24.3 C
Dar es Salaam
Thursday, April 25, 2024

Contact us: [email protected]

TAKUKURU YAIRARUA POLISI KWA RUSHWA

Na JUDITH NYANGE – MWANZA


takukuruTAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoa wa Mwanza, imelitaka Jeshi la Polisi kufanya kazi kwa kuzingatia sheria, kanuni na maadili ya jeshi hilo kwa kuepukana na vitendo vya rushwa ambavyo viwekuwa  vikisababisha malalamiko mengi kwa wananchi.

Wito huo umetolewa jana na Ofisa Uchunguzi Mwandamizi wa Dawati la Elimu kwa Umma wa Takukuru Mkoa wa Mwanza, Maua Ally, wakati wa kikao kilichowakutanisha maofisa, wakaguzi na askari wa vyeo mbalimbali mkoani hapa.

Alisema jeshi hilo limekuwa likipata sifa mbaya na kulalamikiwa na wananchi kutokana na baadhi ya askari ambao si waadilifu kujihusisha na vitendo vya rushwa na kuwafanya wote kupata sifa mbaya ya kudharauliwa na jamii.

“Tubadilike, kwanini mnajifanya miungu watu kwa kujipa nafasi ambazo si zenu? Nyie mpo kwa ajili ya kuwahudumia wananchi, mnawafanya mnaowahudumia kuona hawawezi kupata huduma yenu bila kutoa kitu chochote.

“Wananchi huko mtaani wanasema kuingia polisi ni bure, lakini kutoka mpaka utoe hela, tunapoteza mapato ya Serikali kwa sababu ya watumishi wachache ambao si waadilifu, wanaochukulia rushwa kama mazoea na utamaduni wao, tubadilike na kuzingatia maadili ya kazi yenu,” alisema Ally.

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi, alisema vitendo vya rushwa vinaaibisha Serikali, ni vyema askari hao wakaanza kwa kujionya wenyewe kabla ya kuchukuliwa hatua za kisheria kwani hata miongozo ya kazi ya jeshi hilo inakataza rushwa.

Kamanda Msangi alisema endapo askari wa jeshi hilo atakamatwa kwa makosa au vitendo vinavyoashiria rushwa, hana nafasi tena, anaweza kufukuzwa kazi na kufikishwa mahakamani.

Aliongeza kuwa Takukuru inapata taarifa nyingi kutoka maeneo mengi ikiwamo hospitali, mahakamani ambako wananchi wanategemea kupata huduma, lakini baadhi ya watumishi wamekuwa vikwazo na kutaka hadi wapate kitu kidogo kwanza ndio wawahudumie.

Alisema jeshi hilo limekuwa likifuatilia ripoti mbalimbali zinatolewa na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO’s) na inawezekana kuna askari wachache wanaofanya  mambo yasiyokubalika  kwa jamii na kulichafua Jeshi la Polisi.

Hata hivyo, Kamanda Msangi amewataka askari wa Jeshi la Polisi kufanya kazi zao na kutimiza wajibu wao kulingana na viapo vyao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles