23.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

TAKUKURU KUWAHOJI VIONGOZI SIMBA SC

Na JESSCA NANGAWE


TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Tanzania (Takukuru), imesema itaendelea na uchunguzi kwa viongozi wa Simba mbapo wakati wowote wataitwa kuhojiwa.

Kauli ya Takukuru inakuja baada ya kuwapo utata wa usajili wa beki anayekipiga kwenye kikosi cha Lipuli FC ya Iringa raia wa Ghana, Asante Kwasi, kudaiwa kusaini Simba ambapo mchakato huo unaelezwa kwamba, una mianya ya rushwa.

Akizungumza na MTANZANIA, Mkuu wa Kitendo cha Habari na Mawasiliano wa Taasisi hiyo, Mussa Misalaba, alisema hakuweza kupata mawasiliano yoyote kutoka kwa uongozi wa klabu ya Lipuli kutokana na simu zao kutopokelewa, lakini bado wanaendelea na uchunguzi wao.

“Viongozi wa Lipuli simu zao zilikuwa zinaita tu bila majibu, bado tunawafuatilia na kuwahoji, simu niliyokuwa natumia ilizima, lakini naendelea kuwafuatilia na kujua kitakachofuata,” alisema Misalaba.

Alisema  kuwa, kutokana na suala hili kuwa la kichunguzi zaidi, hawawezi kuweka wazi ni lini hasa watawaita na kuwahoji wahusika hadi hapo watakapomaliza na kisha kuweka wazi kinachoendelea.

“Ni suala la kiuchunguzi zaidi, kisheria hapa mtuhumiwa anahitaji kulindwa, tukianza kuweka wazi nini tunafuatilia, tunaweza tusipate ushirikiano, tutahoji pande zote mbili, wakiwamo viongozi wa Simba pia, kisha tutaweka wazi,” alisema Misalaba.

Licha ya Misalaba kueleza hayo, lakini alikataa kutaja majina ya viongozi hao na sababu hasa za kuhojiwa, kwa sababu ya hofu ya kuvuruga uchunguzi wao ambao wameuanzisha na wanaendeleo nao, ingawa uchunguzi wa Mtanzania umeonyesha kwamba, ni usajili wa Kwasi.

Wiki iliyopita, baadhi ya viongozi wa Lipuli waliitwa na kuhojiwa kwa saa kadhaa na Takukuru Mkoa wa Iringa kisha kuachiwa.

Beki huyo wa kati aliingia mkataba wa miaka miwili na Simba ukiwa na utata, huku akiwa bado ni mchezaji halali wa Lipuli FC, ambapo amebakisha miezi nane kabla ya mkataba na timu hiyo kongwe ya Iringa kumalizika.

Kwasi ameshindwa kuitumikia klabu ya Simba baada ya kuwapo pingamizi kutoka kwa uongozi wa timu ya Lipuli ambayo ilimsajili akiwa mchezaji huru kutoka Mbao FC ya jijini Mwanza.

MTANZANIA lilibaini kuwa, kuna mkataba unamwonyesha Kwasi kama mchezaji wa Gordogordo ya Ghana na kwamba klabu hiyo ilimtoa kwa mkopo kwenda Lipuli baada ya awali kufanya hivyo kwa Mbao FC ya mkoani Mwanza, ingawa alipewa mkataba kama mchezaji huru.

Jana MTANZANIA lilimtafuta Mwenyekiti wa Lipuli FC, Ramadhani Mihano, alisema uongozi wa timu hiyo umemwandika barua mchezaji huyo pamoja na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) inayoeleza utoro wake kambini.

“Leo (jana) mchana tumemwandikia barua mchezaji huyo kwa kumtumia kwa njia ya simu `Whatsapp` na TFF kwa njia ya barua pepe kwa kueleza mchezaji huyo ametoroka na anahitaji kurejea mara mmoja kambini kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa FA,” alisema.

Mihano alisema wanatambua kwamba beki huyo ni mchezaji wao halali kutokana na kuingia na mkataba wa mwaka mmoja akitokea Mbao FC baada ya kumaliza mkataba.

“Kwasi amekuja kwetu kama mchezaji huru, baada ya kujiridhisha na barua aliyokuja nayo ambayo tumeambatanisha katika mkataba wetu uliopo Takukuru baada ya juzi kuhitaji kuona mkataba huo tulipokwenda kuhojiwa.

“Ijumaa iliyopita tuliitwa kweli Takukuru, ambapo walihitaji kuona baadhi ya nyaraka muhimu, ikiwamo mkataba baina yetu na mchezaji na wameendelea kushikilia, kwani bado kuna uchunguzi wanaendelea nao,” alisema Mihano.

Alisema Kwasi amesaini mkataba Simba bila ya kufuata kanuni na Sheria, kutokana na hakuna kiongozi yeyote wa timu hiyo aliyefanya mazungumzo au kupokea barua kutoka kwa wekundu hao wa Msimbazi ikihitaji huduma ya mchezaji huyo.

“Kwa hapa nchini viongozi waliotufuata ni Singida United, wao walikuja wakihitaji kutoa milioni 10, tulipoangalia uwezo wa mchezaji huyo na kiwango chake tumeona ndogo na kuamua kuachana nazo na kuendelea kutumikia Lipuli.

“Gari hakuna sehemu ambayo Singida walisema watatoa gari ndogo aina ya basi na kiasi cha fedha kama inavyodaiwa, nina imani Kwasi angekwenda kuchezea katika kikosi cha timu hiyo,” alisema Mihano.

Kwa upande wa mchezaji huyo, alisema huenda akaondoka nchini na kwenda kwao Ghana kwa ajili ya mapumziko, kisha atarejea Tanzania kwa ajili ya kuendelea na kazi.

“Kuondoka, umesikia wapi! Hizi taarifa ni kweli ila kwa sasa nipo hotelini napumzika, nitaondoka mara mmoja nchini na nitakaa muda mfupi nitarejea,” alisema Kwasi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles