27.2 C
Dar es Salaam
Monday, March 20, 2023

Contact us: [email protected]

CAG wa zamani aeleza alivyoumiza mawaziri

Na FREDRICK KATULANDA – DODOMAMDHIBITI na Mkaguzi Mkuu Mstaafu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, amesema wakati akiwa madarakani aliumiza watu wengi wakiwamo mawaziri lakini alikuwa akitumia sheria.

Utouh alisema hayo jana jijini Dodoma wakati wa kujadili mada ya uongozi kwenye mdahalo uliofanyika katika kuadhimisha wiki ya Asasi za Kiraia mwaka 2018.

Alisema akiwa CAG kwa nafasi yake aliwaumiza wengi wakiwemo mawaziri, lakini kwa kuwa alitenda kwa haki na kuzingatia sheria, leo anaishi na jamii bila hofu.

Alisema wapo viongozi ambao wakitoka madarakani hujawa hofu kuishi na jamii kwa hofu ya kutendewa mabaya na waliowaumiza.

“Nikiwa CAG najua niliumiza watu, lakini nilikuwa nikitimiza wajibu wangu kwa hekima na kuzingatia sheria, leo naishi vyema na jamii mtaani… sasa ukiwa kiongozi ukapendelea familia yako na kuumiza wengine utapata shida,” alisema.

Aliwashauri viongozi na watendaji mbalimbali kutambua ipo siku hawatakuwa madarakani hivyo ni vyema wakazingatia kanuni na sheria wakati wa uongozi wao.

Alisema kila kiongozi anapaswa kutambua kwamba ipo siku atatoka kwenye nafasi yake na kuwaachia wengine, hivyo lazima ashirikiane na anaowaongoza na kuepuka kuwaumiza walio chini.

Utouh alisema ni lazima viongozi wawe na uwezo wa kuchuja taarifa na mashtaka wanayopelekewa dhidi ya watumishi wanaowaongoza.

Alisema tatizo lingine la viongozi ni kutenda mambo kwa mazoea, hivyo aliwashauri wanapoteuliwa au kuchaguliwa, wahakikishe wanatenda mambo yatakayokumbukwa.

Walioumia wakati wa Utouh

Baadhi ya viongozi walioumia wakati wa Utouh, ni pamoja na wale waliofukuzwa kazi baada ya CAG kuchunguza sakata la Akaunti ya Tegeta Escrow na kubainisha kwamba zaidi ya Sh bilioni 300 zilizotolewa kwenye akaunti hiyo, zilikuwa za umma.

Ripoti hiyo ya CAG, ilifanya bunge lililokuwa chini ya Spika Anne Makinda, kufanya kazi mpaka usiku wa manane na baadaye kuazimia kuwa wote waliotajwa wachukuliwe hatua.

Mawaziri waliotajwa kwenye sakata hilo ni Profesa Anna Tibaijuka, ambaye alikuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na ambaye aliingiziwa Sh bilioni 1.6 na mwanahisa wa zamani wa Kampuni ya IPTL, James Rugemarila. Tibaijuka alivuliwa wadhifa huo kutokana na sakata hilo.

Wengine ni aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, ambaye Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete, alisema amemweka kiporo baada ya Bunge kumwona kuwa hakushughulikia vizuri suala hilo na kuisababishia Serikali kukosa mapato.

Wengine ni aliyekuwa mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti na ambaye alikuwa Mwanasheria Mkuu, Andrew Chenge, ambaye aliingiziwa pia Sh bilioni 1.6 kwenye akaunti yake na Rugemarila; waziri wa zamani wa Nishati na Madini, William Ngeleja, aliyeingiziwa Sh milioni 40.4, aliyewahi kuwa Waziri wa Nishati na Madini, Daniel Yona (Sh milioni 40.4), Mbunge wa zamani wa Sumbawanga (CCM), Paul Kimiti (Sh milioni 40.4) na aliyekuwa mjumbe wa Bodi ya Tanesco, Dk. Enos Bukuku (Sh milioni 161.7).

Vigogo waliotajwa kwenye sakata hilo ni Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliackim Maswi, ambaye alisimamishwa, Fredrick Werema, ambaye alijiuzulu kwa maelezo kuwa ushauri wake kuhusu suala la kodi kwenye fedha hizo haukueleweka na ulisababisha tafrani.

Makinda

Katika mdahalo wa jana, Makinda pia alizungumza na kusema sifa kubwa ya kiongozi ni kutambua wajibu wake na kupokea ushauri na kikubwa kuwa mwaminifu.

Alisema uongozi si ulaji na kubainisha amekuwa akisikitishwa na vyombo vya habari pale wanapoandika juu ya teuzi mbalimbali kuweka vichwa vya habari vinavyosema ‘fulani kaula’.

“Ukiteuliwa unaenda kuwatumikia watu, viongozi tambueni ukiamini umeula basi utaenda kuwa fisadi,” alisema.

Akizungumzia wanawake na nafasi zao katika uongozi, alisema ni waziri lakini aliwaonya kuepuka kujinyanyapaa kwa kudhania wao hawajui mambo mengi hivyo hawawezi kuongoza jambo alilosema si kweli.

“Mkiteuliwa usianze kusema mwenyewe mimi mwanamke hili siwezi, mbona hata hao wanaume nao kuna mambo hawayawezi,” alihoji.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
210,784FollowersFollow
563,000SubscribersSubscribe

Latest Articles