NA JENNIFER ULLEMBO, DAR ES SALAAM
JINA la mshambuliaji wa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ anayecheza soka la kulipwa katika klabu ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mbwana Samatta, limegeuka gumzo na kivutio nchini Algeria na kuwapaisha Watanzania wanaoishi huko.
Samatta, ambaye ni miongoni mwa wachezaji wanaounda kikosi cha Stars kitakachoshuka dimbani leo kuikabili Algeria ‘The Desert Foxes’ katika mchezo wa marudiano wa kufuzu Fainali za Kombe la Dunia 2018 nchini Urusi, ameendelea kujikusanyia sifa kutokana na kiwango chake.
Katika mchezo wa awali uliofanyika Uwanja wa Taifa juzi, timu hizo zilitoka sare ya mabao 2-2, huku Samatta akifunga bao la pili katika dakika ya 44 na Elias Maguli akipiga la kwanza huku Islam Slimani, akiipatia Algeria mabao mawili ya kusawazisha.
Straika huyo alikuwa miongoni mwa wafungaji bora wa Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka huu akilingana na Bakri Al-Madina wa El Merreikh, wote wakiwa na mabao saba, pia aliiwezesha klabu yake kutwaa ubingwa wa michuano hiyo dhidi ya USM Alger ya Algeria.
Kituo cha redio cha Clouds FM jana asubuhi kwenye kipindi cha Power Breakfast, kiliripoti taarifa ya mwanafunzi wa Tanzania anayesoma nchini Algeria pamoja na Watanzania wote wanaoishi nchini humo kuwa wamepachikwa jina la nyota huyo.
“Yaani huku kila mtu anaitwa Samatta, nchi yetu ya Tanzania imekuwa kivutio sasa kila mahali wanatuzungumzia sisi tu. Mitaani kote ukipita na ukiwa mtu mweusi au unatokea Tanzania basi wanakuita Samatta, amekuwa maarufu sana hapa.
“Ukionekana umevaa jezi ya Tanzania tu utasikia Samatta Samatta huyo anapita, yaani nchi yetu imekuwa gumzo, ni vyema mchezaji huyu akalilinda jina lake kwa kuongeza juhudi zaidi,” alisema mwanafunzi huyo.
Aliongeza kuwa: “Tunaamini timu yetu itafanya vizuri na wachezaji wetu wengine kama Mrisho Ngassa na Thomas Ulimwengu wataweza kuonyesha ushirikiano wa hali ya juu kufanikisha ushindi wetu.”
Makali ya Samatta yamemfanya awekwe kwenye orodha ya wachezaji 10 wanaowania Tuzo ya Mchezaji Bora Afrika kwa Wachezaji wa Ndani itakayotolewa mwakani, huku akipewa nafasi kubwa kuibeba.