi kuwania nafasi ya ubunge tofauti na ilivyokuwa huko nyuma ambapo kulikuwa na watu wachache waliokuwa wakijitokeza kuwania nafasi mbalimbali.
Pia waliwaomba wagombea wengine kuacha kuchafuana kwani kuna maisha baada ya uchaguzi na kuwataka wafanye siasa zenye uadilifu na kujiepusha na vitendo vya rushwa.