NA AZIZA MASOUD, DAR ES SALAAM
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), imewaagiza maofisa wake kuanza kufanya manunuzi yao katika soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam ili kuweza kuwabaini wafanyabiashara wanaotumia mashine za kielektroniki, EFDs kufanya udanganyifu.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jana, Naibu Mkurugenzi wa Takukuru, Brigedia Jenerali John Mbungo, alisema wamefuatilia mwenendo wa wafanyabiashara katika soko la Kariakoo na kubaini kuwa baadhi yao wanafanya udanganyifu.
“Baada ya kugundua hayo tumeamua kulivalia njuga na kiukweli tumejipanga vizuri kwa kuwaagiza watendaji wa Takukuru wawe wananunua mahitaji yao pale Kariakoo ili tuwe karibu na wafanyabiashara hao kujua namna ambavyo wanaiibia Serikali.
“Wanavyofanya mwananchi ananunua bidhaa ya shilingi laki mbili au tatu anatengenezewa risiti ya EFDs kuonyesha ametoa shilingi elfu tisini, udanganyifu huu unasababisha Serikali kukosa kodi, sasa vitendo hivi tayari vimeanza kuota mizizi kwa baadhi ya wafanyabiashara na tukiviachia vitaendelea na kutapakaa kwa wengine ambao ni waaminifu,” alisema Brigedia Mbungo.
Alisema vitendo hivyo vya udanganyifu wa namna hiyo ni makosa kwa mujibu wa sheria ya Takukuru kifungu namba 2.
“Najua wachambuzi watasema tumeingia kwenye maduka, kimsingi sisi hatuna mipaka tunaingia popote, makosa haya mtu akipatikana na hatia adhabu yake ni kifungo cha miaka mitano au faini ya Sh milioni 10 au zote kwa pamoja, suala hili ni muhimu na nyeti kwa wafanyabiashara vinginevyo wataingia katika mgogoro na Serikali,” alisema.
Alisema Takukuru imeshafanya utafiti katika soko hilo na tayari imeshajua mapato yanayopotea kwa siku moja, mwezi mpaka mwaka.
Alisema zoezi hilo linafanyika kwa mujibu wa sheria chini ya kifungu cha saba mpaka vifungu vidogo vya E, D na F ambavyo vinawapa mamlaka ya kufuatilia mambo mbalimbali yanayotokea nchini.
Alisema taasisi hiyo ina mamlaka ya kufuatilia mambo yanayotokea kwenye taasisi binafsi pamoja na za umma ili kubaini matukio ya vitendo vya ubadhirifu wa fedha, mali au rushwa.
Mkurugenzi Pride asakwa kwa kusababisha hasara Sh bilioni 1.8
Wakati huo huo Brigedia Jenerali Mbungo, alisema Takukuru inamtafuta aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya mikopo ya Pride, Rashidi Malima, kwa kuhusika na wizi wa Sh bilioni 1.8, fedha ambazo zilikuwa katika taasisi hiyo.
Alisema pia inawashikilia na kuendelea kuwahoji aliyekuwa meneja fedha wa taasisi hiyo, Alfred Kasonka, sambamba na watunza fedha, Abdalla Kitwala na Pascal Sima.
Alisema baada ya kupokea taarifa kutoka kwa wananchi wema kuhusu ubadhirifu katika kampuni hiyo, walianza uchunguzi na katika uchunguzi huo waliwatafuta watu wote waliohusika na matukio ya ubadhirifu na wizi wa fedha ambazo zilikuwa kama mtaji Pride.
Alisema uchunguzi huo ulifanikiwa kuwapata viongozi wanadhimu ama waandamizi wa taasisi hiyo ambao ni pamoja na Rashid Malima ambaye alikuwa Mkurugenzi Mtendaji kuanzia mwaka 1993 mpaka 2018.
“Kwa mujibu wa uchunguzi, ushahidi na taarifa tulizonazo huyu bwana ameweza kuiba kiasi cha Sh bilioni moja nukta nane (Sh bilioni 1.8) na hizi ni taarifa ambazo tumefanikiwa kuzipata na kuzikamata, fedha hii inaweza ikawa zaidi ya hapo, uchunguzi unaendelea tujue kiasi gani amechukua,” alisema Brigedia Jenerali Mbungo.
Alisema Malima alikuwa mtendaji mkuu lakini baada ya kuanza kumfuatilia na kusikia anatafutwa amekimbia kwenda nchini Marekani.
“Hii ndiyo sababu ya kuwaita ili muweze kutufikishia ujumbe huu kama mlivyofanya kwa wengine, taarifa tulizonazo amekimbilia Marekani, ni mtu wa miaka sitini na tano, ni mtu mzima huyu lakini mmeona jinsi uhalifu unavyoweza kumsumbua mtu amekimbia nchi yake amekwenda Marekani na sisi bado tunaendelea kumtafuta ili aje aweze kujibu tuhuma zake,” alisema Brigedia Jenerali Mbungo.
Alisema kupitia vyombo vya habari wananchi wanapaswa kutoa taarifa endapo watamwona nchini.
“Tunaomba mwananchi aliye na taarifa kamili atupe maana anaweza akawa yupo nchini hapa watupe taarifa, tunawaomba Watanzania waliopo Marekani wakimwona bwana huyu mwambieni anatafutwa arudi nyumbani.
“Mtu tunapomtafuta kwa utaratibu huu tunakuwa tumeshabaini kuwa huyu mtu ametoroka na sisi kwa njia zetu za ndani humu tumeshindwa kumpata, watu watoe taarifa hata kwakupiga simu ya bure,” alisema Brigedia Jenerali Mbungo.
Alisema mbali na Malima, Takukuru inawashikilia na kuwahoji watumishi wengine watatu wakiwemo Alfred Kasonka, aliyekuwa Meneja wa Fedha, Abdalla Kitwala na Pascal Sima, aliyekuwa mtunza fedha.
“Hawa tunaendelea nao kwa mahojiano na walikuwa wakitoa ushirikiano ambao kiuchunguzi utatusaidia kuweza kusimamisha makosa hayo na tunataka taarifa hii imfikie bwana aliyekimbia nchi aweze kurudi na kuweka rekodi nzuri na Serikali,” alisema Brigedia Jenerali Mbungo.
Akizungumzia kuhusu wakurugenzi wa bodi kuhusishwa na sakata hilo, Brigedia Jenerali Mbungo, alisema wapo baadhi ya wajumbe hao wanaweza wakawa sehemu ya ushahidi kulingana na ushiriki wao.
“Uchunguzi wa bodi ni sehemu ya ushahidi, katika bodi hizi wajumbe wapo wa namna mbili, wapo ambao wanashiriki katika utendaji na wasiokuwa watendaji sehemu kubwa ya pride wajumbe wake si watendaji wanahudhuria tu vikao, hao nao tunaendelea kuwahoji,” alisema Brigedia Jenerali Mbungo.
Alisema Takukuru inazingatia misingi ya dhati na sheria hivyo haipo kwa ajili ya kumwonea mtu na mara zote wanapowaita waandishi wa habari kwa ajili ya kutoa taarifa wanakuwa wameshajiridhisha na uchunguzi wao.
Mkufunzi Duce atoroka na karo za wanafunzi
Katika hatua nyingine Mhasibu wa Chuo cha Ualimu Dar es Salaam (Duce), Josephat Machiwa, anatafutwa na taasisi hiyo kwakukimbia na fedha ambazo zilipaswa zitolewe na wanafunzi kama ada ambazo kiwango chake hakijatajwa.
“Hizi fedha zilikuwa ni za ada, ni kiasi kikubwa cha fedha na kila baada ya muda hii fedha inabadilika kwa hiyo nitashindwa kutaja ni kiasi gani cha fedha kwa sababu kadiri uchunguzi unavyoendelea zinabadilika, Bwana Jospehat popote ulipo jitokeze ripoti kituo cha polisi au cha Takukuru uje uweke rekodi zako vizuri na vyombo vya sheria,” alisema Brigedia Jenerali Mbungo.