26.2 C
Dar es Salaam
Sunday, January 29, 2023

Contact us: [email protected]

Wagombea wengine CCM waingia mitini, Chadema wazidi kupitisha wagombea

Na Waandishi wetu

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimezidi kupata wagombea ubunge kwenye Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba, huku kwa upande wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao juzi walifunga zoezi la kuchukua na kurejesha fomu, wengine wakishindwa kurudisha fomu walizochukua.

Wakati Chadema wakiwa kwenye hatua za mwisho kupata wagombea ubunge watakaoshiriki uchaguzi huo, CCM ambao kwa siku mbili kati ya nne za uchukuaji fomu walijitokeza watu zaidi ya 8,000, wanatarajia kupiga kura Julai 20 kupata wagombea watakaopeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

CHADEMA NA LEMA ARUSHA

Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, kwa tiketi ya Chadema, Godbless Lema, ameshinda kura za maoni kwenye chama chake kwa kupata kura 181 kati ya 203, hivyo kuwa mgombea wa chama hicho kwenye uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.

Lema ambaye pia ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Chadema, alikuwa akishindana na aliyekuwa Diwani wa Kata ya Sombetini, Ally Bananga ambaye amepata kura 22.

Akitangaza matokeo ya uchaguzi huo, Msimamizi wa Uchaguzi huo Michael Kilawila alisema wapiga kura walikuwa 203 na Lema ameshinda kwa asilimia 89.1.

Alisema awali kulikuwa na wagombea wanne ambapo wawili kati yao walipeleka barua za kujiondoa ambao ni Emma Kimambo na Reginald Massawe.

LEMA

Awali Lema akiomba kura kwa wajumbe hao aliwaomba kumchagua na kuacha kupiga kura kishabiki ambazo baadaye zinasababisha madhara ndani ya chama.

Alitolea mfano mwanzoni mwa mwaka huu walifanya uchaguzi lakini badala ya wapiga kura kuchagua viongozi makini walipiga kura kishabiki ambapo baadhi ya viongozi wa wilaya waliochaguliwa katika uchaguzi huo walihamia CCM. 

“Ndugu wajumbe wenzangu mlichagua viongozi wa wilaya kishabiki, nikasema sitaacha mkoa uende kwenye hiyo familia na nilikuwa sina mpango wa kugombea uongozi wa kanda ila nililazimika ili tuwe na viongozi bora,”

“Huu si mkutano wa kishabiki na hii kazi imenipa mateso, dhihaka, matusi na ningeweza hata kuiacha leo. Mji huu mkitaka kesho msiende kwenye uchaguzi mkuu chagueni mtu ambaye si sahihi, fanyeni maamuzi ya busara.

“Kazi hii sifanyi kwa sababu ya pesa, nafanya kwa sababu ya wito na nyie ni mashahidi na hakuna diwani mji huu aliyeshinda bila nguvu zangu hata mgombea mwenzangu nilimsaidia hadi akashinda, nitaona dhihaka kutoka kwenu eti Lema vipindi viwili vinamtosha.

“Tuna hali nzuri katika uchaguzi huu kuliko uchaguzi wowote, tujipange, najua kuna waliokuja hapa wivu tu naye miaka 10 inatosha tumtoe, huu wivu ulikuwepo mkutano mkuu taifa, wakitaka kumtoa Mbowe (Freeman Mbowe, Mwenyekiti Chadema) fikra mbadala siyo kubadilisha mtu, huwezi kutoa komandoo ukaweka koplo, ni kupotea,”alisema

BANANGA

Kwa upande wa Bananga akiomba kura, alisema amejipima na ameridhika ana uwezo wa kuongoza jimbo hilo kwani anajua aina ya mbunge ambaye wananchi wa Arusha wanataka.

“Nimejipima binafsi nimeridhika naweza utumishi wa miaka sita ya udiwani, umenipa uzoefu wa kutosha na ninajua aina ya mbunge wana Arusha wanataka, nitumeni nikawe sauti yenu katika vikao vya maamuzi.

“Nimekuwa miongoni mwa madiwani 12 kati ya mliotutuma mwaka 2015 ambapo wengine waliishia njiani na kuhamia CCM, niko imara na kauli inayopaswa kusikilizwa ni yanayotoka mdomoni kwangu.

“Zipo lugha zisizofaa ambazo zimekuwa sehemu ya siasa Arusha, siyo busara kuzijibu kwani wamepita wasiotakia mema chama chetu wakisema nitahama baada ya matokeo yoyote ya leo, katika uchaguzi huu nina matokeo ya kushinda na kujifunza, nimejiandaa kwa kazi niliyoomba hii ni wakati wa mawazo na fikra mpya na kuleta mabadiliko, miaka 10 tupokezane kama nilivyoacha wengine wapokee Sombetini,” alisema.

Kwa upande wao baadhi ya wajumbe wa mkutano huo walimhoji mtia nia huyo, kuhusu ukaribu wake na baadhi ya makada maarufu wa CCM na kuwa wanahofia kuwa anaweza kukihama chama hicho na kuhamia CCM.

Akijibu alisema “marehemu mzee wangu alikuwa kada mtiifu wa CCM na nyumbani kwetu nje kulikuwa na bendera ya Chadema kwa sababu mimi nilikuwa diwani, nimeishi nao nyumba moja, urafiki wangu na mwana CCM haujawahi kuathiri chama changu na hatupaswi kuwa na taifa linalotengana kwa sababu ya itikadi, nimevuka mengi,” alisema.

VITI MAALUM

Akitangaza matokeo ya kuwania nafasi ya Ubunge wa Viti Maalum katika jimbo hilo, aliyekuwa Mbunge wa nafasi hiyo Joyce Mukya aliwashinda wagombea wenzake wanne kwa kupata kura 55 kati ya 90 zilizopigwa.

MWANZA

Kwa wilaya ya Misungwi  Mkoa wa Mwanza, Chadema imepata mgombea Ubunge wa Jimbo la Misungwi aliyepata kura 33 sawa na asilimia 44 ya wapiga kura 75.

Msimamizi wa uchaguzi wa Kanda ya Ziwa, Focas Laurenti, alimtangaza Shija Shibeshi (32) mshindi kwa kupata kura 33 sawa na asilimia 44.

Laurenti alimtaja aliyemfuata Shija kwa karibu kuwa  ni Sundi Nyanda (43) aliyepata kura 31 sawa na asilimia 41 ya kura zote, na Galuma Kushirimwa (48) aliyepata kura 10 sawa na asilimia 13.

Kwa upande wa viti maalum mgombea alikuwa Sundi Nyanda pekee ambaye alipita kura za ndiyo 10, hapana mbili na kura moja ikaharibika.

Wakati huo huo  Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya hiyo waliochukuwa na kurudisha fomu ya kugombea ubunge jimbo  la Misungwi ni 45 wakiwemo wanawake  watano.

Mchuano mkali katika jimbo hilo unatarajiwa kuwa kati ya mbunge aliyemaliza muda wake Charles Kitwanga(57) na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara,  Alexander Mnyeti(30) .

 SERENGETI,JULAI,17,2020

Katika Wilaya ya Serengeti, wanachama 57 kati ya 59 wa CCM waliochukua fomu kuomba kuteuliwa kuwa wabunge wamerejesha fomu zao.

Katibu wa CCM Wilaya ya Serengeti, Naboth Manyonyi, alisema hadi saa 10 jioni juzi kati ya wanachama hao waliorejesha fomu wanawake ni wanne na wanaume 53.

Alisema asilimia kubwa ya watia nia ni vijana na kwamba zoezi la kuchukua na kurejesha limekwenda vizuri na hapakuwa na changamoto yoyote.

Alisema kwa mujibu wa ratiba kikao cha kura za maoni kinatarajia kufanyika Julai 21 ambapo wajumbe wa mkutano huo zaidi 850 na kila mgombea atajieleza mbele ya wajumbe na kura zitahesabiwa kwa uwazi wenyewe wakishuhudia.

Aidha Manyonyi alisema kuwa kwa upande wa viti maalumu na udiwani watia nia wanawake 60  walijitokeza kuchukua fomu na kurejesha ambapo Julai 25 mwaka huu watapigiwa kura na wajumbe.

Kagera

Mkoani Kagera wagombea 460 wa ubunge kupitia CCM, walichukua na kurejesha fomu za kuwania nafasi hiyo katika majimbo tisa ya uchaguzi mkoani humo.

Katibu wa chama hicho mkoani Kagera, Michael Chonyo alisema idadi hiyo inajumuisha wagombea wa viti maalum.

“Kwa upande wa majimbo waliochukua na kurejesha fomu ni 404, viti maalumu kupitia wazazi, vijana na wanawake idadi ya watia nia 56, hiyo inakamilisha watia nia 460,” alisema Chonyo

Alisema Jimbo la Bukoba Mjini waliojiyokeza ni 57, Bukoba Vijijini 42, Muleba Kaskazini 17, Muleba Kusini 52, Biharamulo 51, Ngara 43, Kyerwa 52, Nkenge (Missenyi) 54 Karagwe 36.

Aliongeza kuwa hatua inayofuata ni kufanya vikao vya mapendekezo ambavyo vitajumuisha vikao vya kura za maoni ya jimbo na mabaraza vitakavyofanyika Julai 20 hadi 21.

Kilimanjaro 

Mkoani Kilimanjaro, idadi wanachama wa CCM waliochukua fomu za kuwania ubunge katika majimbo tisa za Mkoa wa Kilimanjaro ni 392 na waliorejesha ni 386.

Kwa upande wa viti maalumu waliochukua ni 105 na waliorejesha ni 102.

Njombe

Mkoani Njombe, Katibu wa CCM Wilaya ya Njombe, Hanafi Msabaha, alisema katika majimbo matatu wanachama 71 walichukua fomu huku 70 zikirejeshwa.

Akizungumza na Mtanzania mara baada ya muda wa kurudisha fomu kukamilika, Msabaha alisema katika fomu 71 zilizochukuliwa mwanachama mmoja hakurejesha.

“Katika fomu zilizochukuliwa katika majimbo matatu, Njombe mjini wanachama walichukua fomu 35 lakini zimerudishwa 34, Makambako walichukua 17 na wamerudisha wote na Lupembe walikua 19 wamerejesha wote”alisema Msabaha.

Akizungumza kwa njia ya simu katibu wa chama cha mapinduzi CCM Wilaya ya Ludewa, alisema wanachama 26 walichukua fomu na 25 pekee ndio waliorudisha.

Kwa upande wa Jimbo la Makete Katibu Amina Imbo, alisema walichukua fomu ni 35 na 34 walirejesha huku Juma Nambaila Katibu wa CCM Wilaya ya Wanging’ombe akisema wanachama 35 wamechukua fomu na kuzirejesha.

HABARI HII IMEANDALIWA NA TWALAD SALUM, MWANZA, MALIMA LUBASHA, SERENGETI, NYEMO MALECELA, KAGERA, ELIZABETH KILINDI, NJOMBE, SAFINA SARWATT, KILIMANJARO NA JANETH MUSHI – ARUSHA

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles