25.2 C
Dar es Salaam
Monday, March 27, 2023

Contact us: [email protected]

Dawa za kulevya zatikisa Shirika la Posta nchini

ANDREW MSECHU na LOVENESS BERNARD – dar es salaam

MKUU wa Kitengo cha Usalama wa Shirika la Posta nchini, George Mwamgabe ambaye hivi karibuni mwajiri wake alitangaza kwenye magazeti kuwa anatafutwa, amedaiwa kumtegea dawa za kulevya Postamasta Mkuu, Hassan Mwang’ombe.

Taarifa ya Posta iliyotolewa kwenye magazeti ilisema; “kutokana na kutoonekana kazini na nyumbani kwako, baada ya jitihada za kukutafuta kushindikana kwa kipindi cha zaidi ya wiki moja, tunakufahamisha popote ulipo uhudhurie kikao cha nidhamu kitakachofanyika Jumanne Novemba mosi saa nne asubuhi kwenye ukumbi wa mkutano ghorofa ya 12 Posta makao makuu kujibu tuhuma za kinidhamu zinazokukabili.

“Aidha shirika litaendelea na kikao hicho cha nidhamu kama utashindwa kuhudhuria bila taarifa kwa mwajiri wako.”

Wakati taarifa hiyo ikiendelea kusambaa, chanzo cha kuaminika ndani ya Shirika la Posta kiliileza MTANZANIA kuwa Mwamgabe alitoweka baada ya kudaiwa kumtegeshea Mwang’ombe dawa za kulevya ambazo ni heroin gram 1.5 na bangi gramu 100.

Taarifa hizo zilidai kuwa sakata hilo lilitokana na kifurushi kilichotumwa kutoka Morogoro kwenda kwa Mwang’ombe ambaye ni Postamasta Mkuu.

Chanzo hicho kilieleza kuwa dereva aliyekuja na mzigo huo, baada ya kufika kwenye ofisi za Posta alishusha mizigo mingine, lakini alikawia kushusha kifurushi hicho.

“Alipoulizwa sababu za kutokishusha, alidai mtu aliyeelekezwa amkabidhi hamuoni eneo hilo.

“Mizigo hiyo ilifika hapa asubuhi ikitokea Morogoro, kwanza ilianza kucheleweshwa kushushwa kwenye gari, baadaye ilishushwa na kupitishwa kwenye mashine ya ukaguzi na kupelekwa stoo.

“Baadaye majira ya mchana mkuu wa kitengo cha usalama alikuja na kuingia stoo, kisha alipotoka akaagiza mizigo hiyo ikaguliwe upya,” kilisema chanzo hicho.

Kilieleza kuwa mkuu huyo wa ulinzi alisema amepigiwa simu na wasaidizi wake wawili kuwa wana mashaka na mizigo hiyo, hivyo na yeye alimpigia simu mkaguzi wa mizigo ambaye alikuwa msikitini na kumtaka arejee ofisini na kufanya upya ukaguzi.

Baada ya mkaguzi huyo kurejea, ilielezwa kuwa alikuta mizigo hiyo imefungwa tofauti na ilivyokuwa awali.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa chanzo hicho, mkuu huyo wa usalama alisimamia ukaguzi wa mara ya pili na kusema kuwa wamebaini kulikuwa na dawa za kulevya.

Taarifa hizo zilisema kuwa Mwamgabe aliwaita polisi na walichukua mizigo hiyo kisha kuipeleka katika kikosi cha utambuzi cha mbwa ambako walithibitisha kulikuwa na dawa hizo za kulevya na baada ya siku tatu ilirejeshwa Posta, kisha kutoa taarifa kwa Mamlaka ya Kuzuia na Kudhibiti Dawa za Kulevya.

Chanzo hicho kilieleza kuwa tukio hilo lilitokea Septemba 25 na polisi walichukua mizigo hiyo na waliirudisha Septemba 28 na jukumu hilo kukabidhiwa kwa Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya.

 

MKANGANYINGIKO

Kwa mujibu wa mtoa taarifa, upimaji mizigo kwa mara ya pili uliibua mkanganyiko kwa kuwa awali ilivyopimwa kulikuwa na mifuko miwili yenye mchele kilo 25 kila mmoja.

“Mara ya pili baada ya kupimwa kutokana na agizo la mkuu wa usalama, kila mfuko ulikuwa na kilo 20 jambo lililozua utata zaidi,” kilisma chanzo chetu.

Pia inadaiwa kabla ya kuamuru mizigo hiyo kukaguliwa mara ya pili, kamera za usalama za chumba cha kuhifadhia mizigo zilichezewa, kwamba kamera moja ilibadilishwa uelekeo na nyingine ilifutwa baadhi ya matukio.

Inadaiwa mtu aliyekuwa ameingia katika chumba hicho ni Mwamgabe na baada ya kutoka ndipo akaagiza mizigo hiyo ipimwe upya.

Chanzo kingine kilieleza gazeti hili kuwa katika kufuatiliwa ukweli wa suala hilo, mtu wa Posta kutoka Morogoro ambako mzigo ulitumiwa alihojiwa na vyombo vya dola na kuthibitisha kuwa mzigo alioutuma Dar es Salaam ulikuwa ni mifuko miwili yenye kilo 25 za mchele kila mmoja na siyo kilo 20.

Pia inadaiwa kuwa vijana wawili waliohusika kupima mizigo hiyo walipohojiwa walisema siyo kweli kwamba walikuwa wamemweleza mkuu wa usalama kwamba wana wasiwasi na mizigo hiyo kama ambavyo bosi wake huyo alikuwa amedai awali.

Chanzo kilieleza pia kuwa Postamasta Mkuu ilibidi afanyiwe vipimo mbalimbali ili kuthibitisha kama anatumia dawa za kulevya ama laa, na ikathibitika kwamba hatumii dawa hizo.

“Unajua kiasi cha dawa kilichokutwa kwenye hiyo mizigo ni cha matumizi ya mtu tu ambaye hutumia dawa za kulevya, kwahiyo ilibidi bosi apimwe mkojo lakini akabainika yupo salama,” kilieleza chanzo hicho.

Alipoulizwa na MTANZANIA kuhusu taarifa hizo, Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kuzuia na Kudhibiti Dawa za Kulevya, Rogers Sianga, alikiri kuzipokea na kusema kwamba mamlaka yake inaendelea na uchunguzi.

“Ni kweli tumepata taarifa hizo na tunaendelea na uchunguzi, japokuwa taarifa nyingi zina utata na inaonekana kuna mambo yanayoendelea ndani yakihusishwa na mgogoro wa kiuongozi,” alisema.

Msaidizi wa Postamasta Mkuu, Abubakar Athuman, alipoulizwa juu ya dawa hizo kutegewa bosi wake, alisema suala hilo ni binafsi sana na inatakiwa alizungumzie Postamasta Mkuu ambaye kwa sasa yupo nchini Uswisi kikazi.

Alipoulizwa juu ya Mwamgabe kutoonekana ofisini, alisema Postamasta Mkuu ndiye anayepaswa kuzungumzia suala hilo.

Msemaji wa Polisi, Barnabas Mwakalukwa, alisema hajapata taarifa kuhusu tukio hilo na kuelekeza kuwa huenda taarifa hizo ziko kwa watendaji wa chini na kuomba apewe muda kufuatilia.

 

NJIA ZA KUINGIZA DAWA ZA KULEVYA

Katika hatua nyingine, jana Kamishna Sianga alisema wamedhibiti uingizaji wa dawa za kulevya nchini na hali kwa sasa si kama ilivyokuwa siku za nyuma.

Alisema kwa sasa wamebaini kuwa baada ya ulinzi kuimarishwa katika viwanja vya ndege na ukanda wa bahari ya Tanzania, wasafirishaji wa dawa hizi wameanza kutumia pwani ya Msumbiji kisha kusafirisha kwa njia za panya kuingia nchini kwa kutumia magari na pikipiki.

Sianga alisema tofauti na ilivyokuwa siku za nyuma ambapo wasafirishaji walikuwa wakitumia zaidi watu waliokuwa wakimeza dawa hizo kuanzia nusu kilo hadi kilo mbili, kwa sasa wasafirishaji wanatumia njia ya kuficha dawa hizo katika mabegi na mizigo na kusafirisha kwa njia ya ndege na majahazi.

“Lakini zaidi tumebaini kwamba wasafirishaji wamekuwa wakichukua vijana hapa na kuwapa mafunzo, kisha kuwapeleka Afrika Kusini, Angola na Msumbiji ambako huwabebesha mizigo na kuondokea huko.

“Lakini pia tumebaini wanatumia wazee wa hadi miaka 80 na watu wa nje kusafirisha… kuna babu mmoja wa miaka 80 alikamatwa akiwa na dawa za kulevya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere,” alisema.

Alisema tangu kuanza kwa ushirikiano baina ya Mamlama yake na vyombo vya ulinzi vya kimataifa ikiwemo Indian Ocean Forum on Maritime Crimes mwaka 2010 na baadaye Combined Maritime Forces/ CTF 150 vinavyohusisha muungano wa majeshi ya nchi mbalimbali katika bahari ya Hindi vilivyoanzishwa kudhibiti uharamia, imesaidia ukaguzi wa meli na kupungua kasi ya usafirishaji wa dawa za kulevya katika pwani ya bahari hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,213FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles