27.1 C
Dar es Salaam
Thursday, January 2, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

Takukuru kumuhoji tena Seth wa IPTL

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), imeiomba Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kumchukua mshtakiwa Harbinder Singh Seth,  akakamilishe  kuchukuliwa maelezo yake.

Ombi hilo lilitolewa jana mahakamani hapo na Wakili wa Takukuru, Leonard Swai mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi wakati kesi hiyo ilipotajwa.

Swai alidai  upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na kuwa wachunguzi wa Takukuru wataenda kumchukua Seth gerezani.

Naye Wakili wa Utetezi, Dorah Mallaba, alisema Seth ameomba wakati akichukuliwa maelezo wakili wake awepo.

Mawakili hao wa utetezi, Mallaba na Paschal Kamala walisisitiza upande wa mashtaka kukamilisha upelelezi wa kesi hiyo mapema na kwa wakati.

Baada ya kusikiliza hoja zote Hakimu Shaidi aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 8, mwaka huu kwa ajili ya kutajwa  kuangalia kama upelelezi utakuwa umekamilika au  la.

Seth na mshtakiwa mwenzake,  James Rugemarila, wanakabiliwa na mashtaka 12 ya  uhujumu uchumi.

Wanadaiwa  kula njama, kujihusisha na mtandao wa uhalifu, kughushi, kutoa nyaraka za kughushi, kujipatia fedha kwa njia za udanganyifu,  kutakatisha fedha na kuisababisha Serikali hasara ya USD 22,198,544.60 na Sh 309,461,300,158.27.

Mashtaka ya utakatishaji fedha   kwa mujibu wa sheria hayana dhamana.

 

Mbowe na wenzake

Wakati huohuo, kesi inayowakabili viongozi tisa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu itaanza kusikilizwa Novemba Mosi mwaka huu kwa washtakiwa hao kusomewa maelezo ya awali.

Kesi hiyo ya jinai namba 112 ya mwaka huu, inawakabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman  Mbowe, Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu na Naibu katibu Mkuu Bara na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika na Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche.

Wengine ni Mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Bunda, Esther Bulaya, Mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko, Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Vincent Mashinji na Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa.

 

Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi, alidai

mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri, kuwa kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya washtakiwa hao kusomewa maelezo ya awali, lakini wakili anayemtetea Mchungaji Msigwa, Jamuhuri Johnson, aliiomba mahakama iahirishwe.

Wakili huyo aliwasilisha ombi hilo ili apate nafasi ya kupitia jalada la kesi hiyo aweze kujua nini kimekwisha kutokea ndani ya kesi hiyo aweze kumwakilisha mteja wake vizuri.

Wakili huyo wa Msigwa alijitambulisha mahakamani hapo jana baada ya aliyekuwa akimtetea awali, Jeremiah Mtobesya kujitoa Agosti 23, mwaka huu. Washtakiwa wengine wanatetewa na Wakili Peter Kibatala.

Hata hivyo Wakili Nchimbi alipinga ombi hilo na kudai kuwa kwa kuangalia mwenendo wa kesi hiyo ni wazi katika kesi ya msingi hakuna hatua yoyote iliyopigwa zaidi ya washtakiwa kusomewa mashtaka yanayowakabili.

“Katika kuwasomea washtakiwa maelezo ya awali wahusika wakuu ni washtakiwa ambao wakisomewa ndiyo wana wajibu wa kujibu kipi wanakubali na kipi hawakikubali. Hivyo naiomba mahakama kutupilia mbali ombi la utetezi,” alidai Wakili Nchimbi.

Hata hivyo Wakili wa Msigwa, aliendelea kudai kuwa mteja wake si mwanasheria kuna maelezo ambayo amempatia hayaelewi vizuri ndiyo sababu aliomba kupitia jalada.

Baada ya kusikiliza hoja zote, Hakimu Mashauri aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba Mosi, mwaka huu kutoa nafasi kwa wakili huyo kupitia jalada na  washtakiwa hao watasomewa maelezo ya awali siku hiyo.

Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka 13, ikiwamo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji wa kosa la jinai kati ya Februari 1 na 16, 2018, Dar es Salaam.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles