23.2 C
Dar es Salaam
Saturday, July 27, 2024

Contact us: [email protected]

KIMBISA ABWAGWA USPIKA EALA

Na ABRAHAM GWANDU-ARUSHA


HATIMAYE Bunge la Afrika Mashariki (EALA), limemchagua Martine Ngoga kutoka Rwanda kuwa Spika wake na kuwabwaga wapinzani wake Adam Kimbisa kutoka Tanzania na Leontine Nzeymana wa Burundi.

Hatua hiyo sasa inahitimisha malumbano yaliyodumu kwa muda wa siku mbili, kuhusu uhalali wa nani anapaswa kuwa Spika kwa mujibu wa kanuni zinazounda Bunge hilo.

Uchaguzi huo uliofanyika jana mjini hapa, awali ulitawaliwa na malumbano makali huku baadhi ya wabunge wakitaka kuahirishwa kwa mkutano huo kutokana na kutotimia kwa akidi kwa mujibu wa utaratibu.

Kabla ya kuanza kwa uchaguzi huo, baadhi ya wabunge walitaka ufafanuzi wa kina wa kwanini Tanzania na Burundi zimeweka wagombea hali ya kuwa si zamu yao kuongoza chombo hicho.

Katika mkutano huo wa jana, wabunge wa Burundi hawakuhudhuria, huku Tanzania waliohudhuria walikuwa wabunge wawili ambao ni Dk. Ngwaru Maghembe na Dk. Abdulah Makame.

Aliyekuwa wa kwanza kuhoji uhalali wa kikao hicho kutokana na kutotimia kwa akidi, alikuwa ni mbunge Dk. Ngwaru, ambaye alishauri kuahirishwa kwa kikao hicho.

“Ndugu Katibu kutokana na makubaliano miongoni mwa nchi wanachama, kila jambo litafikiwa kutokana na makubaliano na kuzingatia akidi, lakini humu ndani sisi Tanzania tuko wawili na Burundi hawapo kabisa, hatuwezi kufanya chochote kwa mujibu wa sura ya sita ya hati ya makubaliano,” alisema Dk. Ngwaru.

Hoja hiyo ya Dk. Ngwaru iliibua malumbano makali, huku Mbunge kutoka Uganda, Suzani Nakawuki alitumia lugha kali na kudai kwamba wabunge kutoka Tanzania na Burundi wako Arusha kwa ajili ya kula chakula cha bure na posho zinazotokana na kodi za wananchi.

“Hapa tusilete ubabaishaji, kila nchi ilichagua wabunge kuja hapa kuwakilisha nchi zetu. Mleta hoja anasema hawapo wakati tangu jana tunawaona wakifurahia chakula cha bure na nina hakika wamechukua posho. Mimi naomba tufuate utaratibu, hiki ni chombo huru kisiingiliwe na yeyote,” alisema Nakawuki.

Baada ya hoja hiyo, Katibu wa Bunge hilo, Keneth Madete, aliwahesabu wajumbe waliokuwapo ukumbini na kufikia 36 na kuruhusu kuendelea na utaratibu wa uchaguzi wa Spika wa Bunge na kumwita mgombea  Ngoga wa Rwanda ili aweze kujieleza kwa wabunge na kuomba kura.

Alipomaliza aliwaita wagombea Adam Kimbisa (Tanzania) na Leontine Nzeymana (Burundi) ili nao waombe kura, lakini hawakuwapo ukumbini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles