24.4 C
Dar es Salaam
Thursday, October 31, 2024

Contact us: [email protected]

Taifa Stars yaitesa Algeria

Pg 32ABDUCADO EMMANUEL NA THERESIA GASPER

WAKATI timu ya Taifa ya Tanzania ikitarajia kurudiana na Algeria ‘The Desert Foxes’ kwenye Uwanja wa Mustapha Tchaker jijini Blida leo saa 3:15 usiku, Taifa Stars imeonekana kuwatesa wapinzani hao kuelekea mchezo huo wa raundi ya pili kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2018 nchini Urusi.

Kiwango kikubwa walichokionyesha Stars kwenye mchezo wa kwanza uliomalizika kwa sare ya mabao 2-2, bado kimezidi kuwavuruga Algeria ambao hadi sasa hawaamini kama wangekutana na upinzani mkubwa kwenye Taifa dogo la Tanzania.

Hivi sasa hofu kubwa imetanda nchini humo juu ya hatima ya Algeria kusonga mbele kwenye hatua ya mwisho ya makundi, ambapo wamedai ni aibu kubwa kwao kama watatolewa na Tanzania ambayo inashika nafasi ya 135 duniani, huku wao wakiwa ya 26.

Magazeti na vyombo mbalimbali vya habari nchini humo jana vimeripoti kuwa kwa sasa benchi la ufundi la timu hiyo chini ya Mfaransa Christian Gourcuff, linatafuta namna ya kuwadhibiti Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu, waliowasumbua katika mchezo wa kwanza.

“Lazima tufanye kazi ya ziada kwenye mchezo wa kesho (leo) hasa kuzuia makali katika eneo lao la ushambuliaji linaloonekana kuwa ni hatari zaidi, wakiwatumia Samatta (Mbwana) na Ulimwengu (Thomas),” alisema Goucuff kupitia gazeti la Le Jour d’Algerie.

Mfaransa huyo aliongeza kuwa jambo kubwa walilopanga kufanya ni kuumaliza mchezo huo ndani ya kipindi cha kwanza kwa kumiliki mipira na kushambulia kwa kasi ili kuipa presha zaidi Stars.

Gazeti jingine la El Khabar, liliibua madai mengine kuwa Rais wa Shirikisho la Soka Algeria, Mohamed Raouraoua, hajaridhishwa na kiwango walichokionyesha Mbweha hao jijini Dar es Salaam.

Raouraoua pia amelalamikia namna kocha Gourcuff alivyopanga kikosi hicho kwa kuwaweka baadhi ya wachezaji muhimu nje, huku ikidaiwa kuwa hana uhusiano mzuri na Mfaransa huyo ambaye amepanga kuachia ngazi mara baada ya mchezo huo.

Wakati hali ya Algeria ikiwa hivyo, Kocha wa Stars, Charles Mkwasa, kabla ya kuelekea nchini humo juzi, alisema kuwa watakwenda kucheza mchezo huo kwa staili waliyocheza nyumbani kwa kushambulia huku pia wakijilinda.

“Tuna matarajio mazuri kuelekea mchezo wa ugenini, naamini wachezaji wangu watacheza mchezo mzuri kama walivyocheza hapa leo (juzi), naamini Mungu akipenda tutapata matokeo mazuri ugenini, tumewaona wanavyocheza, hawatishi sana,” alisema.

Kerr, Shime, Mwaisabula watoa neno

Kocha Mkuu wa Simba Mwingereza, Dylan Kerr, amesema Stars imepoteza historia ya kuifunga Algeria kutokana na kukosa nafasi nyingi walizotengeneza, kwani Samatta alipata nafasi lakini akashindwa kuzitumia.

 

Aliongeza kuwa Watanzania hawapaswi kumlaumu kocha kwa upangaji wa kikosi chake katika mechi iliyopita, kwani makosa yalifanywa na wachezaji wenyewe ambao watahitaji akili ya ziada kushinda mechi ya marudiano ugenini.

 

Kwa upande wake, mmoja wa makocha vijana nchini, Bakari Shime, anayeifundisha timu ya Mgambo JKT, amesema kitaalamu mechi hiyo ni rahisi kiufundi kwa kuwa tayari benchi la ufundi limeona ubora na udhaifu wa wapinzani wao tofauti na awali.

“Lakini pia kocha ameona ubora na upungufu wa timu yetu na ameona wapi mipango yake ilikwama. Stars ilitengeneza nafasi nyingi za kufunga kwenye mchezo wa awali, naamini zilitokana na mipango ya kocha wetu, hivyo hata mchezo ujao zitatengenezwa nyingine,” alisema.

Naye Kocha mkongwe nchini, Kennedy Mwaisabula, alisema Tanzania ina mlima mrefu kwenye mchezo huo, hasa kutokana na matokeo mabaya waliyopata na kupoteza nafasi nyingi za kufunga nyumbani.

“Waarabu huwa ni wazuri kwenye mechi za nyumbani kwao, Stars inatakiwa kutumia ipasavyo nafasi watakazopata tofauti na awali, namna Algeria walivyocheza kwa kasi dakika 25 za mwisho, ndio staili ile watacheza wakiwa nyumbani kwao, jamaa wanajua kutafuta ushindi kwa namna yoyote ugenini,” alisema.

Taifa Stars ili iitoe Algeria, inatakiwa kupata ushindi wowote au sare ya kuanzia mabao matatu na mshindi wa jumla atafuzu kwa hatua ya makundi itakayohusisha timu 20 na bingwa wa kila kundi atafuzu kwa fainali za michuano hiyo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles